Friday, February 11, 2011

Utetezi katika makosa ya jinai

KATIKA maada hii tutazungumzia kimsingi aina za utetezi katika makosa ya jinai.

Ni muhimu kuzieleza aina mbalimbali za utetezi katika makosa ya jinai kwa kuwa tofauti na mashauri ya madai, makosa ya jinai huandamana na adhabu kali.

Basi ni vyema jamii ikajulishwa kwa undani zaidi jinsi ya kujitetea katika makosa ya jinai.

Maana ya Jinai: Jinai au kwa jina la kitaalamu crime, ni makosa ambayo yamekatazwa na sheria kwa kuwa yana madhara makubwa kwa jamii.

Katika makosa ya aina hii, muathirika ni dola na mkosaji huadhibiwa kwa faini, kifungo au adhabu yeyote nyingine iliyoainishwa na sheria.

Hivyo makosa ya jinai yameorodheshwa katika Sheria ya Kanuni za Adhabu na sheria mbalimbali za nchi.

Makosa hayo ni kama vile wizi, ubakaji, shambulio la kudhuru mwili, jaribio la kutaka kujiua, ubakaji, kulawiti, wizi wa kutumia nguvu na mengine mengi.

Kama ilivyoelezwa, muathirika wa makosa ya jinai ni dola kwa vile dola ndilo linalobeba dhamana ya usalama wa raia.

Kwa hiyo dhamira ya kushtaki mtu aliyetenda kosa la jinai ni Jamhuri.

Hata hivyo, mara nyingine muathirika halisi wa kosa la jinai ni raia au mtu binafsi aliyetendewa kosa la wizi, mauaji au ubakaji.

Muathirika halisi wa kosa la jinai huitwa muathirika wa jinai au mlalamikaji au mhanga.

Adhabu ya makosa ya jinai. Mtu yeyote anayetiwa hatiani kwa makosa ya jinai anaweza kupewa adhabu ya faini, kifungo au vyote viwili isipokuwa kwenye makosa ya mauaji kwa kukusudia ambayo adhabu yake ni kunyongwa mpaka kufa.

Pia adhabu nyinginezo zinaweza kutolewa; kama vile adhabu ya kutoa huduma kwa jamii, mtu kutoa fidia kwa mwathirika, kuchapwa viboko, kuonywa au kukaripwa au kutumikia kifungo cha nje.

Uendeshaji wa kesi za jinai.

Katika makosa ya jinai, Jamhuri inamshtaki mtuhumiwa na kutoa ushahidi ili kuthibitisha tuhuma dhidi ya mshtakiwa.

Mshtakiwa naye anapaswa kupeleka mashahidi wake mahakamani na kutoa utetezi wake dhidi ya shitaka analotuhumiwa nalo.

Pale ambapo mahakama itaona kwamba ushahidi dhidi ya mshitakiwa ni mzito, basi mahakama itatoa kauli kwamba mshitakiwa ana kesi ya kujibu/kujitetea.

Hapa ndipo mshitakiwa atatakiwa kujitetea kwa kutoa ushahidi alionao.

Utetezi katika kesi za jinai.

Mshitakiwa anaweza kuwa ametenda kosa la jinai, na mahakama kumtia hatiani, lakini kutenda kwake kosa hilo kunaweza kuwa kumesababishwa na sababu ambazo sheria inatambua kuwa ni utetezi katika kosa hilo.

Utetezi huo ukikubaliwa mshitakiwa anaweza kufutiwa adhabu, akapunguziwa adhabu au kutopatikana na hatia.

Mazingira au sababu ambazo zinaweza kukubalika kisheria kuwa ni utetezi ni;

1. Upunguani au Kichaa (insane).

Utetezi huu hutolewa pale ambapo mshitakiwa atakuwa ametenda kosa lakini hakuwa anafahamu alichokuwa anakifanya kwa sababu ya kichaa au upunguani.

Hii ina maana kwamba alitenda kosa hilo bila kukusudia.

2. Ulevi wa kupindukia: Ulevi sio utetezi katika makosa ya jinai lakini mshitakiwa akithibitisha kwamba wakati anatenda kosa hilo alikuwa amelewa kiasi cha kutofahamu nini alikuwa anatenda, inaweza ikawa sababu ya utetezi.

Mshitakiwa anatakiwa kuthibitisha kuwa hakuwa anakusudia kunywa pombe ili atende kosa la jinai.

3. Kukosea ukweli: Kuna mazingira fulani fulani ambapo mtu anaweza kutenda kosa la jinai kwa kukosea ukweli.

Mfano wakati wa usiku katika maeneo ambayo yana Nguruwe pori ambao hushambulia mazao ya wakulima; mlinzi aliona mitikisiko ya mpunga akapiga tochi kwenye eneo hilo na kuita kwa kusema kuna mtu hapa? lakini hakuna aliyejibu na kutokana na ufinyu wa mwanga wa tochi yake hakuona kama kulikuwepo watu waliokuwa wakifanya mapenzi, basi mlinzi huyo alirusha mkuki katika eneo lililokuwa na kitu cheusi akidhani alikuwa anamlenga Nguruwe kumbe ukweli ni kuwa yule hakuwa Nguruwe bali walikuwa watu waliokuwa wakifanya mapenzi pale kwenye mpunga.

Mkuki ulimpata mwanamme ambapo alikufa papo hapo.

Katika mazingira haya utetezi kwamba mshtakiwa alikosea ukweli unakubalika na mahakama itamuachia huru mshitakiwa.

4.Kulinda mali, nafsi yako mwenyewe au nafsi ya mwingine: Sheria ya makosa ya jinai inakubali utetezi kuwa mshitakiwa aliua au alijeruhi kwa kujilinda mwenyewe/kutetea nafasi yake au kulinda na kutetea mali yake au kumlinda na kumtetea mtu mwingine dhidi ya uovu wowote ule ambao sheria imeukataza, utetezi huu utakubaliwa na mahakama itamwondolea mshitakiwa wa jinai hii adhabu na hatia.

Hata hivyo, utetezi huu una mipaka yake yaani matumizi ya nguvu dhidi ya uvamizi anaofanyiwa mtu au mali yake yasizidi kipimo.

Ieleweke kuwa, mtuhumiwa hapaswi kutumia nguvu kupita kiasi katika kujibu shambulizi lolote dhidi yake au mali ya mwajiri wake au dhidi yamali yake.

Kwa mfano mtu akikushambulia kwa bakora au jiwe si sahihi kujibu mapigo kwa kutumia bunduki au bastola.

Iwapo mshambuliaji atatumia bunduki au bastola, basi mahakama itaona kuwa matumizi ya bunduki na bastola kujibu mapigo ya bakora au jiwe ni kutumia nguvu kupita kiasi.

5.Kuchukizwa kupita kiasi (Provoke): Kuchukizwa kupita kiasi ni utetezi dhidi ya kosa la jinai kama vile kuua au kujeruhi.

Ili mshitakiwa aweze kukubaliwa ushahidi wake kuwa alikuwa amechukizwa kupita kiasi lazima athibitishe mambo yafuatayo, (i) kwamba alitendewa tendo kiovu na cha kudhalilisha, ambacho kilimdhalilisha yeye binafsi au mtu yeyote ambaye ana husiano naye wa karibu mfano; mzazi wake, mke au mume, dada au kaka, mtoto, mwajiri au mtumishi. (ii) kitendo cha kupandisha hasira kiwe ni cha hali ya juu yaani kama ni maneno yawe makali sana na ya kuudhi au kumdhalilisha mtu katika mambo fulani na kitendo kiwe cha papo kwa hapo yani ghafla ambapo mtu anakosa muda kwa kutuliza hasira. (c) awe amepatwa na hasira kupita kiasi kwa jinsi kwamba alipoteza uwezo wa kujitawala nafsi yake.

Mfano mshitakiwa anapojitetea kuwa alimfumania mkewe au mumewe akifanya mapenzi na mtu mwingine na hivyo akachukua hatua ya kumpiga na kumjeruhi vibaya huyo mtu mwingine au mwanandoa mwenzake, mahakama inaweza kuukubali utetezi huo kwa kuangalia uhusiano wa karibu uliopo kati ya wanandoa.

Utetezi utakubalika tu iwapo mshitakiwa atakuwa ametenda tendo la kupiga na kujeruhi muda huo huo bila kukawia alipo wafumania wahusika yaani hapo kwa hapo.

Katika mazingira hayo yaliyotajwa hapo juu mshitakiwa anaweza akaachiwa huru na mahakama au kupunguziwa adhabu kwa utetezi huo.

7.Umri: Mshitakiwa aliye chini ya umri wa miaka 10 hawezi kushtakiwa kwa kosa la jinai.

Na iwapo ana miaka 12 mahakama haitamhukumu hadi itakapohakikisha kuwa alitenda kosa hilo kwa kukusudia au alikuwa na nia ovu.

Mtoto wa kiume wa miaka chini ya 12 ana hesabika kutokuwa na uwezo wa kutenda kosa la kujamiiana.

8.Kushurutishwa: Mshitakiwa anaweza kujitetea kuwa alishurutishwa na wenzake kutenda kosa la jinai kwa kutishiwa kuuawa au kuumizwa.

Mahakama haitaukubali utetezi iwapo tishio la kuuwa au kuumizwa ni la wakati ujao.

9.Nia njema: Mshitakiwa anaweza kujitetea kuwa alitenda kosa la jinai lakini alikuwa na nia njema.

10.Kinga ya kisheria: Mtu ambaye amekingwa na sheria kwa makosa ya jinai kutokana na wadhifa wake hatashitakiwa kwa makosa ya jinai au akishitakiwa anaweza kujitetea kuwa anayo kinga ya kisheria kwa mfano, hakimu au jaji yeyote hatashitakiwa kwa kosa lolote ambalo atalifanya akiwa katika utekelezaji wa kazi yake.