Monday, June 21, 2010

Pindi tukizishinda changamoto hizi hakuna mtu atakaebakia pembezoni

Na Juma Khamis

KILA ifikapo May 9 ya kila mwaka, Umoja wa Ulaya (EU) huadhimisha siku yake kukumbuka siku ambayo Robert Schuman aliwasilisha pendekezo la kuundwa Muungano wa Ulaya mwaka 1950.

Pendekezo hilo lililopewa jina la "Azimio la Schuman", linachukuliwa kama mzizi uliosababisha kuuundwa kwa Umoja wa Ulaya.

Siku hii huadhimishwa kwa shughuli mbali mbali pamoja na matamasha yanayowakutanisha pamoja raia kutoka Muungano huo.

Siku hiyo pia huadhimishwa katika mataifa mbali mbali duniani, ambayo EU ina ushawishi wake ikiwemo Zanzibar.

Kwa mwaka 2010 Zanzibar ilikuwa mwenyeji, ambapo shughuli mbali mbali za maendeleo ya wananchi ambazo zinaungwa mkono na EU zilipewa kipaumbe cha kwanza.

Kwa mfano Balozi wa EU nchini Tanzania Tim Clarke, alipata fursa ya kukagua miradi ya kilimo katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar, pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wakulima na wananchi kwa ujumla.

Clarke pia alipata fursa ya kusikiliza vilio kutoka kwa wananchi moja kwa moja au kupitia taasisi zinazowakilisha watu wanaoishi pembezoni, ambao idadi yao ni kubwa zaidi.

Licha ya jitihada kubwa zinazochukuliwa na EU, kuanzisha miradi mbali kwa lengo la kuwakomboa watu waliosahaulika, bado tatizo limebakia pale pale; matajiri wanaendelea kunawiri kwa utajiri na maskini wanaendelea kudidimia katika dimbwi la umaskini.

Tatizo ni kwamba miradi mingi inapoanzishwa na kuwa chini ya ufadhili, inawawia vigumu wananchi kuiendeleza baada ya mfadhili kuondoka.

Tatizo hili limejitokeza katika miradi kadhaa, ambayo sasa imekufa kabisa huku faida yake kwa wananchi ambao ndio walengwa ikiwa haionekani.

Tatizo jengine ni wananchi kutoshirikishwa kwa ukamilifu katika miradi husika huku wakipewa asilimia ndogo sana ya uendeshaji wa miradi.

Wao hawana nguvu ya kutumia fedha za miradi badala yake kutakiwa kuomba miradi kwa watu ambao walitakiwa tu kuwa wasimamizi na sio waendeshaji.

Changamoto zinazowakabili watu walioko pembezoni ni nyingi na zinaonekana katika mataifa mbali mbali duniani, lakini athari zaidi inajotokeza katika nchi maskini Zanzibar ikiwa miongoni mwao.

Makundi yaliyo pembezoni bado hayajaonekana ipasavyo na hayafikiwi na rasilimali muhimu za taifa (national cake) au zinawafikia kwa asilimia ndogo ambazo hazikidhi mahitaji yao wala hazitoshelezi kutoka na wingi wao.

Kwa mfano, vijana ambao ndio watu muhimu katika jamii bado wanakabiliwa matatizo makubwa ikiwemo upungufu wa ajira, ambapo zaidi ya asilimia 70 ya vijana hawana ajira za uhakika za kujipatia kipato.

Hali hii huwafanya wengi wao kujitumbukiza katika makundi maovu ya kutumia dawa za kulevya, wizi wa kutumia nguvu na ubakaji.

Ni kweli wizi haukubaliki katika jamii lakini kama kijana huyu angeandaliwa mazingira bora, bila shaka asingekuwa na muda wa kufanya uhalifu.

Lakini pia lazima ifike muda tukubali kuwa mfumo wetu wa elimu, haumsaidii kijana kujitegemea baada ya kumaliza shule.

Wapo wengi ambao wamemaliza elimu ya juu (shahada), lakini hawana kazi za kufanya na badala yake wanaendelea kuwa tegemezi kwa wengine.

Unyanyasaji mkubwa pia unaonekana kushamiri kwa wafanyakazi wa nyumbani, ambao daima wamekuwa wakilalamika lakini maskini sauti zao hazisikilikani na kama vile wameshindwa na mtu wa kuwatetea.

Hawa ni waathirika wa kulipwa mishahara midogo tena isiyo zingatia wakati, kiwango kidogo cha elimu, pamoja na udhalilishaji wa kimapenzi unaofanywa na waajiri.

Baba mwenye nyumba haoni tabu kumuomba penzi mfanyakazi wake wa ndani na kutishia kumfukuza pale anapokataa ‘kumuhudumia’.

Tatizo hili linaweza kuondoka tu kwa kuandaa mikataba kwa wafanyakazi wa ndani, kwa sababu kama zilivyo sekta nyegine sekta hii nayo ni muhimu.

Kundi jengine lililosahaulika ni la watu wenye ulemavu; kundi hili bado halifaidiki na mfumo wa elimu ulipo sasa, unyanyasaji unaofanywa na madereva, lakini pia mfumo wa miundombinu unaonekana haukuwazingatia watu wenye ulemavu.

Kwa mfano barabara hazijatengwa kwa watu wenye ulemavu, hali ambayo huwafanya kugongwa na madereva wazembe.

Changamoto nyengine zinazowakabili watu waliosahaulika ni kukithiri kwa matukio ya ubakaji kwa watoto wadogo, utelekezaji wa familia, upungufu wa miradi kwa wajasiriamali na ukosefu wa sheria zinazozingatia wakati na mazingira halisi yaliyopo sasa.

Kama kweli tutazimaliza changamoto hizi ni dhahiri hakuna mtu atakaebakia pambezoni.

Mwinyihaji aitaka Zantel iwasaidieni wananchi vijijini kunufaika na huduma za kibenki

Na Juma Khamis

WAZIRI wa Nchi (AR) anaeshughulikia fedha na uchumi, Dk. Mwinyihaji Makame, ametoa wito kwa kampuni ya simu za mkononi ya Zantel kuimarisha zaidi huduma zake hasa kwa watu wa vijijini Unguja na Pemba, ambao licha ya kuwa na simu za mkononi lakini wamekuwa wakishindwa kunufaika na huduma za kibenki.

Dk. Mwinyihaji aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi mpya wa huduma za Z- PESA inayotolewa na Zantel.

Alisema watu wa vijijini bado hawajanufaika vya kutosha na huduma za kibenki na kusema muda umefika sasa kwa Zantel kuwafikia kwa upana na haraka zaidi ili na wao waweze kufaidika na huduma hizo.

Kwa mfano alisema utumaji na upokeaji fedha kwa mfumo wa Z-PESA utawasaidia watu wa vijijini kupokea fedha kutoka kwa jamaa zao walioko nje ya Zanzibar kwa wepesi badala ya kwenda kupanga foleni benki ambazo zote zipo mijini.

Aidha alisema kwa kufanya hivyo, lile lengo la serikali la kupunguza umaskini kwa wananchi litaweza kufikiwa.

Waziri Mwinyihaji aliipongeza Zantel kwa kuendelea kuchangia huduma za maendeleo nchini na kuwa walipa kodi wa mwanzo nchini.

Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa Zantel Noel Herrity, alisema Zantel kupitia mfumo wa Z- PESA imekusudia kubadili kabisa maisha ya Wazanzibari.

Herrity alisisitiza umuhimu wa kuleta karibu huduma za kibenki kwa wananchi walio wengi ambao hawapati huduma za kibenki ingawana wana simu za mkononi.

“Zantel tunafahamika kama kampuni bunifu ambayo inajitahidi kuwawezesha Watanzania kupata huduma za mawasiliano zilizo nafuu na katika mfumo huu wa Z PESA tutawaletea wateja wetu huduma za kibenki hasa wale ambao hawana fursa za kupata huduma hizo,” alisema Herrity.

Huduma hiyo za Z PESA imeongezewa huduma mpya ambazo zitawawezesha wateja wa Zantel Zanzibar kulipia na kununua bidhaa tofauti kama umeme maji, tiketi za ndege , kulipia DSTV (cable) pamoja na kutuma na kupokea fedha.

Afisa Mkuu wa Biashara wa Zantel, Norman Moyo alisema katika kufanikisha mfumo huo, Zantel imewahusisha wafanyabiashara, vyama pamoja na makundi yenye wanachama waliosambaa sehemu mbali mbali nchini kuwa mawakala wa Z -PESA.

“Zantel inawawezesha wafanyabiashara ndogondogo kukuza biashara zao katika maeneo mbali mbali ambayo hayajafikiwa na huduma za benki pamoja na kuwaongezea kipato,” alisema Moyo.

Huduma hizo mpya sasa itawawezesha Wazanzibari wenye ndugu zao ndani na nje ya nchi kupokea fedha kwa haraka zaidi.

Hata huvyo, watu waliohudhuria uzinduzi wa mfumo huo, wamesema elimu juu ya matumizi ya mfumo huo inapaswa kutolewa hasa kwa watu wa vijijini, vyengine mfumo unaweza kukosa uungwaji mkono.

“Bado mfumo ni mgumu na kama kweli Zantel wamedhamiria kuwasaidia kibenki hasa kwa watu wa vijijini wanapaswa kupita kila sehemu kutoa elimu kwa wateja wao,” walisema.

Serikali ya Mapindunzi ya Zanzibar inamiliki asilimia 18 ya hisa katika kampuni hiyo.

Balozi Karume: Kura yangu ya ndio au hapana itategemea nani atateuliwa kugombea Urais CCM

Na Juma Khamis
BALOZI wa Tanzania nchini Italia, Ali Abeid Amani Karume (60), amesema kura yake ya NDIO au HAPANA katika kura ya maoni kuamua mfumo wa uendeshaji serikali, itategemea nani atapitishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) Julai 9 kuwa mgombea Urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao.

Kura ya maoni kuhusu mfumo wa serikali itafanyika Julai 31, takribani siku 20 baada ya CCM kuchagua mgombea wake wa Urais.

Balozi Karume aliyasema hayo hoteli ya Serena alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa kutoka chama chake kuteuliwa kuwa mgombea Urais wa Zanzibar.

“Tufikirie kwa makini kabisa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa na mimi hili naliunga mkono lakini kura yangu ya NDIO au HAPANA itategemea mgombea wa Urais wa CCM atatoka upande upi,” alisema Karume.

Hata hivyo, alisema ni matarajio yake kwamba CC itawatendea haki wagombea wote na kuchagua mwanachama ‘asilia’ wa Zanzibar kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar.

“Tutashinda tukichagua kiongozi bora na si bora kiongozi,” alisema Balozi Karume huku akisisitiza kuwa kama atapitishwa na kushinda basi wala rushwa wataendelea tu kubakia na utaifa wa Zanzibar lakini wajiandae kutafuta nchi yao ya kuishi, akimaanisha kwamba atakabiliana kwa nguvu zake zote na mafisadi.

Akizungumzia nia yake ya kugombea kuteuliwa katika nafasi ya Urais, Balozi Karume ambae ni mdogo wa Rais wa sasa wa Zanzibar Amani Abeid Karume alisema: “Nimechangia vya kutosha Tanzania na sasa muda umefika kucha kuchangia nchini kwangu. Nia ninayo, sababu ninayo na uwezo ninao, nakiomba chama kinipitishe.”

Balozi Karume ambae ana kadi ya CCM No. AA 270259 aliyoipata Februari 5, 1977 msukumo mkubwa anaojivunia ni kuungwa mkono na vijana hasa wanawake.

“Kabla ya kuchukua fomu nimeshauriana na wengi wakiwemo Marais wastaafu lakini msukumo nilioupata zaidi ni kutoka kwa vijana na hasa wanawake,” alisema Karume ambae ni mtoto wa pili wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Balozi Karume ambae ana Shahada ya Uzamili (Master Degree) kutoka Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani, aliwahi kusoma pamoja chuoni hapo na Rais wa sasa wa Marekani, Barack Obama wakati huo akichukua shahada ya kwanza aliyopita baada ya kutunukiwa Schorlaship na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1978.

Obama alikuwa nyuma yake kwa mwaka mmoja.

Wakati akichukua fomu, Balozi Karume ambae alikuwa karibu na Mabaunsa na mkewe ambao hata hivyo chanzo kimoja cha habari kilisema ni watoto wake, alisema atahakikisha anapata wadhamini kutoka mikoa yote mitano ya Zanzibar, ingawa sheria kwa kumgombea Urais ni kuwa na wanachama 250 kutoka mikoa mitatu ya Zanzibar.