Monday, June 21, 2010

Mwinyihaji aitaka Zantel iwasaidieni wananchi vijijini kunufaika na huduma za kibenki

Na Juma Khamis

WAZIRI wa Nchi (AR) anaeshughulikia fedha na uchumi, Dk. Mwinyihaji Makame, ametoa wito kwa kampuni ya simu za mkononi ya Zantel kuimarisha zaidi huduma zake hasa kwa watu wa vijijini Unguja na Pemba, ambao licha ya kuwa na simu za mkononi lakini wamekuwa wakishindwa kunufaika na huduma za kibenki.

Dk. Mwinyihaji aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi mpya wa huduma za Z- PESA inayotolewa na Zantel.

Alisema watu wa vijijini bado hawajanufaika vya kutosha na huduma za kibenki na kusema muda umefika sasa kwa Zantel kuwafikia kwa upana na haraka zaidi ili na wao waweze kufaidika na huduma hizo.

Kwa mfano alisema utumaji na upokeaji fedha kwa mfumo wa Z-PESA utawasaidia watu wa vijijini kupokea fedha kutoka kwa jamaa zao walioko nje ya Zanzibar kwa wepesi badala ya kwenda kupanga foleni benki ambazo zote zipo mijini.

Aidha alisema kwa kufanya hivyo, lile lengo la serikali la kupunguza umaskini kwa wananchi litaweza kufikiwa.

Waziri Mwinyihaji aliipongeza Zantel kwa kuendelea kuchangia huduma za maendeleo nchini na kuwa walipa kodi wa mwanzo nchini.

Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa Zantel Noel Herrity, alisema Zantel kupitia mfumo wa Z- PESA imekusudia kubadili kabisa maisha ya Wazanzibari.

Herrity alisisitiza umuhimu wa kuleta karibu huduma za kibenki kwa wananchi walio wengi ambao hawapati huduma za kibenki ingawana wana simu za mkononi.

“Zantel tunafahamika kama kampuni bunifu ambayo inajitahidi kuwawezesha Watanzania kupata huduma za mawasiliano zilizo nafuu na katika mfumo huu wa Z PESA tutawaletea wateja wetu huduma za kibenki hasa wale ambao hawana fursa za kupata huduma hizo,” alisema Herrity.

Huduma hiyo za Z PESA imeongezewa huduma mpya ambazo zitawawezesha wateja wa Zantel Zanzibar kulipia na kununua bidhaa tofauti kama umeme maji, tiketi za ndege , kulipia DSTV (cable) pamoja na kutuma na kupokea fedha.

Afisa Mkuu wa Biashara wa Zantel, Norman Moyo alisema katika kufanikisha mfumo huo, Zantel imewahusisha wafanyabiashara, vyama pamoja na makundi yenye wanachama waliosambaa sehemu mbali mbali nchini kuwa mawakala wa Z -PESA.

“Zantel inawawezesha wafanyabiashara ndogondogo kukuza biashara zao katika maeneo mbali mbali ambayo hayajafikiwa na huduma za benki pamoja na kuwaongezea kipato,” alisema Moyo.

Huduma hizo mpya sasa itawawezesha Wazanzibari wenye ndugu zao ndani na nje ya nchi kupokea fedha kwa haraka zaidi.

Hata huvyo, watu waliohudhuria uzinduzi wa mfumo huo, wamesema elimu juu ya matumizi ya mfumo huo inapaswa kutolewa hasa kwa watu wa vijijini, vyengine mfumo unaweza kukosa uungwaji mkono.

“Bado mfumo ni mgumu na kama kweli Zantel wamedhamiria kuwasaidia kibenki hasa kwa watu wa vijijini wanapaswa kupita kila sehemu kutoa elimu kwa wateja wao,” walisema.

Serikali ya Mapindunzi ya Zanzibar inamiliki asilimia 18 ya hisa katika kampuni hiyo.

No comments:

Post a Comment