Monday, January 31, 2011

Bado sekta ya utalii inahitaji kuangaliwa zaidi

ZANZIBAR kwa kiasi kikubwa inategemea mchango wa sekta ya utalii katika pato lake la taifa, sekta ambayo imeamza kuimarika nchini.

Sekta hiyo inatoa mchango mkubwa kwa sababu ni sekta inayoweza kukua na kutumika kuwavutia wageni kutoka nje kutokana na historia ya nchi na pia mnasaba wake kwa wageni kuwa sehemu ya vivutio vya wageni hao.

Ni jambo la kujivunia kuona kuwa tangu serikali ilipoanzisha sekta hiyo miaka kadha sasa, imeweza kuongeza pato linalotokana na utalii huku hoteli nazo zikiongezeka, hali inayowafanya wageni wengi kuja nchini.

Kama ilivyo kwa sekta nyengine za kuchangia uchumi sekta hiyo pia inakumbwa na matatizo ya hapa na pale kwa sababu inawahusisha binadamu hivyo haiwezi kukosa misuko suko ndani yake.

Hivi sasa kuna malalamiko mengi ndani ya sekta hiyo lakini mengi yanaweza kutatuliwa kwa sababu yanafanywa na binadamu.

Wapo wanaolalamika kukoseshwa ajira katika hoteli za kitalii na badala yake ajira nyingi zimeelekezwa kwa wageni ambao nao pia ni wengi kijumla katika ajira hizo huku wananchi na hasa wazalendo wanaotoka kwenye vijiji vya jirani wakishuhudia.

Matatizo mengine makubwa ambayo ni mazungumzo ya kila siku ni udhaifu unaofanywa na wawekezaji wa kuwadhulumu wafanyakazi mafao yao pamoja na kuwadhalilisha katika kazi hizo na hasa pale wanapodai mishahara yao ambayo hulipwa bila kuzingatia sheria zinazosimamia kazi hiyo.

Kwa kawaida migogoro ya namna hiyo hutakiwa ifanyiwe marekebisho haraka mara baada ya wahusik kufikisha malalamiko yao kwenye vyombo husika.

Pamoja na kuwepo miongozo na sheria za kuzingatiwa lakini wafanyakazi hao wamekuwa wakihangaishwa sana na waajiri na inapotokea kufikisha malalamiko yao katika ngazi ya juu basi hufukuzwa kazi ama kurudishwa kazini kwa kuajiriwa bila mikataba.

Kero hizo zimekuwa zikisikika kila mara lakini maamuzi yanayofikiwa huwa ya kubabaishwa kutokana na uhusiano uliopo kati ya viongozi na waajiri wa hoteli, hali inayonesha mara nyingi kuwepo kwa harufu ya rushwa ndani yake.

Baadhi ya maofisa wanmaopewa jukumu hilo hushirikiana na wageni “kuwanyonga” wenyeji wanapokwenda kudai haki hizo.

Jambo hilo limejitokeza kuwa sehemu ya vikwazo vinavyochangia kasoro zinazojitokeza mara kwa mara katika sekta ya utalii.

Hali hiyo mara kadha imekuwa chanzo cha wamiliki wa hoteli kuikoseha mapato serikali kwa kushirikiana na maofisa wazalendo katika taasisi za umma.

Ninadhani matukio ya udhalilishaji wa aina mbali mbali ni mengi katika sekta hiyo lakini hayafikii mbali kwa vile watetezi wa wafanyakazi hao wanaangalia zaidi maslahi yao badala ya muajiri wake na kutowahurumia ndugu zao wanopata madhila mbele ya wageni.

Hivyo,ni jukumu la serikali sasa kutafuta wawekezaji wenye uwezo wanaoweza pia kuwathamini wafanyakazi wao ambao ndio msingi wa mapato yao ya kila siku.

Hivi hali hii ya kunyanyaswa wafanyakazi wetu itaendelea hadi lini, kwani inalalamikiwa vya kutosha lakini wawekezaji inaonekana hawashtuki kutokana na “kubebwa” na maofisa wasiokuwa waaminifu katika serikali.

Pamoja na hayo, pia kuna haja kwa serikali kuendelea kuitupia macho sekta hiyo, kwa jumla ikiwa ni pamojana kuangalia kiwango cha ukusanyaji wa mapato kama kinakwenda sambamba na hali halisi ya makusanyo.

Wafanyakazi mahoteli walia mishahara yao kucheleweshwa kupindukia

WAFANYAKAZI wengi wa mahoteli hulipwa mishahara yao katikati ya mwezi mwengine wa kazi hali ambayo huwasababishia kuishi katika maisha magumu wao na familia zinazowategemea.

Wakizungumza katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi, wafanyakazi wa mahoteli yaliyopo ukanda wa mashariki katika mkoa wa kaskazini Unguja, wamesema mara nyingi hulipwa mishahara baina ya tarehe 10-15 ya mwezi mwengine wa kazi.

Walisema sababu ya kuchelewa haijulikani kwani mahoteli yanakuwa yamesheni wageni lakini wanapojaribu kuulizia huambiwa anaetaka kazi astahamili na asietaka aondoke.

Aidha, hata pale inapolipwa mishahara hiyo huwa pungufu, wakimaanisha kuwa mshahara wa mwezi mmoja haulingani na mwezi mwengine.

“Inawezekana ikatokea mwezi mmoja ukalipwa pesa nyingi, mwezi unaofata ukapunjwa kwa kweli hatuji sababu,” alisema Zainab Kombo, mfanyakazi wa jikoni katika hoteli moja iliyopo Kiwengwa.

Hata hivyo, Juma Kombo,alisema kupunjwa huko mara nyingi hufanywa na wahasibu au washika fedha wa mahoteli, ambao mara nyingi huwa ni wazalendo.

“Meneja wa hoteli huwa ameshatenga kiwango maalum cha mshahara wa wafanyakazi lakini wahasibu na washika fedha ndio wanaozikata, kile cha juu huchukua wao. Sisi katika hoteli yetu tumegundua kuwa kuna vocha mbili za mishahara,” alisema.

Lakini baadhi ya wahasibu wa mahoteli waliozungumza na gazeti hili, wamekanusha wakisema kuwa mishahara wanayolipa ndiyo ile iliyokubaliwa wakati wafanyakazi wa wakisaini mikataba, lakini walikiri kwamba wakati mwengine inaweza kushuka kutoka na mahudhurio ya mfanyakazi kazini.

Changamoto hizo pamoja na zile za kunyanyaswa, zimekuwa zikiwafanya wafanyakazi wa mahoteli wakati mwengine kufanya matukio ya wizi na kuwashambulia waajiri wao.

Hivi karibuni, mfanyakazi mmoja katika hoteli moja ya kitalii, alimshambulia mwajiri wake alietajwa kwa jina la Marina baada ya kumtukana na kumfananisha na mnyama.

Katika tukio hilo mfanyakazi huyo alidaiwa kusahau ufunguo kwenye debe la taka na hata baada ya kuomba radhi, bosi huyo aliendelea kumshambulia kwa maneno ya kashfa na kumzaba makofi pamoja na kumchania mkoba wake jambo lililomtia hasira na kuanza kumshambulia mwajiri wake.

Mfanyakazi huyo amefukuzwa kufanya kazi katika hoteli hiyo.

Akizungumzia suala la unyanyasaji, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya wafanyakazi wa utalii, mahoteli, hifadhi, majumbani na kazi nyengine (ZATHOCODAWU), Maalim Makame Launi, amesema wafanyakazi wa mahoteli wamekuwa wahanga wa manyanyaso, kupunjwa mishahara na kutolipwa kwa wakati, kufukuzwa kazi ovyo na kutopewa mikata hali ambayo inakwamisha juhudi za serikali za kuimarisha sekta ya utalii na kupunguza umaskini.

Alisema wamekuwa wakisimamishwa kazi na mikataba yao kuvunjwa wakati mwengine bila sababu za msingi lakini vyama vyao vinashindwa kuwafikia kwa kuwatetea kwa sababu wengi si wanachama.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilah Jihad Hassan, alisema serikali sasa inakusudia kuwanyang’anya leseni wawekezaji wanaokiuka sheria za utalii.

Nae Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi amesema serikali haitavumilia wawekezaji wasio waaminifu ambao wmaekuwa wakisababisha umaskini kwa wananchi.

Alisema kwa mfano mmiliki wa hoteli ya kitalii ya Venta Club iliyopo Kiwengwa ameitelekeza hoteli hiyo tokea mwezi Machi mwaka uliopita na kuacha madeni makubwa kwa wafanyakazi na watu waliokuwa wakipeleka bidhaa zao linalofikia shilingi milioni 400 pamoja kodi ya shilingi milioni 600.

Tayari vifaa kadhaa katika hoteli hiyo ikiwemo milango vimeibwa ikiaminika kuwa ni jaribio linalofanywa na wafanyakazi waliokuwa wakitumikia hoteli hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mselem Mtulya amethibitisha kukamatwa kwa vitu kadhaa vilivyoibwa katika hoteli hiyo.

Akizungumzaia masuala ya unyanyasaji, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad amesema serikali haiko tayari kuwavumilia wawekezaji wanaowanyanyasa wafanyakazi katika sekta ya utalii.

Alisema serikali haitawavumuliwa wawekezaji wenye tabia hiyo wakiwa wa nje au wa ndani ambapo kwa kufanya hivyo watakuwa wanavunja sheria.

Alisema serikali itatoa ushirikiano mkubwa kwa wawekezaji kuja kuwekeza Zanzibar lakini haitaridhika kuona wafanyakazi wake wakinyanyaswa.

Friday, January 21, 2011

Ni kosa kwa mwari kupata ujauzito hata kwa hiari yake

Na Juma Khamis
SHERIA ya kuwalinda wari na watoto wa mzazi mmoja, ni moja ya sheria nyingi zilizotungwa na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Sheria hii ilitungwa kutokana na kukithiri kwa matukio ya udhalilishaji wa wari na watoto wadogo, lengo likiwa ni kukomesha unyanyasi huo hapa nchini.

Kabla ya kuja kwa sheria hiyo, idadi kubwa ya watoto na wari walikuwa wakinyanyasika bila ya kuwepo sheria mahasusi ya kuwatetea.

Hata hivyo, licha kuwepo sheria hii, lazima tukiri kwamba bado vitendo vya kuwadhalilisha wari na watoto vimekuwa vikiendelea, huku wari wengi wakipewa ujauzito na kuishia kuolewa huku wakipoteza fursa nyingi muhimu kwa maisha yao, ikiwemo elimu.

Sheria hii inaelezea kwa kina makosa mbali mbali ya jinai ambayo hayakuelezwa na sheria ya makosa ya Jinai (Penal Act No.6 ya mwaka 2004).

Kabla ya kuzungumzia baadhi ya makosa ya jinai katika sheria hii, kwanza tuone maana ya ‘mwari’ kama mmoja ya mlengwa wa sheria hii.

Kwa mujibu wa kifungu cha pili cha sheria hii, mwari ni mwanamke asiepata kuolewa ambaye yuko baina ya umri wa miaka 18 na miaka 21 na asiyepata kuzaa mtoto.

Baadhi ya makosa yanayotambuliwa na sheria hii ni pamoja mwari atakaepatikana na ujauzito ambao ameupata kwa hiari yake.

Adhabu katika kosa hili iwapo atatiwa hatiani ni kutumikia jamii kwa kipindi cha kuanzia miezi mitatu tokea siku aliyojifungua.

Sheria hii pia imebainisha kuwa mtu yeyote atakaehusika na ujauzito wa mwari huyo atakuwa amefanya kosa na pindi atakapotiwa hatiani adhabu yake ni kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu na si zaidi ya miaka mitano.

Pamoja na adhabu hiyo atatakiwa atoe matunzo kwa mtoto atakaezaliwa na mwari huyo.

Sheria pia imesema kuwa ni jukumu la mwari yeyote atakaekuwa mjamzito kutaja jina la mtu aliempa ujauzito huo na pindi mwari huyo atakataa kutaja jila mtu huyo atakuwa ametenda kosa la jinai na endapo atatiwa hatiani adhabu yake ni kutumikia jamii kwa kipindi cha miezi mitatu.

Hata hivyo, itakuwa ni kinga kwa mwari huyo kama atathibitisha kuwa ujauzito huo ameupata kutokana na kubakwa na watu wengi au mazingira mengine ambayo hakuweza kumtambua mbakaji.

Iwapo mwari huyo kwa makusudi amemtaja mtu tofauti na aliyemsababishia ujauzito huo, na kama mahakama itaridhika amefanya hivyo kwa makusudi, atakuwa ametenda kosa la jinai na akipatikana na hatia atatumikia jamii kwa kipindi cha miezi sita.

Ni kosa la jinai kwa mtu mwenye mamlaka ofisini kufanya tendo la ndoa na mtu wa chini yake

Na Juma Khamis
KWA kipindi kirefu kati ya miaka ya 1996 hadi mwanzoni mwa mwaka 1998, Tanzania kama nchi ilishuhudia kuongezeka kwa kiasi kikubwa makosa ya jinai yanayohusiana na ngono.

Kwa wengi waliokuwa wakifuatilia vyombo vya habari walikuwa mashahidi wa kile wanasheria wa makosa ya jinai wanachokiita crime rate, kukua kwa kiasi cha kutisha.

Hata hivyo, mwaka 1998 Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania lilitunga sheria inayoitwa Sheria Maalumu ya Makosa ya Kujamiiana au kwa lugha ya kigeni ‘Sexual Offences Special Provisions Act’ au kwa kifupi SOSPA.

Sheria hii ilitiwa saini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Benjamin Mkapa Julai mwaka 1998.

Kwa kiasi kikubwa sheria hii ilikuwa kama shubiri wa tatizo la makosa ya kujamiiana kama ubakaji au kufanya ngono kinyume cha maumbile katika jamii yetu.

Leo tutaiangalia sheria hii, yaliyomo, adhabu zake na mabadiliko katika sheria hii.

Kwa kiasi kikubwa, sheria hii imekuja kufanya mabadiliko katika sheria kadhaa za makosa ya jinai kama vile Kanuni ya Adhabu (sura ya 16 ya sheria za Tanzania) Sheria ya Ushahidi na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Hivyo sehemu ya kwanza ya sheria hii imefanya mabadiliko katika sheria ya kanuni za adhabu.

Ndani ya sheria hii mvulana ametambuliwa kama mwanamme aliye chini ya miaka 18.

Hii ina maana kwa mtoto wa kiume kutambulika kama mtoto, umri wake ni lazima uwe chini ya miaka 18, wakati kwa msichana, yeye ametambulishwa kama mwanamke aliye chini ya miaka 18 pia.

Chini ya kifungu cha 4 cha sheria hii, kanuni ya adhabu imefanyiwa marekebisho na kwa sasa kwa mtoto ambaye ‘hajakomaa’ (immature) umri wake ni ule ulio chini ya miaka 10.

Kisheria, mtoto huyo hawezi kuwa na mashitaka wala hatia ya makosa ya jinai hata hivyo, marekebisho yaliyofanyika kwenye kifungu kidogo cha 2 cha kifungu cha 15 cha kanuni za adhabu, kinaelekeza kwamba mtoto aliye chini ya miaka 12 hawezi kuwa na hatia ya kosa la jinai isipokuwa kama wakati anatenda au anaacha kutenda tendo (ambalo ni jinai), itathibitishwa kwamba alikuwa na uwezo wa kujua kwamba hatakiwi kutenda au kutokutenda kosa hilo.

Pia kifungu hiko kinamtoa hatiani kwa kosa lolote la jinai mtoto wa kiume aliye chini ya miaka 12 kwa dhana kwamba hawezi kufanya tendo la ngono, kubaka.

Tofauti na wengi wanavyodhani kwamba kubaka ni tendo la kumlazimisha mwanamke kufanya mapenzi, sheria hii imetoa maana pana ya neno kubaka.

Chini ya kifungu cha 5 cha sheria hii, ambacho kimetengeneza kifungu cha 130 cha Kanuni za Adhabu inasomeka kwamba kubaka ni kitendo cha mtu mwanamme kufanya tendo la ndoa na mwanamke bila idhini au kitendo cha kufanya tendo la ndoa na mwanamke ambaye si mke wake au mke wake lakini waliye tengana naye na bila idhini yake; au kwa idhini yake ambayo imepatikana kwa kutumia nguvu, vitisho.

Au kwa kuweka maisha yake katika hofu ya kifo, kuumia, akiwa katika kifungo au kwa idhini yake lakini idhini hiyo ikiwa imepatikana akiwa katika akili iliyochanganyikiwa kama amelewa kwa dawa aliyopewa na mwanamme huyo, isipokuwa endapo itathibitika kwamba kulikuwa na makubaliano awali, mwanamme atahesabika kuwa amebaka kama atafanya tendo la ndoa na msichana aliye chini ya miaka 18 hata kama msichana huyo atakuwa amekubali kufanya tendo la ndoa kwa ridhaa yake.

Pengine kwa kutambua kwamba kuna aina nyingine za ubakaji, sheria hii chini ya kifungu cha 5 kifungu kidogo cha 3 imetoa maana nyingine zaidi ya kubaka kwa kujumuisha maana hiyo kwa kitendo cha mtu mwenye mamlaka katika ofisi anapofanya tendo la ndoa na mtu wa chini yake kimamlaka au pale ofisa mahabusu zilizoanzishwa kisheria atakapofanya ngono na mahabusu mwanamke.

Maana nyingine ya kubaka ni pale maofisa wa afya au hospitali watakapotumia mwanya wa nafasi zao kufanya tendo la ndoa na mgonjwa msichana au mwanamke; au kwa waganga wa tiba za jadi atakaye tumia mwanya wa nafasi yake kufanya tendo la ndoa na wagonjwa wake wa kike, mtumishi wa dini ambaye kwa kutambua ushawishi wake juu ya waumini wake afanye nao ngono nao (waumini wanawake).

Kosa la shambulio la aibu litahesabika tu pale ambapo mtu akiwa na nia ya kusababisha aibu ya kingono kwa mtu yeyote.

Neno lolote, sauti yoyote, ishara yoyote au kuonekana kwa picha yoyote ikimaanisha sauti mdhaliliko wa kijinsia, atakuwa na hatia ya kufanya shambulio la aibu na kwa adhabu atahukumiwa kwanda jela kwa kipindi kisichozidi miaka mitano (5) au faini isiyozidi sh 300,000 au vyote, jela na faini kwa pamoja.

Lakini kama shambulio hili la aibu linahusisha msichana aliye chini ya miaka 18, mtuhumiwa hawezi kujitetea kwamba msichana huyo aliridhia shambulio hilo.

Katika mitaa yetu, baadhi ya mambo yanakemewa vikali na sheria na bado yanapata nafasi, ikiwamo watu kutumia lugha za kudhalilisha kimapenzi watu wengine.

Tunapaswa tujue kwamba haya ni makosa ya jinai na ni lazima hatua za kisheria zichukuliwe ili kuyakabili kama si kuyatokomeza kabisa.

Biashara ya ukahaba

Kosa jingine ambalo sheria hii imelielezea ni lile kosa la kufanya ukahaba.

Hili nalo ni kosa la jinai chini ya kifungu cha 12 cha Sheria ya Makosa ya Kujamiiana, ambacho ni marekebisho ya kifungu cha 139 cha Kanuni za Adhabu.

Kuna sababu au visingizio mbalimbali ambavyo watu wengi hasa mijini wanavitaja kama ndiyo sababu zinazosababisha jinai hii kutendeka, lakini ukweli ni kwamba biashara ya ukahaba imeshamiri sana.

Pamoja na sababu au visingizio vinavyotolewa na watu mbalimbali juu ya kufanya biashara hii, lakini katika upande wa sheria, hili ni kosa la jinai na adhabu yake imeanishwa katika kifungu cha 139 ni kifungo kisichopungua miaka 10 jela na faini isiyopungua sh 100,000 na isiyozidi sh 300,000 au vyote faini na kifungo kwa pamoja.

Usafirishaji wa binadamu

Pamoja na makosa yaliyotajwa hapo juu, kuna kosa lililoorodheshwa kama kosa la kusafirisha binadamu.

Hili limetambuliwa chini ya kifungu cha 139A kama kilivyorekebishwa na kifungu cha 14 cha sheria hii.

Ndani ya kifungu hiki , mtu yeyote atakaethibitika kwamba anatangaza, anasaidia au anapigia upatu kununua au kuuza au kubadilishana mtu yeyote kwa ajili ya kupata pesa au malipo mengine, iwe ndani au kwa nia ya kusafirisha mtu huyo nje ya Jamhuri ya Muungano, bila idhini ya wazazi au waangalizi wake; au akipata idhini ya mwanamke mjamzito kwa ajili ya pesa na kumuasili mtoto wa mwanamke huyo ambaye hajazaliwa.

Au anawasaidia wanawake hao kupata ujauzito kwa nia ya kuzaa au kama anahusika na usajili wa vizazi, akijua na bado akaruhusu kutoa taarifa zisizo sahihi juu ya uzazi wa wowote au akisajili taarifa zisizo sahihi, pia atakuwa na hatia ya kutenda kosa la kusafirisha watu na adhabu yake ni kifungo si chini ya miaka 20 na kisichozidi miaka 30 na fidia isiyopungua sh 300,000 au vyote, jela na faini kwa pamoja.

Kiasi hiki hata hivyo, kitaamuliwa na mahakama.

Wednesday, January 19, 2011

Tuungane na Maalim, Balozi Seif wauza 'unga' watafute kazi nyengine wafanye

Na Juma Khamis
NAAMINI pamoja na ugumu wa vita dhidi ya dawa za kulevya unaoelezwa, iwapo tutashikamana kwa dhati Zanzibar tutashinda na kuwaokoa vijana wetu na janga la dawa za kulevya ambalo limeanza kuleta madhara makubwa na kuonesha hatma mbaya Zanzibar.

Viongozi wa Zanzibar waliopita hasa awamu ya sita walijaribu sana kupambana na biashara pamoja na matumizi ya dawa za kulevya, lakini kutokana na vikwazo vuigumu vilivyokuwa vimejitokeza, ikiwemo kukosekana mshikamano miongoni mwa wanajamii na rushwa mafanikio yalikuwa hafifu.

Lakini kwa serikali hii ya awamu ya saba kutokana na misingi iliyojengewa ya umoja mshikamano na maelewano naweza kusema kwamba wafanyabiashara wa dawa za kulevya iwapo tutaamua kwa dhati basi wakatafute kazi nyengine za kufanya mapema, kabla ya kufichuliwa na kukashifika mbele ya jamii.

Turufu kubwa ya ushindi katika vita hivi itakuwa ni uzalendo miongoni mwa wananchi baada ya kuona viongozi wa juu ni mfano mzuri kwao katika kudumisha mshikamano ambao ulikosekana kwa kiasi kikubwa huko nyuma, na zaidi baada ya kuja kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

Hivi sasa viongozi wetu wote wajuu namaanisha Rais Dk. Shein, Makamo wa kwanza Maalim Seif na Makamo wa pili wa Rais Balozi Idd imedhihirika kwamba wanafanya kazi kwa pamoja na mashirikiano makubwa hali inayomaanisha mwanzo mwema kuelekea kwenye mafanikio.

Kama ingekuwa mpira wa miguu basi tungesema ushindi upo wazi kwasababu viungo wa timu ni wazuri na wanaona sana, na kilichobakia ni mabeki pamoja na wafungaji kuwa imara kwa vile mchezo tumeshaudhibiti pale kati kati, basi kwanini Idara zilizobakia zizembee.

Umoja kati ya viongozi hao haunashaka kutokana na kauli, lakini na matendo tunayoyaona tokea siku za mwanzo za serikali hii ya awamu ya saba, hali inayomaanisha kumbe tukiamua hakuna cha kutushinda.

Rais Dk. Shein tayari alithibitisha umoja na maelewano ya hali ya juu kati yake na wasaidizi wake hao, pale alipokuwa akihutubia kwenye kilele cha maadhimisho ya mika 47 ya Mapinduzi ya Zanzibar wiki uwanja wa Amaan mbele ya umati mkubwa wa wananchi, viongozi na wawakilishi wa mataifa ya kigeni.

Lakini pia Maalim Seif naye alithibitisha mashirikiano makubwa na ya aina yake kati yake Rais Dk. Shein na Balozi Seif Idd katika hafla nyingi ikiwemo mkutano wa kwanza wa hadhara wa CUF tangu walipojumuika katika serikali ya umoja wa kitaifa huko katika viwanja vya Kibandamaiti.

Tukumbuke kwamba viongozi hao wote watatu wanachukia sana rushwa, uzembe na tamaa mbaya ya kujilimbikizia mali, na wameweka uzalendo wao kwa Zanzibar, hivyo matumaini yetu ni vigumu kwa 'vidudu mtu' kujipenyeza katika ngome hiyo.

Nimewataja Maalim Seif kwasababu afisi yake ndiyo iliyokabidhiwa rungu kupambana na dawa za kulevya, na Balozi Seif Idd ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za serikali, wakifanya kazi chini ya Dk. Shein na kwa ufupi ngoma imepata wachezaji.

Kwa vile tumeshadhibiti nafasi za viungo, tuwatake walinzi waetu wa timu hii ambao tunaweza kusema ni polisi, mahakama na taasisi nyengine za ulinzi, usalama na kusimamia haki nao wawe tayari kwa ushindi.

Katika kuktadha huu safu ya wapachika mabao itakuwa ni wanajamii wenyewe, ambao bila shaka wanaishi pamoja na kuwatumikia wauzaji hao wa dawa za kulevya. Vijana wetu wanaathirika sana na dawa hizi za kulevya na watumiaji wanasambaa kwa kasi, leo usijekushangaa ukisikia hata kule nyumbani kwetu kisiwani Tumbatu kuna 'mateja' wa dawa za kulevya..

Tukumbuke kwamba tamaa kwa baadhi ya watendaji wakiwemo baadhi ya Polisi na watendaji wa vyombo vya kutoa haki kama tulivyovitaja hapo juu ni maeneo ambayo yalilega lega sana na maadui kupenya kwa miaka mingi tangu kuja kwa biashara huria nchini kwetu.

Tukio la miaka kadhaa nyuma ambapo tulielezwa kuwa pipi zilizokuwa na dawa za kulevya baadaye ilibainika ulikuwa ni unga wa sembe ni mfano mmoja wapo wa udhaifu katika vyombo vyetu hivi vyenye umuhimu wa kipekee kutokomeza maovu haya.

Wengi tulijiuliza inaama inawezekana mtu kuweka pipi yenye unga wa sembe tumboni kutoka Pakistani hadi ije itolewe Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, basi unga wa sembe huo wa Pakistani ni mzuri sana.

Katika mkutano mmoja kati ya wazazi wa Shehia kadhaa za Mji Mkongwe na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za Baraza la Habari (MCT), wakati huo zikiwa mtaa wa Shangani mjini Zanzibar, hofu kuu ya wazazi katika kuwafichua wahusika wakuu wa dawa za kulevya ilikuwa hofu ya kupelekwa majina yao kwa maharamia hao wa mihadarati.

Hofu hii hakiuwa kwa wazazi wa vijana walioathirika na matumizi ya dawa hizo pekee, lakini baadhi ya Msheha katika mji wa Unguja katika mkutano mmoja wa kujadili tatizo la dawa za kulevya mmoja wao alisema 'leo ukimtaja muuzaji wa dawa za kulevya, basi kesho atakufuata nyumbani na kukuonya kwa vitisho vikubwa kwamba utakiona cha moto'.

Kauli za Masheha na wazazi wa Mji Mkongwe kwa kifupi zilimaanisha kwamba miongoni mwa askari Polisi walikuwepo au wapo wanaonufaika na biashara hiyo na wanatumiwa na vigogo hao wa dawa za kulevya.

Kama tulivyogusia katika safu hii wiki iliyopita rushwa, muhali uliopita kiwango na kulindana ndiyo sumu kwa ustawi wa Zanzibar, kwa vile serikali hii imeonesha nia na kwa vitendo kuondoa hali hiyo kwanini wanajamii wote wasitoe wasishirikiane kutauta matatizo yaliyopo.

Tukijipanga kama hivyo na jamii yote kuonesha kuchoshwa na janga hili linalotishia mustakabali wa Zanzibar, dawa za kulevya zitapita wapi kuwafikia vijana. Hivi sasa wenzetu Kenya katika mji wa Mombasa wamefanikiwa sana kufanya 'unga' ni bidhaa adimu katika eneo hilo na vijana wengi walioathirika kwa muda mrefu sasa wanatibiwa katika vituo na wamekuwa na matumaini mapya.

Sote tunaathiriwa na hali ya kukithiri dawa za kulevya Zanzibar, kwa njia moja ama nyengine kama si mwanao, kaka, rafiki, au jirani yako aliyejiingiza kwenye janga hilo, basi utakuwa umeibiwa nyumbani, umekwapuliwa barabarani, au kama hayo yote hayajakukuta basi utakuwa unaishi kwa hofu usijevamiwa na vijana hao iwe njiani au barabarani siku moja.

Hili la uharibifu wa mazingira lahitaji hatua za haraka kumalizwa

Na Juma Khamis
UHIFADHI wa mazingira ni moja ya hatua muhimu kutokana na kuwa rasilimali ardhi ndio nguzo kuu katika maendeleo ya nchi mbalimbali kote ulimwenguni.

Ili nchi iendelee, ardhi imepewa kipaumbele kwa kuwa watu waliopo wanahitaji rasilimali hiyo kwa shughuli mbalimbali zikiwemo ujenzi, kukata miti kwa ajili ya kuni, makaa, chokaa, uchimbaji mchanga na nyenginezo nyingi zenye umuhimu kwa mwanadamu.
Eneo kuu la mazingira nalo ni ardhi tunayoishi. Ardhi ni eneo ambalo haliongezeki huwa linapungua siku hadi siku kutokana na kukosekana mpangalio madhubuti wa udhibiti na mipango ya ardhi iliyojengeka kisheria, ukosekanaji wa hayo ni janga kwenye taifa lolote lile na hili ndilo linaloendelea hivi sasa visiwani.
Kutokana na umuhimu huo, kwa Zanzibar kadiri siku zinavyokwenda maisha yamekuwa yakikua kwa kasi na ongezeko la watu ni sababu ya shughuli zote hizo kuongezeka kiasi cha kwamba sasa imeonekana ardhi imekuwa ikitumiwa vibaya na kusababisha uharibifu wa mazingira hadi hali hii kuitwa janga la kimazingira.

Janga la kimazingira limesababishwa na watu kutokuwa makini katika matumizi ya ardhi. Hali imekuwa si ya kuridhisha kiasi cha kwamba maeneo mengi yamekuwa hatarini na mmong’onyoko wa ardhi kutokana na shughuli za uchimbaji mchanga kiholela.

Maeneo yaliyotembelewa hivi karibuni na kushuhudiwa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali ni jambo la kushangaza kuona bado jamii haijaelewa madhara ya uharibifu wa mazingira.
Kuna umuhimu mkubwa wa kutolewa elimu ya uhifadhi wa Mazingira. Biashara ya utalii haiwezi kukua bila ya kuwepo mandhari nzuri ya kuvutia, kwani wageni au watalii wengi, wanaotembelea katika Visiwa vya Zanzibar wanataraji kujionea mazingira halisi ili iwe kama zawadi ya kusimulia wafikapo makwao.
Hebu fikiria, iwapo kila siku tutaendelea kuchafua mazingira ya fukwe na bahari pamoja na kuchimba mchanga ni nini athari yake, kama si mmong’onyoko wa fukwe na hatimae hata hayo majengo ya Makumbusho yanayowavutia watalii, yanaweza kuathiriwa na majanga yatokanayo na bahari tusipokuwa makini katika kuyaenzi mazingira yetu.
Lazima ziwepo jitihada za makusudi za uelimishaji wa umuhimu wa uhifadhi wa Mazingira kwa kuwekewa mikakati ya uzuiaji uchimbaji mchanga kiholela. Kuna uhusiano wa mazingira na shughuli za kiuchumi, hasa biashara ya uuzaji mchanga.
Sheria zinapaswa kuchukuliwa kutokana na hali ya kwamba tayari miongozo ya maeneo maalum ya uchimbaji ipo na kuelekeza kiwango kinachofaa kuacha uchimbaji mchanga katika eneo husika.

Hili la kuendelea kuharibiwa mazingira na kufanyiwa uchunguzi wa kina ni lakutia moyo kwani endapo hatua za ziada hazitachukuliwa, tabia ya uharibifu wa mazingira inaweza kuleta madhara hapo baadae.
Katika jitihada zake za kuyanusuru mazingira, Idara ya Mazingira Zanzibar mwaka jana ilisimamisha uchimbaji wa mchanga wa pwani katika Hoteli ya kitalii ya Uroa Bay Beach Resort iliyopo Uroa Wilaya ya Kati Unguja.
Licha ya juhudi hizo na kutolewa taarifa mbalimbali za kuwataka wananchi wasichimbe mchanga katika ameneo hayo, tatizo limekuwa likiendelea katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa pwani.
Watafiti wa mazingira ulimwenguni, wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira pamoja na kutaka umma uelewe au ujiepushe na uharibifu wa mazingira hasa katika maeneo ya bahari na pwani.
Lengo likiwa ni kuboresha biashara ya utalii na kuwavutia wageni wa nje na ndani kwa kufuata mfumo wa utunzaji wa mazingira (Ecotourism) katika maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi Ukanda wa Zanzibar.
Licha ya uchimbaji mchanga kiholela , upandaji wa miti ni moja ya hatua muhimu katika kuhifadhi mazingira ya pwani jambo ambalo limekuwa likizembewa na kusababisha fukwe kadhaa kupoteza haiba yake.
Juhudi za pamoja ni njia pekee itakayosaidia kuwafichua wanaokwenda kinyume na wanaharakati wamazingira. Aidha wakaazi wa maeneo ambayo uharibifu wa mazingira unafanyika wanapaswa kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa katika vyombo husika ili kunusuru makaazi yao na janga la kimazingira.
Katika hatua nyengine, kikao cha baraza la wawakilishi ambacho kinaendelea, kinapaswa kujadili uimarishwaji wa utunzaji wa mazingira kwa kupitishwa sheria zinazofaa ili kuwabana wale wote wanaokwenda kinyume na taratibu zilizopo sasa.
Mazingira yanayotunzwa hususan katika ukanda wa pwani huwa ni kivutio kikuu kwa wenyeji, wageni na hata viumbe vya bahari ambavyo hutumia kwa kutagia.
Tuyatunze mazingira yetu kwa manufaa ya kuvinusuru visiwa vyetu na janga la kimazingira na kudumisha sekta ya utalii ili kuimarisha uchumi sambamba na kuharakisha maendeleo ya wananchi waliowanyonge.