Wednesday, January 19, 2011

Hili la uharibifu wa mazingira lahitaji hatua za haraka kumalizwa

Na Juma Khamis
UHIFADHI wa mazingira ni moja ya hatua muhimu kutokana na kuwa rasilimali ardhi ndio nguzo kuu katika maendeleo ya nchi mbalimbali kote ulimwenguni.

Ili nchi iendelee, ardhi imepewa kipaumbele kwa kuwa watu waliopo wanahitaji rasilimali hiyo kwa shughuli mbalimbali zikiwemo ujenzi, kukata miti kwa ajili ya kuni, makaa, chokaa, uchimbaji mchanga na nyenginezo nyingi zenye umuhimu kwa mwanadamu.
Eneo kuu la mazingira nalo ni ardhi tunayoishi. Ardhi ni eneo ambalo haliongezeki huwa linapungua siku hadi siku kutokana na kukosekana mpangalio madhubuti wa udhibiti na mipango ya ardhi iliyojengeka kisheria, ukosekanaji wa hayo ni janga kwenye taifa lolote lile na hili ndilo linaloendelea hivi sasa visiwani.
Kutokana na umuhimu huo, kwa Zanzibar kadiri siku zinavyokwenda maisha yamekuwa yakikua kwa kasi na ongezeko la watu ni sababu ya shughuli zote hizo kuongezeka kiasi cha kwamba sasa imeonekana ardhi imekuwa ikitumiwa vibaya na kusababisha uharibifu wa mazingira hadi hali hii kuitwa janga la kimazingira.

Janga la kimazingira limesababishwa na watu kutokuwa makini katika matumizi ya ardhi. Hali imekuwa si ya kuridhisha kiasi cha kwamba maeneo mengi yamekuwa hatarini na mmong’onyoko wa ardhi kutokana na shughuli za uchimbaji mchanga kiholela.

Maeneo yaliyotembelewa hivi karibuni na kushuhudiwa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali ni jambo la kushangaza kuona bado jamii haijaelewa madhara ya uharibifu wa mazingira.
Kuna umuhimu mkubwa wa kutolewa elimu ya uhifadhi wa Mazingira. Biashara ya utalii haiwezi kukua bila ya kuwepo mandhari nzuri ya kuvutia, kwani wageni au watalii wengi, wanaotembelea katika Visiwa vya Zanzibar wanataraji kujionea mazingira halisi ili iwe kama zawadi ya kusimulia wafikapo makwao.
Hebu fikiria, iwapo kila siku tutaendelea kuchafua mazingira ya fukwe na bahari pamoja na kuchimba mchanga ni nini athari yake, kama si mmong’onyoko wa fukwe na hatimae hata hayo majengo ya Makumbusho yanayowavutia watalii, yanaweza kuathiriwa na majanga yatokanayo na bahari tusipokuwa makini katika kuyaenzi mazingira yetu.
Lazima ziwepo jitihada za makusudi za uelimishaji wa umuhimu wa uhifadhi wa Mazingira kwa kuwekewa mikakati ya uzuiaji uchimbaji mchanga kiholela. Kuna uhusiano wa mazingira na shughuli za kiuchumi, hasa biashara ya uuzaji mchanga.
Sheria zinapaswa kuchukuliwa kutokana na hali ya kwamba tayari miongozo ya maeneo maalum ya uchimbaji ipo na kuelekeza kiwango kinachofaa kuacha uchimbaji mchanga katika eneo husika.

Hili la kuendelea kuharibiwa mazingira na kufanyiwa uchunguzi wa kina ni lakutia moyo kwani endapo hatua za ziada hazitachukuliwa, tabia ya uharibifu wa mazingira inaweza kuleta madhara hapo baadae.
Katika jitihada zake za kuyanusuru mazingira, Idara ya Mazingira Zanzibar mwaka jana ilisimamisha uchimbaji wa mchanga wa pwani katika Hoteli ya kitalii ya Uroa Bay Beach Resort iliyopo Uroa Wilaya ya Kati Unguja.
Licha ya juhudi hizo na kutolewa taarifa mbalimbali za kuwataka wananchi wasichimbe mchanga katika ameneo hayo, tatizo limekuwa likiendelea katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa pwani.
Watafiti wa mazingira ulimwenguni, wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira pamoja na kutaka umma uelewe au ujiepushe na uharibifu wa mazingira hasa katika maeneo ya bahari na pwani.
Lengo likiwa ni kuboresha biashara ya utalii na kuwavutia wageni wa nje na ndani kwa kufuata mfumo wa utunzaji wa mazingira (Ecotourism) katika maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi Ukanda wa Zanzibar.
Licha ya uchimbaji mchanga kiholela , upandaji wa miti ni moja ya hatua muhimu katika kuhifadhi mazingira ya pwani jambo ambalo limekuwa likizembewa na kusababisha fukwe kadhaa kupoteza haiba yake.
Juhudi za pamoja ni njia pekee itakayosaidia kuwafichua wanaokwenda kinyume na wanaharakati wamazingira. Aidha wakaazi wa maeneo ambayo uharibifu wa mazingira unafanyika wanapaswa kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa katika vyombo husika ili kunusuru makaazi yao na janga la kimazingira.
Katika hatua nyengine, kikao cha baraza la wawakilishi ambacho kinaendelea, kinapaswa kujadili uimarishwaji wa utunzaji wa mazingira kwa kupitishwa sheria zinazofaa ili kuwabana wale wote wanaokwenda kinyume na taratibu zilizopo sasa.
Mazingira yanayotunzwa hususan katika ukanda wa pwani huwa ni kivutio kikuu kwa wenyeji, wageni na hata viumbe vya bahari ambavyo hutumia kwa kutagia.
Tuyatunze mazingira yetu kwa manufaa ya kuvinusuru visiwa vyetu na janga la kimazingira na kudumisha sekta ya utalii ili kuimarisha uchumi sambamba na kuharakisha maendeleo ya wananchi waliowanyonge.

No comments:

Post a Comment