Thursday, May 20, 2010

MUM: Chem chem ya maadili ya kiislamu

Na Juma Khamis

CHUO Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM) ni taasisi binafsi ya elimu ya juu Tanzania iliyoanzishwa na Mfuko wa Maendeleo ya Waislamu (MDF).

MUM kilianzishwa chini ya mkataba maalum Oktoba 23 mwaka 2004 na kupata usajili kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Dira ya MUM ni kuwa taasisi ya elimu iliyo imara na kituo kinachotoa elimu, ambayo inakidhi mahitaji ya jamii ya Kitanzania na dunia kwa ujumla, kwa kuzingatia misingi,miongozo na maadili ya kiislamu.

MUM pia kinajikita kuchangia juhudi za taifa za kutoa elimu bora inayokidhi mahitaji ya watu na soko bila kukiuka misingi ya dini.

Taasisi hii ni taasisi muhimu ya elimu hasa kwa jamii ya kiislamu, ambayo kwa muda mrefu sio kwamba ilinyimwa elimu lakini haikuwa na taasisi ya moja kwa moja ambayo ingetoa elimu kwa jamii hiyo.

Hivyo kwa kwa MUM inaonekana ni faraja kubwa kwa jamii ya Kiislamu Tanzania, Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla, kwani ndio taasisi ambayo inawakutanisha vijana wengi wa kiislamu wenye madhebu tofauti, lakini lengo ni kujifunza kwa maslahi ya jamii inayowazunguka.

Kwa kuwa MUMU ni taasisi binafsi, wanafunzi wanaodahiliwa katika chuo hichi wanatrajiwa kuwa wawe na uwezo wa kujigharamia mafunzo yao, iwe kutoka kwenye mifuko, serikali au taasisi zisizokuwa na kiserikali (NGOs) au mashirika.

Serikali kupitia Bodi ya Mfuko wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB) imekuwa ikiwapatia mikopo wanafunzi wanaosoma chuoni hapo kwa lengo la kuwafanya wanafunzi wasome kwa utulivu.

Kwa kawaida HESLB huwalipia wanafunzi wa vyuo vikuu asilimia 100 iwapo mwanafunzi atakuwa amekidhi masharti, lakini mkopo huo hupungua kwa kadiri mwanafunzi anaposhindwa kukidhi masharti yaliyowekwa na Bodi.

Hata hivyo, upungufu huo hubakia kwenye ada ya masomo tu (tuition fee) lakini pesa za kujimu (accommodation) hulipwa sawa kwa wanafunzi wote, wale waliofadhiliwa kwa asilimia 100 na chini ya hapo.

Kwa MUM inapotokea mwanafunzi kufadhiliwa chini ya asilimia 100, gharama iliyosalia humlazimu mwanafunzi kuilipa mwenyewe kwa utaratibu uliopangwa na chuo.

Ada ya masomo kwa MUM inatofautiana sana na vyuo vikuu vyengine na hili limefanywa kwa kuzingatia hali halisi za Watanzania.

Kwa mfano mwanafunzi wa Kitanzania amekuwa akilipa shilingi 1,200,000 kwa mwaka na raia wa kigeni amekuwa akilipa dola za Marekani 2,100 kwa mwaka.

Gharama nyegine ni za matumizi ya kawaida ya mwanafunzi ambayo ni shilingi 1,835,000 ambazo mara nyingi hutolewa na Bodi ya Mfuko wa Elimu ya Juu.

MUM kimekua kikichua wanafunzi kutoka na uwezo wa chuo; kwa mfano katika mwaka masomo 2005, MUM kilikuwa na wanafunzi 167 kati yao 159 walihitimu shahada ya kwanza katika fani za sanaa, Uhusiano wa umma na masomo ya kiislamu Novemba 2008.

Kutoka mwaka wa masomo 2009/2010 MUM, kilipanga kuongeza idadi ya kozi kutoka tatu hadi saba.

Kozi hizo mpya ni Shahada ya Lugha , Shahada ya Biashara, Shahada ya Sayansi ya Elimu na Shahada ya Sheria na Shariah.

Udahili umekuwa ukifanywa kwa kuzingatia ushindani wa hali ya juu.

Kwa waombaji waliomaliza kidato cha nne na kukaa kusoma shule ya msingi kwa miaka saba, miaka minne sekondari na miaka miwili sekondari ya juu (kidato cha tano na sita), masharti ya chini ya kujiunga na MUM ni kuwa na ama kufaulu kwa alama mbili ambazo zitakuwa na uwezo wa kubeba pointi zisizopungua 4.5 au Diploma inayotambuliwa na inayolingana na maombi ya mwanafunzi.

MUM pia inaweza kumsajili mwanafunzi aliemaliza cheti kwa daraja lisilopungua la pili kwa masharti ya kuidhinishwa na Baraza la Senate la chuo.

Kwa wanafunzi ambao mfumo wao wa elimu unafikia miaka minane kwa shule ya msingi na miaka minne na sekondari ni lazima asome mwaka mmoja katika chuo cha nyumbani anakotoka.

MUM kina vifaa vya kisasa vya kujifunzia; ikiwa ni pamoja na vyumba vya kusomea vya kisasa, ambapo kila chuma kina uwezo wa kubaba wanafunzi 75, maktaba pamoja na fursa kadhaa za kujifunza.

Pia MUM kina kompyuta cha kutosha ambazo zimeunganishwa na mtandano wa internet, studio za redio na tv kwa wanafunzi wa shahada ya mawasiliano ya umma.

Chuo pia kina kampasi yake ambayo ina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 600.

Ingawa MUM bado hakijajiunga na mfumo wa sasa wa kudahili wanafunzi kupitia kompyuta uliobuniwa na TUC, bado wanafunzi watakuwa na fursa za kufaidika na mikopo inayotolewa na HESLB.

Uamuzi wa kutojiunga TCU hautaathiri mustakabli wa MUM na wanafunzi kamwe hawapaswi kuhofia hilo, kwani MUM ni mwanachama wa TCU.

Uamuzi wa kujiunga au kutojiunga na TCU bado unabakia kuwa wa chuo, muhimu tu udahili ufanywe kwa kuzingatia masharti na mahitaji ya TCU.

Chuo Kikuu Morogo chawatoa hofu wanafunzi kuhusu mikopo

Na Juma Khamis

CHUO Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM), kimesema uamuzi wake wa kutojiunga na mfumo wa mpya wa kusajili wanafunzi kupitia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), hauathiri nafasi za wanafunzi kupewa mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania, (HESLB).

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Makamu Mkuu wa chuo hicho (Taaluma), kwa vyombo vya habari na Zanzibar Leo kupata nakala yake, imesema Bodi ya mikopo itaendelea na utaratibu wake wa kawaida wa kuwapatia mikopo wanafunzi wote wanaostahiki ambao watajiunga na MUM.

Kwa hivyo, wanafunzi wanaohitaji msaada wa fedha kutoka HESLB wanatakiwa kuomba kupitia bodi hiyo sambamba na kuomba udahili ambao utatolewa moja kwa moja na chuo badala ya TCU.

Kwa mujibu wa utaratibu mpya wa TCU, udahili kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu kuanzia mwaka wa masomo 2010/2011 utatolewa na tume hiyo na , badala ya mfumo uliozoeleka wa kuomba moja kwa moja kupitia vyuo husika.

Hata hivyo, TCU ilisema Chuo kikuu cha kiislamu Morogoro, Chuo Kikuu Zanzibar (ZU) kilichopo Tunguu na Chuo Kikuu cha Elimu Kishiriki Chukwani havijajiunga na mfumo huo na hivyo wanafunzi wanatakiwa kutuma maombi yao moja kwa moja vyuo husika.

Lakini wanafunzi walipata hofu wakiamini kuwa uamuzi wa vyuo hivyo kutojiunga na TCU ungewafanya kukosa mkopo unaotolewa na bodi ya mikopo na baadhi yao kuamua kutojiunga navyo.

Chuo hicho kimesema mfumo wa TCU ni wa hiari na hauna athari kwa vyuo vinavyokataa kuutumia.

Chuo cha Kiislamu Morogoro kimeanzishwa kuwasaidia wanafunzi ambao wamekosa fursa ya kujiunga na vyuo vyengine.

Tuesday, May 4, 2010

Tutaendelea kumkumbuka marehemu mzee Abeid Karume kwa mema aliyotufanyia

LEO ni Aprili saba,siku hii kwa Wazanzibari na Watanzania kwa Jumla inabakia kuwa nakumbukumbu muhimu.

Siku hii ya leo sote tunamkumbuka marehemu Mzee Abeid Aman Karume aliyeuawa kikatili na wapinga maendeleo.

Kifo chake kiliacha majo nzi na masikitiko makubwa sito tu kwa ndugu na wanafamilia lakini taifa letu la Tanzania , Afrika Mashariki na Afrika yote kwa jumla

Hali hiyo ilitokana na ukweli kwamba Marehemu Mzee Karume alikuwa ni dira sahihi katika kuleta kwanza ukombozi wa kweli wa Zanzibar lakini pia na maendeleo kwa jumla.

Sote tunafahamu kwamba mchango kwetu ulikuwa ni chachu muhimu ya kupata uhuru na hatimaye kuweza kujitawala baada ya kumuondoa Mkoloni na himaya zake.

Kwa ujumla wapinga maendeleo waliochukua kwa kuidhulumu kwa makusudi roho ya kiongozi wetu huyo mpendwa imetuweka kwenye majonzi makubwa tokea siku ya kifo chake na hadi leo tunaendelea kukumbuka.

Tunasema kutokana na umuhimu wake sote wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla tutaendelea kukumbuka na kuuthamini kwa hali na mali mchango wake kwenye taifa leu.

Tunaahidi kutimiza na kuendeleza yale yote mazuri aliyoyanza na kuyadhamiria ya kuleta maendeleo ya kweli kwetu sisi wananchi,.

Mzee Karume kwa makusudi kabisa alipinga ubaguzi wa aina zote na kujitahidi kuwaunganisha wazanzibari wote na watanzania kwa jumla jambo ambalo leo hii tunajivunia kuwa na muungano madhubuti na wa aina yeka duniani.

Tunawaambia wale maahani hawakufanikiwa kuzima fikra sahihi za kimaendeleo za mzee wetu huyo licha ya kumkatili roho yake pasi na sababu yoyote.

Tutaendelea kuhudhunika kwa kuwa ni kipinze chetu na roho yake ilidhulumiwa lakini tutaungana kuendeleza masuala yote ya maendeleo ikiwemo huduma bora kwa jamii kama vile za makaazi bora , elimu , maji umeme , Afya na nyengine zote.

Kwa jumla sisi tunaamini kwamba kumuenzi mzee wetu huyu kwetu sisi sio jambo la bahati mbaya ila ni la dhamira ya kweli kwa kuwa alithubutu kujitolea hata kupoteza roho yake kwa sababu yetu sisi wazanzibar.

Hatuna cha kumlipa mzee wetu huyo zaidi ya kumuombea Mwenyezimungu amlaze mahali pema peponi nasi tukiamini kwamba siku moja tutakwenda huko ingawa yeye alidhulumiwa na mahani.

Tunaahidi kuwendelea kujitolea nafsi zetu katika kuhakikisha kwamba maendeleo ya wananchi wetu yanaimarika hatua kwa hatu ikiwa ni kutimiza malengo ya mapinduzi aliyoyaasisi kiongozi wetu huyo mpendwa.

Tunaami kwamba kufanya hivyo ndio kuitikia wito na dhamira ya kweli ya kumuenzi kwa vitendo kipenzi chetu huyo ambaye sote tunaendelea kuona kwamba kama ingekuwepo tungeza kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo kuliko ilivyo sasa.

Monday, May 3, 2010

Tusherehekee uhuru wa habari kwa kuwasaidia wananchi badala ya kuwa ngazi

Na Juma Khamis

WAANDISHI wa habari duniani kote, jana waliadhimisha siku ya uhuru wa habari, ambao huadhimishwa kila ifikapo Mei 3 ya kila mwaka.

Waandishi wa habari hutumia fursa hii kujikumbusha na kutathmini changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa kazi zao ngumu.

Lakini pia hupata fursa ya kujifunza njia mpya za kupata habari pamoja na kuandika habari zaidi za uchunguzi ambazo haziegemei upande wowote, tena zikiwa na vianzio vingi (multiple sources) na kuachana na habari za fulani kasema, ambazo kimsingi hazipo kwa kuwasaidia wananchi.

Siku hii inaadhimishwa wakati Shirika la Kutetea Haki za Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RWB) lenye makao yake makuu mjini Paris , Ufaransa likiwataja wakandamizaji wakuu 40 wa uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Licha ya kwamba Shirika hilo hutoa orodha mpya kila mwaka , lakini kila mara hupatikana wale wanaoendelea kuziendea kinyume haki za uhuru wa vyombo vya habari.

Katika ripoti ya mwaka huu, Shirika hilo limewahusisha wanasiasa, viongozi wa kidini na viongozi wa makundi ya wapiganaji, makundi ambayo yalikuwa nadra kuyakuta katika ripoti zilizopita.

Kimsingi kila mtu ana haki ya kutoa mawazo yake, haki hii inajumuisha kuwa huru, uhuru wa kusema pamoja na kupata habari na fikra kutoka katika vyanzo vyovyote bila ya kuwekewa mipaka.

Kwa mujibu wa shirika hilo, makundi hayo yaliyotajwa kuwa yanakiuka uhuru wa kupashana habari, yana nguvu, ni hatari , hutumia nguvu na hayaguswi na sheria.

Watu hawa wanaokandamiza uhuru wa vyombo vya habari wana nguvu za kukagua habari, kuwaweka kizuizini waandishi habari, kuwateka nyara, kuwatesa na katika hali mbaya kabisa hata kuwaua.

Kwa bahati mbaya sana katika ripoti ya mwaka huu, Marais saba na viongozi kadha wa serikali wako katika orodha hiyo , ikiwa ni pamoja na rais wa China Hu Jintao, rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad, rais Paul Kagame wa Rwanda, Raul Castro wa Cuba na Waziri Mkuu wa Russia, Vladimir Putin, Waziri ambae alitarajiwa kuwa mtetezi mkubwa wa waandishi wa habari .

Wengine wapya katika orodha hiyo ambayo hupitiwa upya kila mwaka ya wakandamizaji wa haki za uhuru wa habari ni pamoja na mkuu wa kundi la Taliban, Mullar Mohammed Omar.

Kiongozi huyo wa Taliban , ambaye ushawishi wake umesambaa hadi Pakistan pamoja na nchi nzima ya Afghanistan , anajiunga na orodha hiyo kwa sababu kile kinachoitwa vita vitakatifu ambavyo anaviongoza ambavyo pia hulenga vyombo vya habari.

Viongozi hao huwatisha waandishi habari kwa sababu tu hawataki kuandika kuhusu mawazo yao binafsi, au ushindi hata pale wanaposhindwa.

Bila shaka vitisho kwa waandishi habari vinaimarisha hali ya raia kujenga hofu na kuelemea upande mmoja hata kama hawauungi mkono.

Kwa Tanzania, uhuru wa habari kinadharia unaonekana kukua kidogo, hasa baada ya serikali kuruhusu watu binafsi kuwekeza katika sekta ya habari.

Vyombo mbali mbali binafsi vimeanzishwa huku wananchi wakipata fursa pana zaidi ya kuvitumia.

Hata hivyo, tatizo bado liko katika upatikanaji wa habari nyeti ambazo zinaigusa moja kwa moja jamii, na ambazo ndio zinazotakiwa na jamii hiyo.

Kwa mfano, bado waandishi wa habari wamekuwa wakikabiliwa na matatizo wanapofuatilia habari zenye uhusiano na masuala ya rushwa au ukandamizaji wa haki za binaadamu.

Watoa habari nao ni changamoto nyegine katika kufanikisha uhuru wa habari. Wao wamekuwa woga kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari kwa kuhofia kupoteza nafasi zao au heshima katika jamii.

Zipo taarifa nyingi zinazowahusisha waandishi wa habari kukabiliwa na vitisho vya kuuawa kwa kisingizio cha kuingilia maslahi ya watu fulani pale wanaporipoti habari za upande mmoja baada ya kuchoshwa na urasimu walio nao viongozi ambao walipaswa kulizungumzia suala hilo kwa upande wa pili.

Changamoto nyegine, ni ile iyowakuta waandishi wa habari wenyewe kwa wenyewe, au taasisi moja ya habari na nyengine, na zaidi hili limejitokeza hapa Zanzibar.

Taasisi zinazosimamia masuala ya habari, zimekuwa zikikumbwa na migogoro ya ndani, ambayo yamesababisha baadhi yao kufa au kuzimia kabisa na kushindwa kufikia lile lengo la kuanzishwa kwake.

Hali hii inasababisha waandishi wa habari Zanzibar kushindwa kuwa na chombo cha kutetea maslahi yao.

Hata hivyo, katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, waandishi wa habari wanaweza kuonekana watu kwa kuwa wako watu waliojiandaa kuwatumia kama ngazi kufikia malengo yao.

Hapa waandishi wa habari watatumiwa kuripoti hata msaada wa shilingi 10,000 kwa sababu tu mtu fulani anataka jimbo fulani.

Hivyo basi, tunapoadhimisha uhuru wa habari tukumbuke wajibu wetu wa kuisadia jamii badala ya wachahe wanaotaka kututumia kama ngazi.