Thursday, May 20, 2010

Chuo Kikuu Morogo chawatoa hofu wanafunzi kuhusu mikopo

Na Juma Khamis

CHUO Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM), kimesema uamuzi wake wa kutojiunga na mfumo wa mpya wa kusajili wanafunzi kupitia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), hauathiri nafasi za wanafunzi kupewa mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania, (HESLB).

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Makamu Mkuu wa chuo hicho (Taaluma), kwa vyombo vya habari na Zanzibar Leo kupata nakala yake, imesema Bodi ya mikopo itaendelea na utaratibu wake wa kawaida wa kuwapatia mikopo wanafunzi wote wanaostahiki ambao watajiunga na MUM.

Kwa hivyo, wanafunzi wanaohitaji msaada wa fedha kutoka HESLB wanatakiwa kuomba kupitia bodi hiyo sambamba na kuomba udahili ambao utatolewa moja kwa moja na chuo badala ya TCU.

Kwa mujibu wa utaratibu mpya wa TCU, udahili kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu kuanzia mwaka wa masomo 2010/2011 utatolewa na tume hiyo na , badala ya mfumo uliozoeleka wa kuomba moja kwa moja kupitia vyuo husika.

Hata hivyo, TCU ilisema Chuo kikuu cha kiislamu Morogoro, Chuo Kikuu Zanzibar (ZU) kilichopo Tunguu na Chuo Kikuu cha Elimu Kishiriki Chukwani havijajiunga na mfumo huo na hivyo wanafunzi wanatakiwa kutuma maombi yao moja kwa moja vyuo husika.

Lakini wanafunzi walipata hofu wakiamini kuwa uamuzi wa vyuo hivyo kutojiunga na TCU ungewafanya kukosa mkopo unaotolewa na bodi ya mikopo na baadhi yao kuamua kutojiunga navyo.

Chuo hicho kimesema mfumo wa TCU ni wa hiari na hauna athari kwa vyuo vinavyokataa kuutumia.

Chuo cha Kiislamu Morogoro kimeanzishwa kuwasaidia wanafunzi ambao wamekosa fursa ya kujiunga na vyuo vyengine.

No comments:

Post a Comment