Thursday, May 20, 2010

MUM: Chem chem ya maadili ya kiislamu

Na Juma Khamis

CHUO Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM) ni taasisi binafsi ya elimu ya juu Tanzania iliyoanzishwa na Mfuko wa Maendeleo ya Waislamu (MDF).

MUM kilianzishwa chini ya mkataba maalum Oktoba 23 mwaka 2004 na kupata usajili kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Dira ya MUM ni kuwa taasisi ya elimu iliyo imara na kituo kinachotoa elimu, ambayo inakidhi mahitaji ya jamii ya Kitanzania na dunia kwa ujumla, kwa kuzingatia misingi,miongozo na maadili ya kiislamu.

MUM pia kinajikita kuchangia juhudi za taifa za kutoa elimu bora inayokidhi mahitaji ya watu na soko bila kukiuka misingi ya dini.

Taasisi hii ni taasisi muhimu ya elimu hasa kwa jamii ya kiislamu, ambayo kwa muda mrefu sio kwamba ilinyimwa elimu lakini haikuwa na taasisi ya moja kwa moja ambayo ingetoa elimu kwa jamii hiyo.

Hivyo kwa kwa MUM inaonekana ni faraja kubwa kwa jamii ya Kiislamu Tanzania, Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla, kwani ndio taasisi ambayo inawakutanisha vijana wengi wa kiislamu wenye madhebu tofauti, lakini lengo ni kujifunza kwa maslahi ya jamii inayowazunguka.

Kwa kuwa MUMU ni taasisi binafsi, wanafunzi wanaodahiliwa katika chuo hichi wanatrajiwa kuwa wawe na uwezo wa kujigharamia mafunzo yao, iwe kutoka kwenye mifuko, serikali au taasisi zisizokuwa na kiserikali (NGOs) au mashirika.

Serikali kupitia Bodi ya Mfuko wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB) imekuwa ikiwapatia mikopo wanafunzi wanaosoma chuoni hapo kwa lengo la kuwafanya wanafunzi wasome kwa utulivu.

Kwa kawaida HESLB huwalipia wanafunzi wa vyuo vikuu asilimia 100 iwapo mwanafunzi atakuwa amekidhi masharti, lakini mkopo huo hupungua kwa kadiri mwanafunzi anaposhindwa kukidhi masharti yaliyowekwa na Bodi.

Hata hivyo, upungufu huo hubakia kwenye ada ya masomo tu (tuition fee) lakini pesa za kujimu (accommodation) hulipwa sawa kwa wanafunzi wote, wale waliofadhiliwa kwa asilimia 100 na chini ya hapo.

Kwa MUM inapotokea mwanafunzi kufadhiliwa chini ya asilimia 100, gharama iliyosalia humlazimu mwanafunzi kuilipa mwenyewe kwa utaratibu uliopangwa na chuo.

Ada ya masomo kwa MUM inatofautiana sana na vyuo vikuu vyengine na hili limefanywa kwa kuzingatia hali halisi za Watanzania.

Kwa mfano mwanafunzi wa Kitanzania amekuwa akilipa shilingi 1,200,000 kwa mwaka na raia wa kigeni amekuwa akilipa dola za Marekani 2,100 kwa mwaka.

Gharama nyegine ni za matumizi ya kawaida ya mwanafunzi ambayo ni shilingi 1,835,000 ambazo mara nyingi hutolewa na Bodi ya Mfuko wa Elimu ya Juu.

MUM kimekua kikichua wanafunzi kutoka na uwezo wa chuo; kwa mfano katika mwaka masomo 2005, MUM kilikuwa na wanafunzi 167 kati yao 159 walihitimu shahada ya kwanza katika fani za sanaa, Uhusiano wa umma na masomo ya kiislamu Novemba 2008.

Kutoka mwaka wa masomo 2009/2010 MUM, kilipanga kuongeza idadi ya kozi kutoka tatu hadi saba.

Kozi hizo mpya ni Shahada ya Lugha , Shahada ya Biashara, Shahada ya Sayansi ya Elimu na Shahada ya Sheria na Shariah.

Udahili umekuwa ukifanywa kwa kuzingatia ushindani wa hali ya juu.

Kwa waombaji waliomaliza kidato cha nne na kukaa kusoma shule ya msingi kwa miaka saba, miaka minne sekondari na miaka miwili sekondari ya juu (kidato cha tano na sita), masharti ya chini ya kujiunga na MUM ni kuwa na ama kufaulu kwa alama mbili ambazo zitakuwa na uwezo wa kubeba pointi zisizopungua 4.5 au Diploma inayotambuliwa na inayolingana na maombi ya mwanafunzi.

MUM pia inaweza kumsajili mwanafunzi aliemaliza cheti kwa daraja lisilopungua la pili kwa masharti ya kuidhinishwa na Baraza la Senate la chuo.

Kwa wanafunzi ambao mfumo wao wa elimu unafikia miaka minane kwa shule ya msingi na miaka minne na sekondari ni lazima asome mwaka mmoja katika chuo cha nyumbani anakotoka.

MUM kina vifaa vya kisasa vya kujifunzia; ikiwa ni pamoja na vyumba vya kusomea vya kisasa, ambapo kila chuma kina uwezo wa kubaba wanafunzi 75, maktaba pamoja na fursa kadhaa za kujifunza.

Pia MUM kina kompyuta cha kutosha ambazo zimeunganishwa na mtandano wa internet, studio za redio na tv kwa wanafunzi wa shahada ya mawasiliano ya umma.

Chuo pia kina kampasi yake ambayo ina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 600.

Ingawa MUM bado hakijajiunga na mfumo wa sasa wa kudahili wanafunzi kupitia kompyuta uliobuniwa na TUC, bado wanafunzi watakuwa na fursa za kufaidika na mikopo inayotolewa na HESLB.

Uamuzi wa kutojiunga TCU hautaathiri mustakabli wa MUM na wanafunzi kamwe hawapaswi kuhofia hilo, kwani MUM ni mwanachama wa TCU.

Uamuzi wa kujiunga au kutojiunga na TCU bado unabakia kuwa wa chuo, muhimu tu udahili ufanywe kwa kuzingatia masharti na mahitaji ya TCU.

No comments:

Post a Comment