Monday, May 3, 2010

Tusherehekee uhuru wa habari kwa kuwasaidia wananchi badala ya kuwa ngazi

Na Juma Khamis

WAANDISHI wa habari duniani kote, jana waliadhimisha siku ya uhuru wa habari, ambao huadhimishwa kila ifikapo Mei 3 ya kila mwaka.

Waandishi wa habari hutumia fursa hii kujikumbusha na kutathmini changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa kazi zao ngumu.

Lakini pia hupata fursa ya kujifunza njia mpya za kupata habari pamoja na kuandika habari zaidi za uchunguzi ambazo haziegemei upande wowote, tena zikiwa na vianzio vingi (multiple sources) na kuachana na habari za fulani kasema, ambazo kimsingi hazipo kwa kuwasaidia wananchi.

Siku hii inaadhimishwa wakati Shirika la Kutetea Haki za Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RWB) lenye makao yake makuu mjini Paris , Ufaransa likiwataja wakandamizaji wakuu 40 wa uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Licha ya kwamba Shirika hilo hutoa orodha mpya kila mwaka , lakini kila mara hupatikana wale wanaoendelea kuziendea kinyume haki za uhuru wa vyombo vya habari.

Katika ripoti ya mwaka huu, Shirika hilo limewahusisha wanasiasa, viongozi wa kidini na viongozi wa makundi ya wapiganaji, makundi ambayo yalikuwa nadra kuyakuta katika ripoti zilizopita.

Kimsingi kila mtu ana haki ya kutoa mawazo yake, haki hii inajumuisha kuwa huru, uhuru wa kusema pamoja na kupata habari na fikra kutoka katika vyanzo vyovyote bila ya kuwekewa mipaka.

Kwa mujibu wa shirika hilo, makundi hayo yaliyotajwa kuwa yanakiuka uhuru wa kupashana habari, yana nguvu, ni hatari , hutumia nguvu na hayaguswi na sheria.

Watu hawa wanaokandamiza uhuru wa vyombo vya habari wana nguvu za kukagua habari, kuwaweka kizuizini waandishi habari, kuwateka nyara, kuwatesa na katika hali mbaya kabisa hata kuwaua.

Kwa bahati mbaya sana katika ripoti ya mwaka huu, Marais saba na viongozi kadha wa serikali wako katika orodha hiyo , ikiwa ni pamoja na rais wa China Hu Jintao, rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad, rais Paul Kagame wa Rwanda, Raul Castro wa Cuba na Waziri Mkuu wa Russia, Vladimir Putin, Waziri ambae alitarajiwa kuwa mtetezi mkubwa wa waandishi wa habari .

Wengine wapya katika orodha hiyo ambayo hupitiwa upya kila mwaka ya wakandamizaji wa haki za uhuru wa habari ni pamoja na mkuu wa kundi la Taliban, Mullar Mohammed Omar.

Kiongozi huyo wa Taliban , ambaye ushawishi wake umesambaa hadi Pakistan pamoja na nchi nzima ya Afghanistan , anajiunga na orodha hiyo kwa sababu kile kinachoitwa vita vitakatifu ambavyo anaviongoza ambavyo pia hulenga vyombo vya habari.

Viongozi hao huwatisha waandishi habari kwa sababu tu hawataki kuandika kuhusu mawazo yao binafsi, au ushindi hata pale wanaposhindwa.

Bila shaka vitisho kwa waandishi habari vinaimarisha hali ya raia kujenga hofu na kuelemea upande mmoja hata kama hawauungi mkono.

Kwa Tanzania, uhuru wa habari kinadharia unaonekana kukua kidogo, hasa baada ya serikali kuruhusu watu binafsi kuwekeza katika sekta ya habari.

Vyombo mbali mbali binafsi vimeanzishwa huku wananchi wakipata fursa pana zaidi ya kuvitumia.

Hata hivyo, tatizo bado liko katika upatikanaji wa habari nyeti ambazo zinaigusa moja kwa moja jamii, na ambazo ndio zinazotakiwa na jamii hiyo.

Kwa mfano, bado waandishi wa habari wamekuwa wakikabiliwa na matatizo wanapofuatilia habari zenye uhusiano na masuala ya rushwa au ukandamizaji wa haki za binaadamu.

Watoa habari nao ni changamoto nyegine katika kufanikisha uhuru wa habari. Wao wamekuwa woga kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari kwa kuhofia kupoteza nafasi zao au heshima katika jamii.

Zipo taarifa nyingi zinazowahusisha waandishi wa habari kukabiliwa na vitisho vya kuuawa kwa kisingizio cha kuingilia maslahi ya watu fulani pale wanaporipoti habari za upande mmoja baada ya kuchoshwa na urasimu walio nao viongozi ambao walipaswa kulizungumzia suala hilo kwa upande wa pili.

Changamoto nyegine, ni ile iyowakuta waandishi wa habari wenyewe kwa wenyewe, au taasisi moja ya habari na nyengine, na zaidi hili limejitokeza hapa Zanzibar.

Taasisi zinazosimamia masuala ya habari, zimekuwa zikikumbwa na migogoro ya ndani, ambayo yamesababisha baadhi yao kufa au kuzimia kabisa na kushindwa kufikia lile lengo la kuanzishwa kwake.

Hali hii inasababisha waandishi wa habari Zanzibar kushindwa kuwa na chombo cha kutetea maslahi yao.

Hata hivyo, katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, waandishi wa habari wanaweza kuonekana watu kwa kuwa wako watu waliojiandaa kuwatumia kama ngazi kufikia malengo yao.

Hapa waandishi wa habari watatumiwa kuripoti hata msaada wa shilingi 10,000 kwa sababu tu mtu fulani anataka jimbo fulani.

Hivyo basi, tunapoadhimisha uhuru wa habari tukumbuke wajibu wetu wa kuisadia jamii badala ya wachahe wanaotaka kututumia kama ngazi.

No comments:

Post a Comment