Saturday, April 24, 2010

Utaratibu wa uendeshaji kesi za jinai

Na Juma Khamis
KATIKA mada hii tunakusudia kuanisha utaratibu wa kisheria kuhusu uendeshaji wa mashauri ya jinai.

Kimsingi ni muhimu kuweka bayana mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanagusa mwenendo mzima wa uendeshaji wa kesi za jinai na haki za wahusika yaani walalamikaji, watuhumiwa wa makosa, washitakiwa na wale waliopatikana na hatia.Wadau katika usimamizi wa haki katika mwenendo wa jinai ni jamii nzima kwa ujumla.

Hata hivyo, jamii inawakilishwa na vyombo vilivyopewa mamlaka kisheria.

Vyombo hivyo ni Mamlaka ya Upelezi yaani Polisi, Mamlaka ya Uendeshaji wa Mashtaka ambayo ni ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Mamlaka ya kusikiliza za kutoa uamuzi wa mashtaka hayo yaani Mahakama.

Hebu kabla hatujasonga mbele zaidi tuangalie makosa ya jinai na mashauri ya madai.

Ili kupata ufahamu wa kutosha na kuweza kuzingatia zaidi mada hii, ni vyema tukatofautisha walau kwa mukhtasari makosa ya jinai na mashauri ya madai.

Jinai kama ilivyotafsiriwa na vitabu mbali mbali vya sheria ni kutenda au kutokutenda jambo kunakomfanya mtu aadhibiwe kisheri.

Kwa ufafanuzi zaidi makosa ya jinai ni yale ambayo jamii inayaona bayana kuwa ni makosa yanayoigusa na mwenye kuyatenda anastahili kupewa adhabu kisheria.

Makosa haya yameanishwa katika sheria ya adhabu na katika vitabu vyengine vinavyohusika na upewaji adhabu kutokana na makosa mengineyo.

Kimsingi katika makosa ya jinai Dola, Jamhuri au serikali ndiyo hulalamika, kwa hivyo uhusiano wakisheria katika jinai ni baina ya mshitakiwa na Mamlaka ya nchi.

Kwa upande mwengine mashauri ya madai yanahusisha watu binafsi kutokana na kudaiana haki zao zinazotokana na mahusiano yatokanayo na makubaliano au kuaminiana kisheria ambapo mtu mmoja hakutekeleza makubaliano hayo au hakulipa anachodaiwa.

Madai kwa mujibu wa sheria hayahusishi adhabu bali mdaiwa hutakiwa kulipa au kutekeleza wajibu kutokana na makubaliano yaliyofikiwa.


Lakini kwa faida ya wasomaji, katika mada hii tutazingatia zaidi makosa ya jinai na jinsi ya kuyaendesha.

Mahakama zote zimepewa uwezo wa kusikiliza kesi za jinai kwa mujibu wa sheria.

Uwezo wa mahakama na mahakimu umeelezwa na sheria ya Mahakimu wa Mahakama za mwanzo, wilaya na za mkoa.

Ukubwa au umaalum wa kesi huzingatiwa katika kuamua ni mahakama ipi kesi ifunguliwe.

Katika kutekeleza hayo sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai imeeleza uwezo wa kutoa adhabu kwa mahakama zote.
Mahakama kuu ina uwezo wa kutoa adhabu yoyote au kutoa amri yoyote zilizoruhusiwa na sheria.

Kifungu cha 7 cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinaeleza uwezo huo.

Kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha sheria hiyo, mahakama ya mkoa imepewa uwezo wa kutoa adhabu ya kifungo kisichozidi miaka saba, faini isiyozidi shilingi milioni nne, kutumikia jamii kwa muda usiozidi miezi 12.

Mahakama ya wilaya nayo imepewa nguvu katika kifungu cha 9 kutoa adhabu ya kifungo kisichozidi miaka mitanom, faini isiyozidi shillingi milioni mbili na kutumikia jamii kwa kipindi kisichozidi miezi sita.

Kifungu cha 10 kinaipa uwezo mahakama ya mwanzo kutoa adhabu ya kifungo kisichozidi miezi mitatu, faini isiyozidi shilingi 100,000 na kutumikia jamii kwa kipindi kisichozidi miezi miwili.

Adhabu hizo za kutumikia jamii zimewekwa kwa mujibu wa kanuni za kutumikia jamii kanuni zilizotungwa na Jaji Mkuu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa jinai, Mahakama ya mkoa imepewa uwezo wa kutoa adhabu kubwa zaidi hata kufikia kifungo cha maisha cha maisha ikwa baadhi ya makosa kwa mfano makosa yaliyotajwa na vifungu vya 125, 132, 150, 151, 160, 161, 286, 287, 324, 342(3),(4) na 343 vya sheria ya adhabu No.6/2004.

Mahakama hizo pia zaweza kuwa na nguvu zaidi iwapo zitapewa nguvu hizo na sheria ya Mahakimu wa Mahkama.

Kuhusu uwezo wa kusikiliza kesi za watoto (Juveniles) mahakama iliyopewa uwezo huo kwa mujibu wa sheria ni mahakama ya mkoa.

Watoto wasiozidi umri wa miaka 16 ndio husikilizwa katika mahakama za watoto.

Ukamataji, Upekuzi na Haki zake
Miongoni mwa hatua za awali kuhusiana na usimamizi wa m wenendo wa Jinai ni ukamataji na upekuzi wa watuhumiwa.

Namna ya ukamataji imeelezwa katika kifungu cha 13 cha sheria ya Mwenendo wa Jinai kwamba Polisi au mtu mwengine anapomkamata mtu analazimika kumgusa mtu huyo anayetakiwa kukamatwa.

Kifungu kidogo cha (2) cha kifungu hicho kinamtaka mkamataji kutumia kila njia muhimu kufanikisha ukamataji huo.

Ukamataji umegawanyika katika makundi mawili.

Ukamataji bila ya kutumia hati ya kukamata umeelezwa katika kifungu cha 21 cha sheria ya Mwenendo wa Jinai ambapo Polisi wanaruhusiwa kukamata watuhumiwa au wahalifu waliotenda au wanaotenda makosa yanayoonekana au kujulikana wazi wazi.

Zaidi ya makosa hayo yaliyotajwa na kifungu cha 21, makosa mengine yote yanayosalia yanahitaji kwanza hati ya kukamata (Arrest warrant), ambayo hutolewa na mahakama pekee.

Katika kufanikisha ulamataji, mambo mengine hutokea kama vile upekuaji wa eneo alilokamatwa mtuhumiwa kwa mujibu wa kifungu cha 14, ruhusa ya kuvunja ili kukamata au kuvunja ili kutoka iwapo mkamataji amefungiwa ndani kama kinavyoeleza kifungu cha 15.

Sheria pia inawapa watu binafsi au raia wa kawaida uwezo wa kukamata, kama ilivyoanishwa katika kifungu cha 26 na 44 kwa mahakimu kulingana na makosa na aina ya makosa hayo na namna yalivyotendeka.

Upekuzi: Hatua hii inahusu upekuzi wa watu na upekuzi wa maeneo.

Mtu aliyekamatwa hupekuliwa na Polisi na mali/vitu vyake au vilivyokamatwa miongoni mwake huhifadhiwa kwa mujibu wa kifungu cha 17.

Lakini kama tulivyoona awali eneo ambalo mtu anayekamatwa amepatikana hupekuliwa pia.

Sheria pia inawapa polisi uwezo wa kusimamia na kupukua gari na vyombo mbali mbali vya usafiri na usafirishaji iwapo kuna hisia au tuhuma za kuwepo mali au mhalifu katika vyombo hivyo kama ilivyoolezwa katika kifungu cha 18.

Lakini kifungu cha 19 kimezingatia stara ya mwanamke kwa kutana upekuzi wake ufanywe na wanawake wenziwe.

Kwa ujumla ukamataji na upekuzi ni matukio yanayokwenda pamoja na kwa mujibu wa sheria zipo haki ya msingi ambazo lazima zitekelezwe katika hatua hizo.

Haki za mtuhumiwa/mshitakiwa
Haki hizi zinaanzia wakati wa kukamatwa. Kifungu cha 30 kinamtaka mkamataji kujitambulisha na amweleze mkamatwaji makosa yake.

Haki nyegine ni ile ya kutowekwa ndani zaidi ya saa 24 bila ya kufikishwa mahakamani kama ilivyoanishwa katika kifungu cha 24.

Kifungu cha 32 kimakataza Polisi kumuweka mtu kizuizini bila ya sababu za msingi.

Mtu aliyekamatwa huhojiwa kuhusiana na tuhuma dhidi yake, hata hivyo kifungu cha 33 kinaelezea kwamba muda huo wa kuhojiwa usizidi saa nne au ikibidi kuongezwa muda huo kwa mujibu wa kifungu cha 34 basi usizidi saa nane au maombi ya kuzidishwa muda yapelekwe kwa Hakimu.

Tuesday, April 13, 2010

Wanaoomba Vyuo Vikuu sasa kutuma maombi TCU

Na Juma Khamis
UTARATIBU wa kujiunga na Vyuo Vikuu vya elimu ya juu nchini umebadilika na utaanza kutumika mwaka huu wa masomo 2010/2011.

Kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), waombaji watatakiwa kuomba udahili moja kwa moja kupitia TCU kwa kutumia mtandao wa intaneti na simu za mkononi.

Utaratibu huo mpya unafuta ule wa zamani ambapo wanafunzi walikuwa wakituma maombi moja kwa moja vyuo vikuu.

Hata hivyo, utaratibu huo hautatumika kwa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) kilichopo Tunguu, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Zanzibar Chukwani na Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro kwa kuwa havijajiunga na mfumo huo.

Wanafunzi wanaoomba katika Vyuo hivyo, watalazimika kutumia mfumo wa zamani wa kutuma maombi yao moja kwa moja chuoni.

Utaratibu huo mpya unawahusu wale watakaoomba udahili kwa kutumia sifa za kidatu cha sita , walizozipata kuanzia mwaka 1988 hadi mwaka 2010 na wale wenye vyeti vya nchi nyegine.

TCU imesema maombi kwa wanafunzi waliomaliza kidatu cha sita mwaka 1988 hadi mwaka uliopita na wale wenye vyeti vya nje yameanza tokea Aprili 8 mwaka huu.

Aidha Tume hiyo imesema kwa wale waliomaliza kidatu cha sita mwaka huu wataanza kuomba udahili Aprili 30 au wakati wowote majibu yao ta mitihani itakapotangazwa.

Saturday, April 10, 2010

Ijumaa kuu:Siku Yesu aliyosulubiwa msalabani

Na Juma Khamis (kwa msaada wa maandiko)
Leo ni Siku ya Ijumaa Kuu, ambapo wakristo duniani kote wanaungana wenzao, kukumbuka mateso aliyoyapata Yesu Kristo, wakati aliposulubiwa msalabani huko Jerusalem, yapata miaka 2, 000 iliyopita

Kumbukumbu hii, inaadhimishwa kwa ibada ya Ijumaa Kuu iliyojaa historia ya mateso ya Yesu Kristu.

Tendo la Yesu kufa msalabani linaonesha jinsi Yesu Kristu alivyokubali kubeba makosa ya wakiristu ikiwa ni fidia ya maisha kwa Mungu.

Hata hivyo, kufa msalabani hakuna maana kuwa Yesu alikuwa na dhambi.

Maandiko ya kikiristu (biblia) yanabainisha kuwa Yesu alikubali kuzibeba dhambi za wafuasi wake katika mwili wake juu ya msalaba, ili wapate kufa wakiwa hawana dhambi na kuishi kwa ajili ya uadilifu.

Kwa kadiri ya mafundisho ya Kanisa Katoliki, dhambi ni matendo yoyote ya makusudi ambayo mtu anayotenda kwa kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu, yaani kuvunja amri 10 za Mungu.

Ili dhambi iitwe dhambi ni lazima itendwe kwa makusudi, yaani na mtu mwenye akili timamu.

Ijumaa kuu inaadhimishwa wakati dunia leo ikiwa imegubikwa na matendo mengi ya dhambi, huku matendo mazuri ya kumtukuza Mungu yakipungua na matendo mabaya ya kishetani yakitawala nafsi za watu na kusababisha watu waishi katika ulimwengu wa kutupiana mpira.

Serikali kwa upande inalaumu madhehebu ya dini, vivyo hivyo madhehebu ya dini yanailaumu serikali kwamba imekuwa laini mno kuruhusu na kuachia kila kitu, hata yale yanayokiuka maadili ya jamii

Kwa upande mwingine wazazi wanalaumu kuwa watoto wa siku hizi hawana heshima, watoto nao wanalaumu wazazi kuwa wao wamelegea katika suala la malezi, yaani wazazi wamekuwa huria mno katika suala la malezi na hawaishi na kutenda kulingana na umri wao.

Mfano mdogo tu, baba wa miaka 60 leo anafikishwa mahakamani kwa kulawiti mtoto wa miaka 12.

Pia kuna kutupiana mpira kati ya masikini na matajiri, kwamba maskini wanalalamika kuwa matajiri ndio chanzo cha uozo wote katika jamii, watu maarufu kujihusisha dawa ya kulevya na athari zake zinawakumba watoto wa maskini.

Pia mvutano mwingine ni kati ya nchi maskini na tajiri, Afrika inazilaumu nchi za Magharibi kuwa zinaua maadili ya Kiafrika kwa kusambaza utamaduni wake mchafu.

Lakini cha kujiuliza, hakuna sera zinazopaswa kuwekwa na nchi kama hizo kuzuia uingiaji wa tamaduni hizo?.

Kwa mfano, angalia suala la ndoa za mashoga, kuna nchi za Kiafrika zimeruhusu kufungisha ndoa za mashoga.

Ndio tendo la ushoga lilikuwepo lakini halikuwa limewekewa sheria ya kuliruhusu mpaka kwenye nyumba za ibada lifanyiwe ibada na kurasimishwa rasmi kuwa huyu mwanamume ni mke wangu na mimi mwanamume mwenziwe ni mume wake.

Sikuu ya Ijumaa kuu inafuatiwa na Pasaka ambayo historia yake imeanza mbali.

Siku hii ndio aliyofufukua Yesu Kiristu baada ya kusulubiwa msalabani.

Kabla ya kuja kwa dini ya Kikiristu, watu walikuwa na dini mbali mbali lakini baada ya kuanza, watu walianza kupuuza utamaduni wa kuabudu miungu na taratibu za watu wa mataifa mbali mbali, walianza kusherehekea sikukuu ya Pasaka, kama ishara ya kukubali utamaduni mpya.

Utamaduni mpya ulihimiza watu waache kuabudu miungu na kumfuata Yesu Kristo kama mfalme na mwokozi wa watu wote duniani.

Jina la Pasaka limetokana na neno la Kiebrania lenye maana ya pasaka.

Jina hilo lina maana ya kupita juu, kukaa juu au mlinzi kama ilivyoandikwa katika Biblia.

Sherehe za Pasaka ya Kikristo ni chimbuko la sherehe ya Pasaka ya Kiyahudi.

Kwa Kiswahili majina ya sherehe za Kikristo na Kiyahudi, hazitofautiani kwa kuwa tukio la kusulubiwa na kufufuka kwa Yesu Kristo lilitokea wakati wa sikukuu ya Pasaka ya Kiyahudi mwaka wa 30 kabla ya Kristo.

Kwa mujibu wa historia ya dini ya Kikristo, wakristo wa kwanza walikuwa Wayahudi.

Awali Wayahudi hao walikuwa wakisherehekea sikukuu ya Kiyahudi pamoja na kumbukumbu ya kufufuka kwa Yesu Kristo.

Hata hivyo, Wayahudi waliojikita kwenye dini ya Kikristo, waliamua kutenganisha sherehe hizo na kufuata kalenda tofauti, kwa lengo la kuimarisha dini ya Kikristo.

Pasaka ya Kiyahudi ni miongoni mwa sikukuu muhimu na yenye mtazamo wa kipekee kwa Wayahudi, kwani inatumika kukumbuka jinsi Wanaisraeli walivyofanikiwa kuwa huru, baada ya

Pasaka ya Kikristo inashabihiana sana na Pasaka ya Kiyahudi kutokana na historia ya Pasaka hizo mbili.

Kwa mujibu wa maandiko Musa alitumwa na Mungu kuwaondoa Wanaisraeli katika hali ya utumwa katika nchi ya Misri kisha kuwaongoza kwenda nchi ya ahadi.

Hata hivyo, mfalme wa Misri mwenye cheo cha Farao alikaidi amri ya Mungu na kuendelea kuwashikilia Wanaisraeli.

Kama ilivyo kwa Wayahudi, Pasaka ya wakristo inahesabiwa kuwa sikukuu muhimu kabisa katika ukiristo.

Tarehe ya Pasaka inafuata mwandamo wa mwezi, hivyo sikukuu hiyo haina tarehe maalumu katika kalenda ya kawaida.

Lengo la siku hii ni kuhimiza umoja aliokuwa nao Yesu Kristu kwani maandiko yanasema kabla Yesu Kristo hajasulubiwa msalabani alifanya karamu na kula pamoja na wanafunzi wake ili kuhimiza umoja na ushirikiano baina yao.

Kanali Kima atangaza kugombea Ubunge Chwaka

KANALI mstaafu wa JWTZ, Said Ali Khamis, maarufu Said Kima, ametangaza azma yake ya kugombea nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Chwaka, kupitia chama tawala cha CCM.

Akizungumza katika mahojiano maalum nyumbani kwake Chukwani, Kima ambae aligombea nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2005, alisema lengo lake ni kushirikiana na watu wa Chwaka kuliletea maendeleo Jimbo hilo.

Kanali huyo alishindwa na Mbunge wa sasa wa Jimbo hilo, Yahya Kassim.

Kima ambae aliwahi kuwa rubani wa ndege ya Rais wa serikali ya awamu ya pili ya Zanzibar, alisema anataka yale mazuri aliyoyapata kuyafanyia kazi kwa maslahi ya watu wa Chwaka na wilaya nzima ya Kati.

“Sina uwezo wa kuleta maendeleo peke yangu, lakini kwa sababu nimejifunza mengi mazuri, nitashirikiana na watu wa Chwaka kuhakikisha tunapata maendeleo,” alisema.

Mgombea huyo ambae ni mwanachama hai wa CCM alielipia kadi yake hadi mwaka 2013, alisema kama atashinda, Chwaka itakuwa Jimbo la mfano kwa maendeleo katika wilaya ya Kati.

Akizungumzia suala la elimu, Kima alisema inasikitisha kuona wilaya nzima ya kati haina skuli ya sekondari ya juu na hivyo, atahakikisha anatumia ushawishi alionao pamoja na wabunge wengine wa wilaya hiyo, kuipatia wilaya ya Kati skuli ya aina hiyo.

“Chwaka tumebahatika kuwa na Chuo Kikuu, lakini wanafunzi wengi wanaoingia pale ni kutoka nje ya Chwaka na wilaya ya kati, inasikitisha sana kuona tumeshindwa hata kuanzisha skuli ya elimu ya juu katika wilaya yetu,” alisema.

“Lazima tukubali kuwa wilaya ya Kati tuko nyuma sana kielimu na sasa muda umefika wa kusema basi na inatosha kuwa watu wa mwisho,” alisema.

Kanali Kima ambae aliwahi kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Zanzibar, alisema lengo lake jengine ni kuhakikisha barabara ya Ukongoroni inajengwa kwa kiwango cha lami katika kipindi kifupi.

“Suala la Ukongoroni linanisikitisha, kama Mungu atanijaalia nikashinda, basi barabara hii itajengwa katika kipindi kifupi sana,” aliongeza.

Kujitangaza kwa Kima kunachukuliwa kama changamoto kubwa kwa Mbunge wa sasa, ambae kuna dalili ya kuomba kurejea tena katika Jimbo hilo kwa awamu ya nne (miaka 20), ingawa bado hajathibitisha.

Ni jukumu la mwari kumtaja mtu aliempa ujauzito

Na Juma Khamis
SHERIA ya kuwalinda wari na watoto wa mzazi mmoja, ni moja ya sheria nyingi zilizotungwa na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Sheria hii ilitungwa kutokana na kukithiri kwa matukio ya udhalilishaji wa wari na watoto wadogo, lengo likiwa ni kukomesha unyanyasi huo.

Hata hivyo, licha kuwepo sheria hii, lazima tukiri kwamba bado vitendo vya kuwadhalilisha wari vimekuwa vikiendelea, huku wari wangi wakipewa ujauzito na kuishia kuolewa.

Sheria hii inaelezea kwa kina makosa mbali mbali ya jinai ambayo hayakuelezwa na sheria ya makosa ya Jinai (Penal Act No.6 ya mwaka 2004).

Kabla ya kuzungumzia baadhi ya makosa ya jinai katika sheria hii, kwanza tuone maana ya ‘mwari’ kama mmoja ya mlengwa wa sheria hii.

Kwa mujibu wa kifungu cha pili cha sheria hii, mwari ni mwanamke asiepata kuolewa ambaye yuko baina ya umri wa miaka 18 na miaka 21 na asiyepata kuzaa mtoto.

Baadhi ya makosa yanayotambuliwa na sheria hii ni pamoja mwari atakaepatikana na ujauzito ambao ameupata kwa hiari yake.

Adhabu katika kosa hili iwapo atatiwa hatiani ni kutumikia jamii kwa kipindi cha kuanzia miezi mitatu tokea siku aliyojifungua.

Sheria hii pia imebainisha kuwa mtu yeyote atakaehusika na ujauzito wa mwari huyo atakuwa amefanya kosa na pindi atakapotiwa hatiani adhabu yake ni kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu na si zaidi ya miaka mitano .

Pamoja na adhabu hiyo atatakiwa atoe matunzo kwa mtoto atakaezaliwa na mwari huyo.

Sheria pia imesema kuwa ni jukumu la mwari yeyote atakaekuwa mjamzito kutaja jina la mtu aliempa ujauzito huo na pindi mwari huyo atakataa kutaja jila mtu huyo atakuwa ametenda kosa la jinai na endapo atatiwa hatiani adhabu yake ni kutumikia jamii kwa kipindi cha miezi mitatu.

Hata hivyo, itakuwa ni kingi kwa mwari huyo kama atathibitisha kuwa ujauzito huo ameupata kutokana na kubakwa na watu wengi au mazingira mengine ambayo hakuweza kumtambua mbakaji.

Iwapo mwari huyo kwa makusudi amemtaja mtu tofauti na aliyemsababishia ujauzito huo, na kama mahakama itaridhika amefanya hivyo kwa makusudi, atakuwa ametenda kosa la jinai na akipatikana na hatia atatumikia jamii kwa kipindi cha miezi sita.

Friday, April 9, 2010

Magonjwa sugu ya macho sasa yatibiwa Z’bar

Na Juma Khamis
MAGONJWA sugu ya macho Zanzibar kama presha ya macho (glaucoma) na mtoto wa jicho sasa yanatibiwa nchini kwa kutumia teknolojia ya kisasa, inayotumiwa katika nchi kadhaa zilizoendelea ikiwemo Marekani na Ulaya.

Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili, daktari bingwa wa upasuaji wa macho kutoka China anaefanya kazi hospitali kuu ya Mnazimmoja, Dkt. Ji Jiangdong, alisema Zanzibar ni moja kati ya nchi zinazotumia huduma bora na ya kisasa zaidi katika kutibu maradhi ya macho.

Alisema wagonjwa wa macho sasa wana fursa sawa na zile wanazopata wagonjwa wenzao kutoka Marekani na mataifa ya Ulaya na katika baadhi ya miji nchini China.

“Hakuna upasuaji tunaofanya, badala yake tunatumia mashine maalum ambayo inanyonya mtoto wa jicho kwa kasi kubwa,” alisema Dkt Jiangdong.

Alisema mashine inayotumiwa ni aina ya Phacoemulsification ambayo ni ya kisasa na inapatikana katika hospitali kubwa duniani hasa nchi zilizoendelea na matibabu hufanywa kwa msaada wa Ultra Sound.

Aidha alisema mgonjwa anaefanyiwa matibabu sasa hapaswi kudungwa tena sindano, badala yake hutumia dawa maalum ya usingizi.

Alisema Zanzibar inapaswa kujivunia uhusiano wake na China kwani vifaa vilivyoletwa na serikali ya China havipo katika baadhi hospitali kubwa za mijini nchini humo.

“Hii ni huduma ghali sana duniani lakini kwa sababu Zanzibar na China ni marafiki wa karibu sana, tumeleta huduma hii ili watu wa Zanzibar nao wafaidike,” alisema.

Aidha alisema operesheni za macho kwa watoto wadogo, ambazo kabla zilikuwa zikifanyika katika hospitali ya CBRT kwa gharama za serikali ya Zanzibar sasa zinafanywa katika hospitali ya Mnazi mmoja.

Dkt. Jiangdong alisema asilimia 6.7 ya watu weusi wako kwenye hatari ya kuugua presha ya macho ikilinganishwa na watu weupe ambao ni asilimia 1-2.

Alisema mara nyingi huwapata watu walio na umri wa miaka 30-40 na 35-50.

Mapema Daktari dhamana wa kitengo cha macho katika hospitali hiyo, Dkt. Slim Mohammed, alisema gharama za matibabu kama hayo ambazo katika hospitali za Tanzania Bara zinafanywa kwa zaidi ya shilingi 400,000, kwa Zanzibar mgonjwa hutakiwa kuchangia shilingi 15,000 tu.

Aidha alisema kile kilio cha wananchi kudai kuwa viongozi wamekuwa wakifuata matibabu nje ya nchi sasa kimekwisha kwa kuwa viongozi wa juu wamekuwa wakipatiwa matibabu katika kliniki hiyo.

“Hakuna sababu kwa viongozi kufuata huduma ya macho nje ya nchi kwa sababu kile wanachokifata sasa kinapatikana Zanzibar,” alisema.

Gazeti hili lilimshuhudia Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Mawasiliano na Uchukuzi, Machano Othman Said akipatiwa huduma ya macho katika kliniki hiyo.

Akizungumzia suala la wataalamu wazalendo watakaotoa huduma hiyo baada ya jopo la madaktari wa China kuondoka, Dkt. Mohammed alisema serikali tayari inasomesha wataalamu wake nchini China.

“Wataalamu wanzalendo tayari wako China na hivi karibuni tunatarajiwa watarejea kuanza kutoa huduma ya macho,” alisema.

Hata hivyo, alisema serikali ina mkataba na China kwa karibu miaka 10 wa kuwapatia madaktari bingwa wa fani tofauti.

Alisema matibabu ya presha ya macho mara nyingi hufanywa kwa kutumia dawa, upasuaji na hatua zinachukuliwa kutibu maradhi hayo kwa kutumia leser ambayo kwa sasa inatumiwa Afrika Kusini pekee.

Dkt. Mohammed alisema presha ya macho ni ugonjwa wa pili baada ya mtoto wa jicho unao
sababisha upofu Zanzibar.

Hivyo, aliwataka wananchi kuwahi hospitali haraka mara wanapoona dalili za kuumwa na kichwa au kutoona vizuri.

Tayari zaidi ya wagonjwa 600 wameshapatiwa matibabu ya macho tokea kuja kwa madaktari bingwa kutoka China, Unguja na Pemba na lengo ni kuwahudumia wagonjwa 1,400 kwa mwaka.

China ndio mfadhili mkuu wa kiliniki ya macho Zanzibar, ambapo imechangia vifaa vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya dola 800,000 pamoja na jopo la madaktari bingwa.

Uvimbe wa Ini sasa watibiwa bila kupasuliwa Mnazi Mmoja

Na Juma Khamis

KWA mara ya kwanza katika historia ya Zanzibar, madaktari bingwa wa upasuaji kutoka China, wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji wagonjwa watano waliokuwa wakisumbuliwa na uvimbe wa usaha katika ini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, daktari bingwa wa upasuaji Dk. Yong Shi, alisema wagonjwa hao walikuwa wakikabiliwa na ugonjwa unaosababishwa na mkusanyiko wa usaha katika ini (liver abscess).

Alisema upasuaji huo ambao ni wa kwanza kufanyika Zanzibar, umechukua dakika mbili tu kwa kila mgonjwa na unafanywa kwa utaalamu wa hali ya juu.

Upasuaji huo unaofanywa kwa muongozo wa Ultra Sound, ni wa kisasa na maarufu katika nchi nyingi duniani, lakini kwa Zanzibar ni mara ya kwanza kufanyika.

Mgonjwa hutobolewa sehemu ndogo ya tumbo na kupenyezwa kifaa maalum (tube) ambacho kwa wakati mmoja kina uwezo wa kutibu na kuingiza dawa kwenye sehemu iliyoathirika.

Dk. Yong alisema kabla ya teknolojia hiyo mpya kwa Zanzibar, mgonjwa kama huyo angelazimika kupasuliwa sehemu kubwa ya tumbo na kuondolewa sehemu iliyoathirika, kitendo ambacho ni hatari kwa maisha ya mgonjwa.

Alisema teknolojia hiyo, haina maumivu yoyote kwa mgonjwa na anaweza kupata nafuu katika kipindi kifupi tokea afanyiwe upasuaji.

“Upasuaji huu hauna maumivu kwa mgonjwa, mgonjwa anaweza kupona haraka, kuliko upasuaji uliokuwa ukifanywa kabla,” alisema Dk. Yong.

Alisema dalili za ugonjwa huo ni maumivu makali ya tumbo, homa na mgonjwa huwa hawezi kupinda.

“Kwa Zanzibar mgonjwa kama huyu angelazimika kufanyiwa upasuaji mkubwa na kukatwa sehemu kubwa sana ambayo inachukua muda mrefu kupona. Bila shaka upasuaji huu umefanikiwa kwa kiasi kikubwa, na tunajivunia,” alisema.

Akizungumzia ugonjwa wa vijiwe katika damu (blood stones), Dk. Shi alisema Wazanzibari wengi wanasumbuliwa na ugonjwa huo.

Aidha alisema, wengi wanaokwenda hospitali kwa kesi za kusumbiliwa uvimbe, vibofu vya mkojo au vijiwe kwenye damu ni wanaume na wanawake huenda hospitali wakiwa tayari wameshaathiriwa na maradhi hayo.

Mapema, mgonjwa Ali Juma ambae amefanyiwa upasuaji wa usaha katika ini aliliambia gazeti hili, kuwa maisha yake sasa yameokoka baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Juma ambae amehamishiwa hospitali ya Mnazi Mmoja akitokea hospitali ya Abdalla Mzee, Pemba, alisema kabla ya upasuaji alikuwa akipata maumivu makali ya tumbo na homa za mara kwa mara na kushindwa kufanya kazi zake vizuri kwa kuwa alishindwa kuinama na kupinda.

Akionekana mkakamavu, siku chache tu baada ya upasuaji huo, Juma alisema hali yake ya afya imerejea ya kawaida na hakuna maumivu yoyote aliyopata na anayopata baada ya upasuaji huo.

Dk. Shi alifanya upasuaji huo akisaidiwa na daktari wazalendo, akiwemo Dk. Suleiman Aboud Jumbe.

China yaipatia Zanzibar msaada

SERIKALI ya China imeipatia msaada wa vifaa mbali mbali vya kisasa vyenye thamani ya shilingi milioni 64 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vya uimarishaji wa huduma za afya katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja.

Vifaa hivyo vitatumika katika hospitali ya Mnazimmoja kwa ajili ya huduma za upasuaji pamoja na sehemu ya macho.

Akipokea msaada huo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Sultan Mohammed Mughery amesema kuwa China imefanikisha kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza sekta ya afya kwa Unguja na Pemba.

Amesema msaada huo walioutoa utawezesha katika kufanya kazi hizo kwa urahisi na ufanisi mkubwa wa kuwahudumia wananchi wa Zanzibar.

Aidha Waziri Mughery amesifu jitihada za Serikali za China katika kuwapatia wataalamu mbali mbali ikiwemo wa maradhi ya wanawake kwa Hospitali kuu ya Mnazimmoja, macho pamoja na sehemu nyemgine.

Ameahidi kuwa vifaa hivyo vitatumika kwa uwangalifu ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kusaidia utoaji wa huduma kuwa zenye ubora wa hali ya juu.

Nae kiongozi wa madaktari kutoka nchini China Dk Zhu Xiangjuan amesema nchi yake itaendeleza kila aina misaada kwa Zanzibar katika kustawisha maisha ya wazanzibari kwa huduma za afya.

Amesema wataendeleza kuwapatia madaktari vifaa pamoja na mafunzo kwa wafanyakazi wa Zanzibar ili waweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi wa hali ya juu.

China na Zanzibar imekuwa marafiki kwa kipindi cha miaka 46 sasa na wanaendelea kuisaidia Zanzibar katika nyanja tofauti ikiwemo madaktari pamoja na mambo mbali mbali na sasa wapo madaktari wapatao 21 ambao wanatoa huduma za kiafya kwa Unguja na Pemba.

Migomo katika maeneo ya kazi ni haki ya mwajiriwa

Na Juma Khamis
KATIKA safu hii leo alau kwa muhtasari tutaangalia asili ya uhusiano kati ya mwajiri na mwajiriwa mahapa pa kazi.

Kimsingi mwajiri tunaweza kumuelezea kama mtu (kampuni) mwenye kumiliki mtaji ambao unahitaji kutumika ili uwe na tija kwake, sio kama mwajiriwa.
Mwajiriwa ni yule mtu anaemiliki nguvu kazi ambao uhai na kustawi wake kunahitaji mtaji ili iweze kuwa na manufaa kwa muhusika.
Hapa ukiangalia utaona picha ya kutegemeana kati ya pande hizi mbili katika mikataba ya ajira (contract of service/ contract for service), yaani mtaji hautakuwa na manufaa yoyote kwa mwajiri endapo ataukalia nyumbani tu bila ya kuuwekeza.

Hivyo hivyo, mwajiriwa hatapata tija inayotokana na na nguvu kazi yake kama nguvu hizo ataamua kukaa nazo tu bila ya kuziwekeza kwe mwenye mtaji.

Kwa mantiki hiyo, kila upande unategemea upande mwengine.
Kutokana na hilo, ndipo tunapopata uhimuhimu wa mahusiano (relation) baina ya mwajiri na mwajiriwa katika mazingira ya kazi.
Lakini kama ilivyo kawaida, penye mkusanyiko mkubwa wa watu, migogoro na hali ya kutoelewana hasa kimaslahi sehemu ya kazi ni sehemu ya maisha na utamaduni uliozoeleka ingawa haupendwi sana na upande wa mwajiri.
Hii ni kwa sababu mwajiri siku zote anachotaka kuona kutoka kwenye mtaji wake ni faida tu na sio kitu chenginecho.
Ni kawaida katika maisha yetu kusikia migomo katika maeneo mbali mbali ya kazi na hata katika taasisi za elimu kama vyuo vikuu, ingawa kwa upande wetu Zanzibar matukio hayo ni machache kutokea, na pale inapotokea basi huwa kimya kimya na haileti athari kubwa.
Migomo mahala pa kazi ni kitendo cha wafanyakazi katika taasisi fulani kusitisha huduma zao.
Migomo hii imegawanyika katika sehemu mbali mbali kulingana na mbinu inayotumika kufanikisha mgomo husika.

Kwa mfano’ Go slow’ huu ni aina ya mgomo ambao kwa kawaida mwajiriwa hasitishi kutoa huduma zake, lakini anapunguza uzalishaji kiasi tu cha kumuathiri mwajiri.
Aina nyengine ya mgomo inaitwa ‘Pen down’ , katika aina hii ya mgono, mwajiriwa anafika kama kawaida yake katika sehemu yake ya kazi, lakini anasitisha kutoa huduma.
Aina hii inatofautiana na aina nyegine ya mgomo ambayo kwa jina la kisheria unaitwa ‘sit down’, katika aina hii mfanyakazi anafika sehemu yake ya kazi lakini anakataa kufanya kazi lakini pia anakataa kuondoka.
Mara nyingi, aina hii ya mgomo, hutumiwa vyombo vya usalama kuwaondoa wafanyakazi wanaokata kuondoka katika eneo la kazi.
‘Tool down’ hii ni aina ya mgomo, ambapo mfanyakazi anabakia katika sehemu yake ya kazi, lakini anasita kutoa huduma kwa kipindi kifupi, pengine dakika 10, saa moja na kadhalika.
Mgomo kama huu ulishawahi kufanywa na taasisi mbali mbali za fedha na athari yakae ikaonekana katka matawi ya taasisi hizo hapa Zanzibar.
Migomo mengine inayotambuliwa ni ‘lock out’ na ‘lock in’ ambapo mwajiriwa ama humfungia mwajiri wake nje ya ofisi (yaani humzuia kuingia ofisini) au humfungia mwajiri wake ndani ya ofisi (yaani kumzuia kutoka nje ya ofisi).
Kwa mwajiriwa mgomo ni ishara ya kuushinikiza uongozi (mwajiri) kutekeleza matakwa ya mfanyakazi.
Neno mgomo kama linavyosomeka, limebeba dhana nzima ya shari zaidi.

Kwa tafsiri ya mitaani, mgomo hutafsiriwa kama kitendo cha mwajiriwa kuasi na kukaribisha ghasia katika eneo la kazi, dhana ambayo haina mashiko ya kisheria.
Lakini katika hali ya mahusiano memea kazini, mgomo ni moja kati ya njia zinazokubalika kisheria kutumika kwa mfanyakazi kudai haki yake anayohisi kuwa imeporwa na ainaelekea kuporiwa na mwajiri.
Mgomo ni moja ya silaha inayokubalika kutumika kukabiliana na mwajiri ambae hataki kuthamini na kusikiliza kilio cha mtumishi wake.
Uhalali na uharamu wa mgomo utategemea malengo na jinsi utakavyotekelezwa.
Hapa naaminisha kuwa kuna maeneo mgomo haukubaliki.
Migomo kisheria huchukuliwa kama moja ya njia muhimu zinazowakutanisha ana kwa ana mwajiri na mwajiriwa na kutatua matatizo yao bila kuushirikisha upande wa tatu ambao unakua na udhaifu mkubwa katika kufikia maamuzi ya pamoja (collective agreement) kama ilivyoelezwa katika sheria ya mahusiano kazini No. 11 ya mwaka 2005.

Waandishi wa habari wanawajibika mbele ya sheria kwa makosa yanayotendwa na kalamu zao

SHERIA ya makosa ya jinai namba 6 ya mwaka 2004, imeeleza kwa kina baadhi ya makosa ambayo yanaweza kutendwa na waandishi wa habari.

Sheria hii imefafanua jinsi mwandishi wa habari anavyoweza kupatikana na hatia na makosa ambayo atayatenda na kuchukuliwa kama jinai dhidi ya Jamhuri.

Sheria hii imetambua kuwa mwandishi wa habari atakuwa amefanya kosa iwapo kwa kudhamiria au bila kudhamiria atachapisha habari za uongo ambazo zinaweza kusababisha fujo, hofu na kuchafua amani katika jamii.

Neno kuchapisha hapa halikutafsiriwa tu kwa vyombo vya habari vya kuchapisha (printing media) lakini hata kwa vyombo vyengine vya vya habari ambavyo kwa jina la kihabari vitambuliwa kama electronic media, mfano redio au televisheni.

Katika dunia ya sasa, vyombo vya habari vimekuwa vikutumika kwa njia moja au nyengine kuchapisha ama habari za uongo au habari zinazoegemea upande (single side story).

Kwa mfano katika mauaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka 1994, mahakama ya inayosikiliza kesi za mauaji hayo ICTR imewapata na hatia waandishi wa habari kadhaa kwa kutangaza habari za uongo au za uchochezi dhidi ya jamii moja.

Sheria hii ya mwaka 2006, pia imeeleza kuwa iwapo mwandishi wa habari atakutwa na hatia ya kuandika habari ya uongo na pindi atakapotiwa hatiani, adhabu yake haitazidi kifungo cha miaka miwili.

Hata hivyo, itakuwa ni kinga kwa kosa hili iwapo mshitakiwa atathibitisha kuwa kabla ya kuchapisha habari hiyo atakuwa amechukua hatua kuthibitisha usahihi wa habari hizo na kumpelekea kaumini kuwa habari hiyo ni ya kweli.

Kosa jengine ambalo sheria hii imelizingatia kwa mwandishi wa habari ni kuchapisha kitu chochote kwa lengo la kusomwa na kupelekea kushusha hadhi, kusababisha chuki au kashfa kwa mtoto wa Mfalme wa kigeni, Balozi, au kiongozi wa nje.

Au kwa lengo la kuchafua amani na urafiki kati ya Zanzibar na nchi ambayo mtu huyo anatoka.


Kosa jengine ni kuchapisha au kueneza jina au kitu chochote kitakachofichua jina la muathirika wa makosa ya kujamiiana (mfano mtu aliebakwa).

Adhabu kwa kosa hili ni kifungo kisichozidi miaka miwili au faini isiyozidi shilingi 300,000.

Isipokwa kama kuna amri ya maandishi ya afisa husika wa kituo cha polisi au afisa mpelelezi wa kosa hilo kwa nia njema (good faith) na kwa lengo la upelelezi, au kwa ruhusa ya maandishi ya muathirika (victim) au kama muathirika amefariki au ni mtoto mdogo au mwendawazimu kwa ruhusa ya jamaa wa karibu wa muathirika huyo na kwa ruhusa ya afisa husika wa kituo cha polisi.

Au kwa ruhusa ya mahakama katika kuchapisha jina la muathirika kinyume chake mtu atakaefanya hivyo bila ya ruhusa atakuwa amefanya kosa la jinai.

Ushahidi ni tegemeo muhimu kwa maamuzi ya mahakama

Na Juma Khamis
KIMSINGI mahakama ambayo ni moja ya mihimili mikuu mitatu ya dola, ndicho chombo chenye mamlaka ya kusikiliza au kuamua mashauri na kesi mbali mbali zinazoibuka miongoni mwa jamii.
Katika kusimamia na kutimiza wajibu wake kisheria hutegemea uwasilishaji wa ushahidi wa pande zote mbili katika kesi, yaani ushahidi wa upande wa mashtaka (Prosecution side) ambao kwa kawaida ndio unaoanzisha kesi na upande wa utetezi (Defensive side).
Ni kwa kuzingatia ushahidi huo ndio mahakama huwa na uwezo wa kupima na kuchambua kwa kina ushahidi uliowasilishwa kabla ya kuamua ni upande upi katika kesi una haki au upande upi umeshindwa kutokana na udhaifu wa ushahidi wake.
Kwa mujibu wa sheria ya ushahidi, ushahidi wa kusikia au kwa lugha ya kisheria ‘hear say evidence’ ni moja kati ya aina mbali mbali za ushahidi unaoweza kutumika katika kuthibitisha ukweli wa shauri lililofunguliwa mahakamani.
Hata hivyo, kimsingi aina hii ya ushahidi ni miongoni mwa ushahidi usiokubalika kutumika katika kuthibitisha kesi yoyote mahakamani, isipokuwa katika mazingira fulani.

Ushihidi wa kusikia, unatokana na maelezo ya kusikia kutoka kwa mtu mwengine ambaye ndiye aliyeshuhudia tukio lililoshuhudiwa.
Wanataaluma mbali mbali wa sheria (Jurists) wametafsiri kwamba ushahidi wa kusikia (Hear say Evidence) ni aina ya ushahidi ambao maelezo yake yametolewa na shahidi ambaye kimsingi hawezi kuutolea ushahidi mahakamani.
Yaani ushahidi ambao hutolewa na mtu ambae yeye binafsi hajashuhudia tukio, isipokuwa kwa kusikia tu kutoka kwa wengine.
Sababu ya kukataliwa kwa aina hii ya ushahidi katika kuthibitisha madai mahakamani ni kwamba haiwezekani katika hali ya kawaida kumuhoji shahidi juu ya kama hilo linalozungumzwa na mwengine ni la kweli au la.
Hii inawezekana pale tu inapotokea mtoaji halisi wa taarifa anapokuwa mahakamani kama shahidi, yaani shahidi aliyeshuhudia ukweli husika.
Sababu yengine inatokana na tabia ya kibinadamu. Hakuna mtu anaebisha kwamba ushahidi unaotolewa kwa kukariri au kurudia kilichosemwa na mwengine huwa na tabia ya kupotosha ukweli kwa kuwa kuna taarifa zitapunguzwa uhalisia wake na nyengine zitatiwa chumvi.
Sababu nyengine muhimu ni kutokana na wakati shahidi anapojaribu kurudia kauli ambayo aliitoa awali inakua na nguvu zaidi ikilinganishwa na kauli au taarifa za kusikia kutoka kwa mtu wa pili.
Kwa kawaida ushahidi hutengenezwa aidha kwa kuzungumza kwa mdomo au maelezo ya uthibitisho wa jambo, pia inaweza kwa kutumia mtindo wa kuwasilisha nyaraka (documents) zinazothibitisha ukweli mbele ya mahakama.
Pia inaweza kuhusisha aina yoyote ya mawasiliano ilimradi tu ni katika kuthibitisha.
Njia hizi zote zinaweza kuwa ni moja kwa moja au kupitia mtu mwengine.
Endapo ushahidi huo utatolewa kwa nia ya kutaka kuthibitisha uhalali kwa kauli iliyotumika, basi ushahidi huo utakuwa ni wa kusikia na hivyo hautakubalika mahakamani.
Ushahidi unaokubalika na mahakama ni ule wa kuthibitisha kauli inayothibitisha ukweli wa shauri au kesi hiyo.

Magonjwa sugu ya macho sasa yatibiwa Z’bar

Na Juma Khamis
MAGONJWA sugu ya macho Zanzibar kama presha ya macho (glaucoma) na mtoto wa jicho sasa yanatibiwa nchini kwa kutumia teknolojia ya kisasa, inayotumiwa katika nchi kadhaa zilizoendelea ikiwemo Marekani na Ulaya.

Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili, daktari bingwa wa upasuaji wa macho kutoka China anaefanya kazi hospitali kuu ya Mnazimmoja, Dkt. Ji Jiangdong, alisema Zanzibar ni moja kati ya nchi zinazotumia huduma bora na ya kisasa zaidi katika kutibu maradhi ya macho.

Alisema wagonjwa wa macho sasa wana fursa sawa na zile wanazopata wagonjwa wenzao kutoka Marekani na mataifa ya Ulaya na katika baadhi ya miji nchini China.

“Hakuna upasuaji tunaofanya, badala yake tunatumia mashine maalum ambayo inanyonya mtoto wa jicho kwa kasi kubwa,” alisema Dkt Jiangdong.

Alisema mashine inayotumiwa ni aina ya Phacoemulsification ambayo ni ya kisasa na inapatikana katika hospitali kubwa duniani hasa nchi zilizoendelea na matibabu hufanywa kwa msaada wa Ultra Sound.

Aidha alisema mgonjwa anaefanyiwa matibabu sasa hapaswi kudungwa tena sindano, badala yake hutumia dawa maalum ya usingizi.

Alisema Zanzibar inapaswa kujivunia uhusiano wake na China kwani vifaa vilivyoletwa na serikali ya China havipo katika baadhi hospitali kubwa za mijini nchini humo.

“Hii ni huduma ghali sana duniani lakini kwa sababu Zanzibar na China ni marafiki wa karibu sana, tumeleta huduma hii ili watu wa Zanzibar nao wafaidike,” alisema.

Aidha alisema operesheni za macho kwa watoto wadogo, ambazo kabla zilikuwa zikifanyika katika hospitali ya CBRT kwa gharama za serikali ya Zanzibar sasa zinafanywa katika hospitali ya Mnazi mmoja.

Dkt. Jiangdong alisema asilimia 6.7 ya watu weusi wako kwenye hatari ya kuugua presha ya macho ikilinganishwa na watu weupe ambao ni asilimia 1-2.

Alisema mara nyingi huwapata watu walio na umri wa miaka 30-40 na 35-50.

Mapema Daktari dhamana wa kitengo cha macho katika hospitali hiyo, Dkt. Slim Mohammed, alisema gharama za matibabu kama hayo ambazo katika hospitali za Tanzania Bara zinafanywa kwa zaidi ya shilingi 400,000, kwa Zanzibar mgonjwa hutakiwa kuchangia shilingi 15,000 tu.

Aidha alisema kile kilio cha wananchi kudai kuwa viongozi wamekuwa wakifuata matibabu nje ya nchi sasa kimekwisha kwa kuwa viongozi wa juu wamekuwa wakipatiwa matibabu katika kliniki hiyo.

“Hakuna sababu kwa viongozi kufuata huduma ya macho nje ya nchi kwa sababu kile wanachokifata sasa kinapatikana Zanzibar,” alisema.

Gazeti hili lilimshuhudia Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Mawasiliano na Uchukuzi, Machano Othman Said akipatiwa huduma ya macho katika kliniki hiyo.

Akizungumzia suala la wataalamu wazalendo watakaotoa huduma hiyo baada ya jopo la madaktari wa China kuondoka, Dkt. Mohammed alisema serikali tayari inasomesha wataalamu wake nchini China.

“Wataalamu wanzalendo tayari wako China na hivi karibuni tunatarajiwa watarejea kuanza kutoa huduma ya macho,” alisema.

Hata hivyo, alisema serikali ina mkataba na China kwa karibu miaka 10 wa kuwapatia madaktari bingwa wa fani tofauti.

Alisema matibabu ya presha ya macho mara nyingi hufanywa kwa kutumia dawa, upasuaji na hatua zinachukuliwa kutibu maradhi hayo kwa kutumia leser ambayo kwa sasa inatumiwa Afrika Kusini pekee.

Dkt. Mohammed alisema presha ya macho ni ugonjwa wa pili baada ya mtoto wa jicho unao
sababisha upofu Zanzibar.

Hivyo, aliwataka wananchi kuwahi hospitali haraka mara wanapoona dalili za kuumwa na kichwa au kutoona vizuri.

Tayari zaidi ya wagonjwa 600 wameshapatiwa matibabu ya macho tokea kuja kwa madaktari bingwa kutoka China, Unguja na Pemba na lengo ni kuwahudumia wagonjwa 1,400 kwa mwaka.

China ndio mfadhili mkuu wa kiliniki ya macho Zanzibar, ambapo imechangia vifaa vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya dola 800,000 pamoja na jopo la madaktari bingwa.