Friday, April 9, 2010

Waandishi wa habari wanawajibika mbele ya sheria kwa makosa yanayotendwa na kalamu zao

SHERIA ya makosa ya jinai namba 6 ya mwaka 2004, imeeleza kwa kina baadhi ya makosa ambayo yanaweza kutendwa na waandishi wa habari.

Sheria hii imefafanua jinsi mwandishi wa habari anavyoweza kupatikana na hatia na makosa ambayo atayatenda na kuchukuliwa kama jinai dhidi ya Jamhuri.

Sheria hii imetambua kuwa mwandishi wa habari atakuwa amefanya kosa iwapo kwa kudhamiria au bila kudhamiria atachapisha habari za uongo ambazo zinaweza kusababisha fujo, hofu na kuchafua amani katika jamii.

Neno kuchapisha hapa halikutafsiriwa tu kwa vyombo vya habari vya kuchapisha (printing media) lakini hata kwa vyombo vyengine vya vya habari ambavyo kwa jina la kihabari vitambuliwa kama electronic media, mfano redio au televisheni.

Katika dunia ya sasa, vyombo vya habari vimekuwa vikutumika kwa njia moja au nyengine kuchapisha ama habari za uongo au habari zinazoegemea upande (single side story).

Kwa mfano katika mauaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka 1994, mahakama ya inayosikiliza kesi za mauaji hayo ICTR imewapata na hatia waandishi wa habari kadhaa kwa kutangaza habari za uongo au za uchochezi dhidi ya jamii moja.

Sheria hii ya mwaka 2006, pia imeeleza kuwa iwapo mwandishi wa habari atakutwa na hatia ya kuandika habari ya uongo na pindi atakapotiwa hatiani, adhabu yake haitazidi kifungo cha miaka miwili.

Hata hivyo, itakuwa ni kinga kwa kosa hili iwapo mshitakiwa atathibitisha kuwa kabla ya kuchapisha habari hiyo atakuwa amechukua hatua kuthibitisha usahihi wa habari hizo na kumpelekea kaumini kuwa habari hiyo ni ya kweli.

Kosa jengine ambalo sheria hii imelizingatia kwa mwandishi wa habari ni kuchapisha kitu chochote kwa lengo la kusomwa na kupelekea kushusha hadhi, kusababisha chuki au kashfa kwa mtoto wa Mfalme wa kigeni, Balozi, au kiongozi wa nje.

Au kwa lengo la kuchafua amani na urafiki kati ya Zanzibar na nchi ambayo mtu huyo anatoka.


Kosa jengine ni kuchapisha au kueneza jina au kitu chochote kitakachofichua jina la muathirika wa makosa ya kujamiiana (mfano mtu aliebakwa).

Adhabu kwa kosa hili ni kifungo kisichozidi miaka miwili au faini isiyozidi shilingi 300,000.

Isipokwa kama kuna amri ya maandishi ya afisa husika wa kituo cha polisi au afisa mpelelezi wa kosa hilo kwa nia njema (good faith) na kwa lengo la upelelezi, au kwa ruhusa ya maandishi ya muathirika (victim) au kama muathirika amefariki au ni mtoto mdogo au mwendawazimu kwa ruhusa ya jamaa wa karibu wa muathirika huyo na kwa ruhusa ya afisa husika wa kituo cha polisi.

Au kwa ruhusa ya mahakama katika kuchapisha jina la muathirika kinyume chake mtu atakaefanya hivyo bila ya ruhusa atakuwa amefanya kosa la jinai.

No comments:

Post a Comment