Friday, April 9, 2010

Uvimbe wa Ini sasa watibiwa bila kupasuliwa Mnazi Mmoja

Na Juma Khamis

KWA mara ya kwanza katika historia ya Zanzibar, madaktari bingwa wa upasuaji kutoka China, wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji wagonjwa watano waliokuwa wakisumbuliwa na uvimbe wa usaha katika ini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, daktari bingwa wa upasuaji Dk. Yong Shi, alisema wagonjwa hao walikuwa wakikabiliwa na ugonjwa unaosababishwa na mkusanyiko wa usaha katika ini (liver abscess).

Alisema upasuaji huo ambao ni wa kwanza kufanyika Zanzibar, umechukua dakika mbili tu kwa kila mgonjwa na unafanywa kwa utaalamu wa hali ya juu.

Upasuaji huo unaofanywa kwa muongozo wa Ultra Sound, ni wa kisasa na maarufu katika nchi nyingi duniani, lakini kwa Zanzibar ni mara ya kwanza kufanyika.

Mgonjwa hutobolewa sehemu ndogo ya tumbo na kupenyezwa kifaa maalum (tube) ambacho kwa wakati mmoja kina uwezo wa kutibu na kuingiza dawa kwenye sehemu iliyoathirika.

Dk. Yong alisema kabla ya teknolojia hiyo mpya kwa Zanzibar, mgonjwa kama huyo angelazimika kupasuliwa sehemu kubwa ya tumbo na kuondolewa sehemu iliyoathirika, kitendo ambacho ni hatari kwa maisha ya mgonjwa.

Alisema teknolojia hiyo, haina maumivu yoyote kwa mgonjwa na anaweza kupata nafuu katika kipindi kifupi tokea afanyiwe upasuaji.

“Upasuaji huu hauna maumivu kwa mgonjwa, mgonjwa anaweza kupona haraka, kuliko upasuaji uliokuwa ukifanywa kabla,” alisema Dk. Yong.

Alisema dalili za ugonjwa huo ni maumivu makali ya tumbo, homa na mgonjwa huwa hawezi kupinda.

“Kwa Zanzibar mgonjwa kama huyu angelazimika kufanyiwa upasuaji mkubwa na kukatwa sehemu kubwa sana ambayo inachukua muda mrefu kupona. Bila shaka upasuaji huu umefanikiwa kwa kiasi kikubwa, na tunajivunia,” alisema.

Akizungumzia ugonjwa wa vijiwe katika damu (blood stones), Dk. Shi alisema Wazanzibari wengi wanasumbuliwa na ugonjwa huo.

Aidha alisema, wengi wanaokwenda hospitali kwa kesi za kusumbiliwa uvimbe, vibofu vya mkojo au vijiwe kwenye damu ni wanaume na wanawake huenda hospitali wakiwa tayari wameshaathiriwa na maradhi hayo.

Mapema, mgonjwa Ali Juma ambae amefanyiwa upasuaji wa usaha katika ini aliliambia gazeti hili, kuwa maisha yake sasa yameokoka baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Juma ambae amehamishiwa hospitali ya Mnazi Mmoja akitokea hospitali ya Abdalla Mzee, Pemba, alisema kabla ya upasuaji alikuwa akipata maumivu makali ya tumbo na homa za mara kwa mara na kushindwa kufanya kazi zake vizuri kwa kuwa alishindwa kuinama na kupinda.

Akionekana mkakamavu, siku chache tu baada ya upasuaji huo, Juma alisema hali yake ya afya imerejea ya kawaida na hakuna maumivu yoyote aliyopata na anayopata baada ya upasuaji huo.

Dk. Shi alifanya upasuaji huo akisaidiwa na daktari wazalendo, akiwemo Dk. Suleiman Aboud Jumbe.

2 comments:

  1. is this service still available please,notfy me

    ReplyDelete
  2. my phone ,0712401386 please notify me if that services is still available

    ReplyDelete