Friday, April 9, 2010

Ushahidi ni tegemeo muhimu kwa maamuzi ya mahakama

Na Juma Khamis
KIMSINGI mahakama ambayo ni moja ya mihimili mikuu mitatu ya dola, ndicho chombo chenye mamlaka ya kusikiliza au kuamua mashauri na kesi mbali mbali zinazoibuka miongoni mwa jamii.
Katika kusimamia na kutimiza wajibu wake kisheria hutegemea uwasilishaji wa ushahidi wa pande zote mbili katika kesi, yaani ushahidi wa upande wa mashtaka (Prosecution side) ambao kwa kawaida ndio unaoanzisha kesi na upande wa utetezi (Defensive side).
Ni kwa kuzingatia ushahidi huo ndio mahakama huwa na uwezo wa kupima na kuchambua kwa kina ushahidi uliowasilishwa kabla ya kuamua ni upande upi katika kesi una haki au upande upi umeshindwa kutokana na udhaifu wa ushahidi wake.
Kwa mujibu wa sheria ya ushahidi, ushahidi wa kusikia au kwa lugha ya kisheria ‘hear say evidence’ ni moja kati ya aina mbali mbali za ushahidi unaoweza kutumika katika kuthibitisha ukweli wa shauri lililofunguliwa mahakamani.
Hata hivyo, kimsingi aina hii ya ushahidi ni miongoni mwa ushahidi usiokubalika kutumika katika kuthibitisha kesi yoyote mahakamani, isipokuwa katika mazingira fulani.

Ushihidi wa kusikia, unatokana na maelezo ya kusikia kutoka kwa mtu mwengine ambaye ndiye aliyeshuhudia tukio lililoshuhudiwa.
Wanataaluma mbali mbali wa sheria (Jurists) wametafsiri kwamba ushahidi wa kusikia (Hear say Evidence) ni aina ya ushahidi ambao maelezo yake yametolewa na shahidi ambaye kimsingi hawezi kuutolea ushahidi mahakamani.
Yaani ushahidi ambao hutolewa na mtu ambae yeye binafsi hajashuhudia tukio, isipokuwa kwa kusikia tu kutoka kwa wengine.
Sababu ya kukataliwa kwa aina hii ya ushahidi katika kuthibitisha madai mahakamani ni kwamba haiwezekani katika hali ya kawaida kumuhoji shahidi juu ya kama hilo linalozungumzwa na mwengine ni la kweli au la.
Hii inawezekana pale tu inapotokea mtoaji halisi wa taarifa anapokuwa mahakamani kama shahidi, yaani shahidi aliyeshuhudia ukweli husika.
Sababu yengine inatokana na tabia ya kibinadamu. Hakuna mtu anaebisha kwamba ushahidi unaotolewa kwa kukariri au kurudia kilichosemwa na mwengine huwa na tabia ya kupotosha ukweli kwa kuwa kuna taarifa zitapunguzwa uhalisia wake na nyengine zitatiwa chumvi.
Sababu nyengine muhimu ni kutokana na wakati shahidi anapojaribu kurudia kauli ambayo aliitoa awali inakua na nguvu zaidi ikilinganishwa na kauli au taarifa za kusikia kutoka kwa mtu wa pili.
Kwa kawaida ushahidi hutengenezwa aidha kwa kuzungumza kwa mdomo au maelezo ya uthibitisho wa jambo, pia inaweza kwa kutumia mtindo wa kuwasilisha nyaraka (documents) zinazothibitisha ukweli mbele ya mahakama.
Pia inaweza kuhusisha aina yoyote ya mawasiliano ilimradi tu ni katika kuthibitisha.
Njia hizi zote zinaweza kuwa ni moja kwa moja au kupitia mtu mwengine.
Endapo ushahidi huo utatolewa kwa nia ya kutaka kuthibitisha uhalali kwa kauli iliyotumika, basi ushahidi huo utakuwa ni wa kusikia na hivyo hautakubalika mahakamani.
Ushahidi unaokubalika na mahakama ni ule wa kuthibitisha kauli inayothibitisha ukweli wa shauri au kesi hiyo.

No comments:

Post a Comment