Saturday, April 10, 2010

Ni jukumu la mwari kumtaja mtu aliempa ujauzito

Na Juma Khamis
SHERIA ya kuwalinda wari na watoto wa mzazi mmoja, ni moja ya sheria nyingi zilizotungwa na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Sheria hii ilitungwa kutokana na kukithiri kwa matukio ya udhalilishaji wa wari na watoto wadogo, lengo likiwa ni kukomesha unyanyasi huo.

Hata hivyo, licha kuwepo sheria hii, lazima tukiri kwamba bado vitendo vya kuwadhalilisha wari vimekuwa vikiendelea, huku wari wangi wakipewa ujauzito na kuishia kuolewa.

Sheria hii inaelezea kwa kina makosa mbali mbali ya jinai ambayo hayakuelezwa na sheria ya makosa ya Jinai (Penal Act No.6 ya mwaka 2004).

Kabla ya kuzungumzia baadhi ya makosa ya jinai katika sheria hii, kwanza tuone maana ya ‘mwari’ kama mmoja ya mlengwa wa sheria hii.

Kwa mujibu wa kifungu cha pili cha sheria hii, mwari ni mwanamke asiepata kuolewa ambaye yuko baina ya umri wa miaka 18 na miaka 21 na asiyepata kuzaa mtoto.

Baadhi ya makosa yanayotambuliwa na sheria hii ni pamoja mwari atakaepatikana na ujauzito ambao ameupata kwa hiari yake.

Adhabu katika kosa hili iwapo atatiwa hatiani ni kutumikia jamii kwa kipindi cha kuanzia miezi mitatu tokea siku aliyojifungua.

Sheria hii pia imebainisha kuwa mtu yeyote atakaehusika na ujauzito wa mwari huyo atakuwa amefanya kosa na pindi atakapotiwa hatiani adhabu yake ni kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu na si zaidi ya miaka mitano .

Pamoja na adhabu hiyo atatakiwa atoe matunzo kwa mtoto atakaezaliwa na mwari huyo.

Sheria pia imesema kuwa ni jukumu la mwari yeyote atakaekuwa mjamzito kutaja jina la mtu aliempa ujauzito huo na pindi mwari huyo atakataa kutaja jila mtu huyo atakuwa ametenda kosa la jinai na endapo atatiwa hatiani adhabu yake ni kutumikia jamii kwa kipindi cha miezi mitatu.

Hata hivyo, itakuwa ni kingi kwa mwari huyo kama atathibitisha kuwa ujauzito huo ameupata kutokana na kubakwa na watu wengi au mazingira mengine ambayo hakuweza kumtambua mbakaji.

Iwapo mwari huyo kwa makusudi amemtaja mtu tofauti na aliyemsababishia ujauzito huo, na kama mahakama itaridhika amefanya hivyo kwa makusudi, atakuwa ametenda kosa la jinai na akipatikana na hatia atatumikia jamii kwa kipindi cha miezi sita.

No comments:

Post a Comment