Saturday, April 10, 2010

Kanali Kima atangaza kugombea Ubunge Chwaka

KANALI mstaafu wa JWTZ, Said Ali Khamis, maarufu Said Kima, ametangaza azma yake ya kugombea nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Chwaka, kupitia chama tawala cha CCM.

Akizungumza katika mahojiano maalum nyumbani kwake Chukwani, Kima ambae aligombea nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2005, alisema lengo lake ni kushirikiana na watu wa Chwaka kuliletea maendeleo Jimbo hilo.

Kanali huyo alishindwa na Mbunge wa sasa wa Jimbo hilo, Yahya Kassim.

Kima ambae aliwahi kuwa rubani wa ndege ya Rais wa serikali ya awamu ya pili ya Zanzibar, alisema anataka yale mazuri aliyoyapata kuyafanyia kazi kwa maslahi ya watu wa Chwaka na wilaya nzima ya Kati.

“Sina uwezo wa kuleta maendeleo peke yangu, lakini kwa sababu nimejifunza mengi mazuri, nitashirikiana na watu wa Chwaka kuhakikisha tunapata maendeleo,” alisema.

Mgombea huyo ambae ni mwanachama hai wa CCM alielipia kadi yake hadi mwaka 2013, alisema kama atashinda, Chwaka itakuwa Jimbo la mfano kwa maendeleo katika wilaya ya Kati.

Akizungumzia suala la elimu, Kima alisema inasikitisha kuona wilaya nzima ya kati haina skuli ya sekondari ya juu na hivyo, atahakikisha anatumia ushawishi alionao pamoja na wabunge wengine wa wilaya hiyo, kuipatia wilaya ya Kati skuli ya aina hiyo.

“Chwaka tumebahatika kuwa na Chuo Kikuu, lakini wanafunzi wengi wanaoingia pale ni kutoka nje ya Chwaka na wilaya ya kati, inasikitisha sana kuona tumeshindwa hata kuanzisha skuli ya elimu ya juu katika wilaya yetu,” alisema.

“Lazima tukubali kuwa wilaya ya Kati tuko nyuma sana kielimu na sasa muda umefika wa kusema basi na inatosha kuwa watu wa mwisho,” alisema.

Kanali Kima ambae aliwahi kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Zanzibar, alisema lengo lake jengine ni kuhakikisha barabara ya Ukongoroni inajengwa kwa kiwango cha lami katika kipindi kifupi.

“Suala la Ukongoroni linanisikitisha, kama Mungu atanijaalia nikashinda, basi barabara hii itajengwa katika kipindi kifupi sana,” aliongeza.

Kujitangaza kwa Kima kunachukuliwa kama changamoto kubwa kwa Mbunge wa sasa, ambae kuna dalili ya kuomba kurejea tena katika Jimbo hilo kwa awamu ya nne (miaka 20), ingawa bado hajathibitisha.

No comments:

Post a Comment