Friday, April 9, 2010

China yaipatia Zanzibar msaada

SERIKALI ya China imeipatia msaada wa vifaa mbali mbali vya kisasa vyenye thamani ya shilingi milioni 64 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vya uimarishaji wa huduma za afya katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja.

Vifaa hivyo vitatumika katika hospitali ya Mnazimmoja kwa ajili ya huduma za upasuaji pamoja na sehemu ya macho.

Akipokea msaada huo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Sultan Mohammed Mughery amesema kuwa China imefanikisha kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza sekta ya afya kwa Unguja na Pemba.

Amesema msaada huo walioutoa utawezesha katika kufanya kazi hizo kwa urahisi na ufanisi mkubwa wa kuwahudumia wananchi wa Zanzibar.

Aidha Waziri Mughery amesifu jitihada za Serikali za China katika kuwapatia wataalamu mbali mbali ikiwemo wa maradhi ya wanawake kwa Hospitali kuu ya Mnazimmoja, macho pamoja na sehemu nyemgine.

Ameahidi kuwa vifaa hivyo vitatumika kwa uwangalifu ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kusaidia utoaji wa huduma kuwa zenye ubora wa hali ya juu.

Nae kiongozi wa madaktari kutoka nchini China Dk Zhu Xiangjuan amesema nchi yake itaendeleza kila aina misaada kwa Zanzibar katika kustawisha maisha ya wazanzibari kwa huduma za afya.

Amesema wataendeleza kuwapatia madaktari vifaa pamoja na mafunzo kwa wafanyakazi wa Zanzibar ili waweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi wa hali ya juu.

China na Zanzibar imekuwa marafiki kwa kipindi cha miaka 46 sasa na wanaendelea kuisaidia Zanzibar katika nyanja tofauti ikiwemo madaktari pamoja na mambo mbali mbali na sasa wapo madaktari wapatao 21 ambao wanatoa huduma za kiafya kwa Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment