Saturday, April 24, 2010

Utaratibu wa uendeshaji kesi za jinai

Na Juma Khamis
KATIKA mada hii tunakusudia kuanisha utaratibu wa kisheria kuhusu uendeshaji wa mashauri ya jinai.

Kimsingi ni muhimu kuweka bayana mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanagusa mwenendo mzima wa uendeshaji wa kesi za jinai na haki za wahusika yaani walalamikaji, watuhumiwa wa makosa, washitakiwa na wale waliopatikana na hatia.Wadau katika usimamizi wa haki katika mwenendo wa jinai ni jamii nzima kwa ujumla.

Hata hivyo, jamii inawakilishwa na vyombo vilivyopewa mamlaka kisheria.

Vyombo hivyo ni Mamlaka ya Upelezi yaani Polisi, Mamlaka ya Uendeshaji wa Mashtaka ambayo ni ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Mamlaka ya kusikiliza za kutoa uamuzi wa mashtaka hayo yaani Mahakama.

Hebu kabla hatujasonga mbele zaidi tuangalie makosa ya jinai na mashauri ya madai.

Ili kupata ufahamu wa kutosha na kuweza kuzingatia zaidi mada hii, ni vyema tukatofautisha walau kwa mukhtasari makosa ya jinai na mashauri ya madai.

Jinai kama ilivyotafsiriwa na vitabu mbali mbali vya sheria ni kutenda au kutokutenda jambo kunakomfanya mtu aadhibiwe kisheri.

Kwa ufafanuzi zaidi makosa ya jinai ni yale ambayo jamii inayaona bayana kuwa ni makosa yanayoigusa na mwenye kuyatenda anastahili kupewa adhabu kisheria.

Makosa haya yameanishwa katika sheria ya adhabu na katika vitabu vyengine vinavyohusika na upewaji adhabu kutokana na makosa mengineyo.

Kimsingi katika makosa ya jinai Dola, Jamhuri au serikali ndiyo hulalamika, kwa hivyo uhusiano wakisheria katika jinai ni baina ya mshitakiwa na Mamlaka ya nchi.

Kwa upande mwengine mashauri ya madai yanahusisha watu binafsi kutokana na kudaiana haki zao zinazotokana na mahusiano yatokanayo na makubaliano au kuaminiana kisheria ambapo mtu mmoja hakutekeleza makubaliano hayo au hakulipa anachodaiwa.

Madai kwa mujibu wa sheria hayahusishi adhabu bali mdaiwa hutakiwa kulipa au kutekeleza wajibu kutokana na makubaliano yaliyofikiwa.


Lakini kwa faida ya wasomaji, katika mada hii tutazingatia zaidi makosa ya jinai na jinsi ya kuyaendesha.

Mahakama zote zimepewa uwezo wa kusikiliza kesi za jinai kwa mujibu wa sheria.

Uwezo wa mahakama na mahakimu umeelezwa na sheria ya Mahakimu wa Mahakama za mwanzo, wilaya na za mkoa.

Ukubwa au umaalum wa kesi huzingatiwa katika kuamua ni mahakama ipi kesi ifunguliwe.

Katika kutekeleza hayo sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai imeeleza uwezo wa kutoa adhabu kwa mahakama zote.
Mahakama kuu ina uwezo wa kutoa adhabu yoyote au kutoa amri yoyote zilizoruhusiwa na sheria.

Kifungu cha 7 cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinaeleza uwezo huo.

Kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha sheria hiyo, mahakama ya mkoa imepewa uwezo wa kutoa adhabu ya kifungo kisichozidi miaka saba, faini isiyozidi shilingi milioni nne, kutumikia jamii kwa muda usiozidi miezi 12.

Mahakama ya wilaya nayo imepewa nguvu katika kifungu cha 9 kutoa adhabu ya kifungo kisichozidi miaka mitanom, faini isiyozidi shillingi milioni mbili na kutumikia jamii kwa kipindi kisichozidi miezi sita.

Kifungu cha 10 kinaipa uwezo mahakama ya mwanzo kutoa adhabu ya kifungo kisichozidi miezi mitatu, faini isiyozidi shilingi 100,000 na kutumikia jamii kwa kipindi kisichozidi miezi miwili.

Adhabu hizo za kutumikia jamii zimewekwa kwa mujibu wa kanuni za kutumikia jamii kanuni zilizotungwa na Jaji Mkuu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa jinai, Mahakama ya mkoa imepewa uwezo wa kutoa adhabu kubwa zaidi hata kufikia kifungo cha maisha cha maisha ikwa baadhi ya makosa kwa mfano makosa yaliyotajwa na vifungu vya 125, 132, 150, 151, 160, 161, 286, 287, 324, 342(3),(4) na 343 vya sheria ya adhabu No.6/2004.

Mahakama hizo pia zaweza kuwa na nguvu zaidi iwapo zitapewa nguvu hizo na sheria ya Mahakimu wa Mahkama.

Kuhusu uwezo wa kusikiliza kesi za watoto (Juveniles) mahakama iliyopewa uwezo huo kwa mujibu wa sheria ni mahakama ya mkoa.

Watoto wasiozidi umri wa miaka 16 ndio husikilizwa katika mahakama za watoto.

Ukamataji, Upekuzi na Haki zake
Miongoni mwa hatua za awali kuhusiana na usimamizi wa m wenendo wa Jinai ni ukamataji na upekuzi wa watuhumiwa.

Namna ya ukamataji imeelezwa katika kifungu cha 13 cha sheria ya Mwenendo wa Jinai kwamba Polisi au mtu mwengine anapomkamata mtu analazimika kumgusa mtu huyo anayetakiwa kukamatwa.

Kifungu kidogo cha (2) cha kifungu hicho kinamtaka mkamataji kutumia kila njia muhimu kufanikisha ukamataji huo.

Ukamataji umegawanyika katika makundi mawili.

Ukamataji bila ya kutumia hati ya kukamata umeelezwa katika kifungu cha 21 cha sheria ya Mwenendo wa Jinai ambapo Polisi wanaruhusiwa kukamata watuhumiwa au wahalifu waliotenda au wanaotenda makosa yanayoonekana au kujulikana wazi wazi.

Zaidi ya makosa hayo yaliyotajwa na kifungu cha 21, makosa mengine yote yanayosalia yanahitaji kwanza hati ya kukamata (Arrest warrant), ambayo hutolewa na mahakama pekee.

Katika kufanikisha ulamataji, mambo mengine hutokea kama vile upekuaji wa eneo alilokamatwa mtuhumiwa kwa mujibu wa kifungu cha 14, ruhusa ya kuvunja ili kukamata au kuvunja ili kutoka iwapo mkamataji amefungiwa ndani kama kinavyoeleza kifungu cha 15.

Sheria pia inawapa watu binafsi au raia wa kawaida uwezo wa kukamata, kama ilivyoanishwa katika kifungu cha 26 na 44 kwa mahakimu kulingana na makosa na aina ya makosa hayo na namna yalivyotendeka.

Upekuzi: Hatua hii inahusu upekuzi wa watu na upekuzi wa maeneo.

Mtu aliyekamatwa hupekuliwa na Polisi na mali/vitu vyake au vilivyokamatwa miongoni mwake huhifadhiwa kwa mujibu wa kifungu cha 17.

Lakini kama tulivyoona awali eneo ambalo mtu anayekamatwa amepatikana hupekuliwa pia.

Sheria pia inawapa polisi uwezo wa kusimamia na kupukua gari na vyombo mbali mbali vya usafiri na usafirishaji iwapo kuna hisia au tuhuma za kuwepo mali au mhalifu katika vyombo hivyo kama ilivyoolezwa katika kifungu cha 18.

Lakini kifungu cha 19 kimezingatia stara ya mwanamke kwa kutana upekuzi wake ufanywe na wanawake wenziwe.

Kwa ujumla ukamataji na upekuzi ni matukio yanayokwenda pamoja na kwa mujibu wa sheria zipo haki ya msingi ambazo lazima zitekelezwe katika hatua hizo.

Haki za mtuhumiwa/mshitakiwa
Haki hizi zinaanzia wakati wa kukamatwa. Kifungu cha 30 kinamtaka mkamataji kujitambulisha na amweleze mkamatwaji makosa yake.

Haki nyegine ni ile ya kutowekwa ndani zaidi ya saa 24 bila ya kufikishwa mahakamani kama ilivyoanishwa katika kifungu cha 24.

Kifungu cha 32 kimakataza Polisi kumuweka mtu kizuizini bila ya sababu za msingi.

Mtu aliyekamatwa huhojiwa kuhusiana na tuhuma dhidi yake, hata hivyo kifungu cha 33 kinaelezea kwamba muda huo wa kuhojiwa usizidi saa nne au ikibidi kuongezwa muda huo kwa mujibu wa kifungu cha 34 basi usizidi saa nane au maombi ya kuzidishwa muda yapelekwe kwa Hakimu.

No comments:

Post a Comment