Thursday, August 12, 2010

Wabunge, Wawakilishi twambieni mtafanya nini kupunguza mimba kwa wanafunzi wa kike?

SKULI za awali, msingi na sekondari sasa zimeenea kila kona ya Zanzibar.

Wazanzibari wameitikiwa kwa vitendo wito wa serikali wa kuwataka kuanzisha skuli katika maeneo yao huku serikali nayo ikiunga mkono kwa upande wake lengo ni kukidhi mahitaji ya wanafunzi hasa kutokana na kuwepo idadi kubwa ya wanafunzi wanaomaliza skuli za msingi na kuhitaji kuingia sekondari.

Sitaki kuzungumzia yote, leo hii nachagua tatizo moja tu ambalo ni wanafunzi wengi wa kike kupata ujauzito na hivyo kulazimika kukatisha masomo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (2010), kila mwaka kiasi cha wanafunzi 50 wa kike hukatisha masomo kutokana na kupewa ujauzito, hali ambayo huwafanya wanafunzi kufuta kabisa ndoto zao za kujiimarisha katika maisha yao ya baadae na kuendelea kuwa tegemezi.

Inawezekana tatizo hili limekuwa kubwa zaidi kutokana na kuachiwa walimu na wazee peke yao, huku wabunge, wawakilishi na madiwani ambao wana wajibu mkubwa wa kusimamia skuli hizi kwa mambo yote ya kulea wanafunzi wanaosoma, wakilipa kisogo tatizo hili.

Wao wamezigeuza skuli kama sehemu ya mradi wa kupata kura za wananchi wa maeneo hayo mara uchaguzi unapokaribia.

Nasema hivyo kwa vile mwanasiasa anapopata fursa ya kwenda kutembelea skuli, anapeleka tu msaada wa mabati au saruji, ili aweke kwenye orodha ya mambo aliyoyafanya wakati wa uongozi wake, lakini hawatengi muda wa kuzungumza na wanafunzi mara wanapotembelea skuli hizo.

Wengi wanakwenda kutoa msaada ilimradi waonekane wamefanya mambo mengi kusaidia skuli zilizo katika majimbo yao, wakisahau kwamba kumbe wanafunzi wanajitaji msaada mkubwa zaidi wa kupewa elimu ya kujitambua kutoka kwa viongozi wao.

Kwa bahato nzuri nimekuwa nikipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wanafunzi na kuwauliza kama wamewahi angalau kukaa na Wawakilishi wao, Wabunge au Madiwani kuzungumzia matatizo yao, wengi walikiri kuwa hawajawahi.

Wanafunzi wengine hawafahamu hata majina ya wabunge, wawakilishi na madiwani wao na wengine hata sura zao.

Hii ni ishara kuwa licha ya wanasiasa kudai kuwa wanatembelea skuli zao; lakini hawatoi fursa ya kuzungumza na wanafunzi.

Hali hii imefanya hata ukizungumza na wabunge, wawakilishi na madiwani licha ya kujigamba kutembelea skuli hizo, lakini hawana takwimu sahihi za idadi ya wanafunzi wanaoacha shule kwa sababu ya ujauzito.

Kinakera zaidi i kwa diwani ambaye anashughulika na skuli moja pengine kwenye wadi yake, naye hana takwimu za wanafunzi wanaokatisha masomo kwa tatizo la mimba katika skuli yake.

Hii ni kwa sababu diwani akienda kwenye skuli jambo la maana analoona ni kusimamia ujenzi wa nyumba ya mwalimu au kuangalia ujenzi wa vyumba vya madarasa na kama wazazi wametoa mchango kwa ajili ya ujenzi wa darasa au nyumba ya mwalimu.

Hii ni kazi nzuri wanayofanya wanasiasa wetu majimboni, lakini kinachochefua ni kuona viongozi hawa ambao tumewapa dhamana ya kutuongoza, wanaonekana hawajali tatizo la wanafunzi ambao wanakatisha masomo kwa ujauzito.


Hii ina maana kuwa kitendo cha viongozi hawa wa kisiasa kutokerwa na tatizo hili la wanafunzi kupata ujauzito, ndicho kinachofanya wasisumbuke kuzungumzia suala hilo.

Tabia hii ya wanasiasa wetu kutofanya suala la mimba kuwa ajenda yao ya kisiasa, limefanya tatizo hili kuongezeka na iwapo hali hii ikiachwa iendelee, wanafunzi wengi wa kike wanaofaulu hawatamaliza masomo yao.

Ni wakati muafaka sasa, kwamba suala hili liwe ajenda ya wanasiasa, wayaone matatizo mengi yanayowafanya wanafunzi hawa wapate ujauzito ili waweze kuyashughulikia.

Bila kufanya hivyo matatizo yanayochangia wanafunzi hao kupata ujauzito, yataendelea kuwepo na idadi ya wanaopata ujauzito itaongezeka.

Naomba wagombea watakaopitishwa na vyama vyao kugombea, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani waliingize kwenye ajenda suala hili ili kuokoa watoto hawa wa kike wasikatishe masomo.

Watwambie wakati wa kampeni watafanya nini kupunguza au kulimaliza tatizo hili linalozikabili skuli nyingi za kata.
Ingawa kwa upande wake serikali kuu, imechukua juhudi za makusudi kuhakikisha wanafunzi wanaokatisha masomo kwa ujauzito wanarejea skuli baada ya kujifungua, utekelezaji wa sera hii mihimu kuwekewa msisitizo ili kuhakikishwa wanafunzi wa kike wanapata fursa sawa ya elimu na wanaume.

Tunaamini kwa pamoja tunaweza kuliweka tatizo la mimba kwa wanafunzi kuwa ajenda muhimu kwa jamii yetu.

Michango, misaada kwa wagombea na vyama vya siasa isitolewe wakati wa kampeni

Taarifa ya gharama itakayotolewa na mgombea, kwa madhumuni ya sheria hii, na pasipokuwa na sababu nyegine itachukuliwa kuwa ni ushahidi unaotosha kuwa mgombea amewasilisha taarifa ya fedha kwa Katibu wa Chama wa Wilaya au Katibu Mkuu atatoa hati ya uthibitisho kuwa mgombea huyo ametekeleza sheria.

Kwa kuzingatia umuhimu wa shreia hii, michango ya hiyari na zawadi zinazotolewa kwa chama na wagombea inataka pawepo na uwazi katika utoaji wake.

Sheria inaeleza kwamba kila chama cha siasa kilichopokea michango inayozidi shilingi milioni moja kutoka kwa mchangiaji binafsi au shilingi milioni mbili kutoka kwa taasisi kitoe taarifa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kujaza fomu maalum.

Sheria pia inataka fedha hizo zihifadhiwe katika hesabu ya benki (account) maalum itakayofunguliwa kwa ajili hiyo.

Fedha hizo zitalipwa na kutumika kutoka account hiyo, kama ilivyoelezwa na sheria hii katika kifungu cha 11(1).

Sheria pia inafafanua utaratibu wa vyama au wagombea kupata misaada kutoka nje ya nchi.

Sheria inazuia michango na misaada hiyo isitolewe wakati wa kampeni.

Inaruhusu Vyama vya Siasa au wagombea kupokea misaada kutoka nje ya nchi siku tisini (90) kabla ya uchaguzi mkuu au siku thelathini (30) kabla ya uchaguzi mdogo.

Pia inataka kuwepo uwazi na taarifa itolewe kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Uwajibikaji wa Asasi zisizo za Kiserikali

Sheria hii inaweka pia sharti la uwajibikaji kwa taasisi zisizo za kiserikali, vikundi vya kidini au vikundi vya kijamii ambavyo, kwa madhumuni ya uchaguzi vingependa kushiriki kwa:

(a) Uhamasishaji au

(b) Kuelimisha jamii katika mwenendo wa kampeni za uchaguzi. Vikundi hivi vinatakiwa kutoa taarifa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu gharama zilizotumika katika uchaguzi ndani ya siku tisini (90) baada ya uchaguzi.

Pia sheria inaeleza kuwa taasisi hizi au vikundi vya kijamii hivyo, havitaruhusiwa kutumia gharama zaidi ya kiwango kilichoanishwa katika kanuni.

Hivyo basi taasisi za kiraia, taasisi za kidini au taasisi za kijamii itakayaohusika katika kuchangia shughuli za uchaguzi inayo wajibu wa kutunza taarifa za fedha zinazoelezea mapato na matumizi hayo.

Viwango vya gharama za uchaguzi

Sheria ya gharama za uchaguzi inaweka utaratibu wa kudhibiti gharama za uchaguzi kwa kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana kuweka viwango vya gharama za uchaguzi.

Viwango hivyo vimezingatia, tofauti ya majimbo, idadi ya watu, aina ya wagombea pamoja na miundombinu.

Kwa mfano, kwa wagombea Ubunge kiwango cha chini ni milioni 30, wakati kiwango cha juu ni milioni 80 na viti maalum isioyozidini shilingi milioni 10.

Hivyo basi chama au mgombea atakayevuka kiwango kilichowekwa lazima atoe maelezo ya kuridhisha bila kufanya hivyo atakuwa ametenda kosa.

Lengo ni kujenga nidhamu na usawa miongoni mwa vyama vya siasa na wagombea katika uchaguzi.

Mgawanyo wa matumizi baina ya Chama na mgombea

Sheria ya gharama za uchaguzi katika kifungu cha 17(1) kinaruhusu mgawanyo wa gharama za uchaguzi zilizotumika na mgombea mwenyewe na zile ambazo chama cha siasa kimetumia kumtangaza mgombea pamoja na mikutano yote; kwa hali hiyo chama kitafanya mambo yafuatayo.

a) Kuweka mgawanyo ulio wazi baina ya matumizi ya mgombea kadiri itakavyowezekana na yale yaliyoyofanywa na chama.

b) Ndani ya siku 30 baada ya kupiga kura chama kitamfahamisha mgombea kiasi cha gharama kilichogawanywa ambacho kitakuwa ni sehemu ya gharama za uchaguzi za mgombea.