Thursday, August 12, 2010

Wabunge, Wawakilishi twambieni mtafanya nini kupunguza mimba kwa wanafunzi wa kike?

SKULI za awali, msingi na sekondari sasa zimeenea kila kona ya Zanzibar.

Wazanzibari wameitikiwa kwa vitendo wito wa serikali wa kuwataka kuanzisha skuli katika maeneo yao huku serikali nayo ikiunga mkono kwa upande wake lengo ni kukidhi mahitaji ya wanafunzi hasa kutokana na kuwepo idadi kubwa ya wanafunzi wanaomaliza skuli za msingi na kuhitaji kuingia sekondari.

Sitaki kuzungumzia yote, leo hii nachagua tatizo moja tu ambalo ni wanafunzi wengi wa kike kupata ujauzito na hivyo kulazimika kukatisha masomo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (2010), kila mwaka kiasi cha wanafunzi 50 wa kike hukatisha masomo kutokana na kupewa ujauzito, hali ambayo huwafanya wanafunzi kufuta kabisa ndoto zao za kujiimarisha katika maisha yao ya baadae na kuendelea kuwa tegemezi.

Inawezekana tatizo hili limekuwa kubwa zaidi kutokana na kuachiwa walimu na wazee peke yao, huku wabunge, wawakilishi na madiwani ambao wana wajibu mkubwa wa kusimamia skuli hizi kwa mambo yote ya kulea wanafunzi wanaosoma, wakilipa kisogo tatizo hili.

Wao wamezigeuza skuli kama sehemu ya mradi wa kupata kura za wananchi wa maeneo hayo mara uchaguzi unapokaribia.

Nasema hivyo kwa vile mwanasiasa anapopata fursa ya kwenda kutembelea skuli, anapeleka tu msaada wa mabati au saruji, ili aweke kwenye orodha ya mambo aliyoyafanya wakati wa uongozi wake, lakini hawatengi muda wa kuzungumza na wanafunzi mara wanapotembelea skuli hizo.

Wengi wanakwenda kutoa msaada ilimradi waonekane wamefanya mambo mengi kusaidia skuli zilizo katika majimbo yao, wakisahau kwamba kumbe wanafunzi wanajitaji msaada mkubwa zaidi wa kupewa elimu ya kujitambua kutoka kwa viongozi wao.

Kwa bahato nzuri nimekuwa nikipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wanafunzi na kuwauliza kama wamewahi angalau kukaa na Wawakilishi wao, Wabunge au Madiwani kuzungumzia matatizo yao, wengi walikiri kuwa hawajawahi.

Wanafunzi wengine hawafahamu hata majina ya wabunge, wawakilishi na madiwani wao na wengine hata sura zao.

Hii ni ishara kuwa licha ya wanasiasa kudai kuwa wanatembelea skuli zao; lakini hawatoi fursa ya kuzungumza na wanafunzi.

Hali hii imefanya hata ukizungumza na wabunge, wawakilishi na madiwani licha ya kujigamba kutembelea skuli hizo, lakini hawana takwimu sahihi za idadi ya wanafunzi wanaoacha shule kwa sababu ya ujauzito.

Kinakera zaidi i kwa diwani ambaye anashughulika na skuli moja pengine kwenye wadi yake, naye hana takwimu za wanafunzi wanaokatisha masomo kwa tatizo la mimba katika skuli yake.

Hii ni kwa sababu diwani akienda kwenye skuli jambo la maana analoona ni kusimamia ujenzi wa nyumba ya mwalimu au kuangalia ujenzi wa vyumba vya madarasa na kama wazazi wametoa mchango kwa ajili ya ujenzi wa darasa au nyumba ya mwalimu.

Hii ni kazi nzuri wanayofanya wanasiasa wetu majimboni, lakini kinachochefua ni kuona viongozi hawa ambao tumewapa dhamana ya kutuongoza, wanaonekana hawajali tatizo la wanafunzi ambao wanakatisha masomo kwa ujauzito.


Hii ina maana kuwa kitendo cha viongozi hawa wa kisiasa kutokerwa na tatizo hili la wanafunzi kupata ujauzito, ndicho kinachofanya wasisumbuke kuzungumzia suala hilo.

Tabia hii ya wanasiasa wetu kutofanya suala la mimba kuwa ajenda yao ya kisiasa, limefanya tatizo hili kuongezeka na iwapo hali hii ikiachwa iendelee, wanafunzi wengi wa kike wanaofaulu hawatamaliza masomo yao.

Ni wakati muafaka sasa, kwamba suala hili liwe ajenda ya wanasiasa, wayaone matatizo mengi yanayowafanya wanafunzi hawa wapate ujauzito ili waweze kuyashughulikia.

Bila kufanya hivyo matatizo yanayochangia wanafunzi hao kupata ujauzito, yataendelea kuwepo na idadi ya wanaopata ujauzito itaongezeka.

Naomba wagombea watakaopitishwa na vyama vyao kugombea, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani waliingize kwenye ajenda suala hili ili kuokoa watoto hawa wa kike wasikatishe masomo.

Watwambie wakati wa kampeni watafanya nini kupunguza au kulimaliza tatizo hili linalozikabili skuli nyingi za kata.
Ingawa kwa upande wake serikali kuu, imechukua juhudi za makusudi kuhakikisha wanafunzi wanaokatisha masomo kwa ujauzito wanarejea skuli baada ya kujifungua, utekelezaji wa sera hii mihimu kuwekewa msisitizo ili kuhakikishwa wanafunzi wa kike wanapata fursa sawa ya elimu na wanaume.

Tunaamini kwa pamoja tunaweza kuliweka tatizo la mimba kwa wanafunzi kuwa ajenda muhimu kwa jamii yetu.

No comments:

Post a Comment