Friday, April 9, 2010

Magonjwa sugu ya macho sasa yatibiwa Z’bar

Na Juma Khamis
MAGONJWA sugu ya macho Zanzibar kama presha ya macho (glaucoma) na mtoto wa jicho sasa yanatibiwa nchini kwa kutumia teknolojia ya kisasa, inayotumiwa katika nchi kadhaa zilizoendelea ikiwemo Marekani na Ulaya.

Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili, daktari bingwa wa upasuaji wa macho kutoka China anaefanya kazi hospitali kuu ya Mnazimmoja, Dkt. Ji Jiangdong, alisema Zanzibar ni moja kati ya nchi zinazotumia huduma bora na ya kisasa zaidi katika kutibu maradhi ya macho.

Alisema wagonjwa wa macho sasa wana fursa sawa na zile wanazopata wagonjwa wenzao kutoka Marekani na mataifa ya Ulaya na katika baadhi ya miji nchini China.

“Hakuna upasuaji tunaofanya, badala yake tunatumia mashine maalum ambayo inanyonya mtoto wa jicho kwa kasi kubwa,” alisema Dkt Jiangdong.

Alisema mashine inayotumiwa ni aina ya Phacoemulsification ambayo ni ya kisasa na inapatikana katika hospitali kubwa duniani hasa nchi zilizoendelea na matibabu hufanywa kwa msaada wa Ultra Sound.

Aidha alisema mgonjwa anaefanyiwa matibabu sasa hapaswi kudungwa tena sindano, badala yake hutumia dawa maalum ya usingizi.

Alisema Zanzibar inapaswa kujivunia uhusiano wake na China kwani vifaa vilivyoletwa na serikali ya China havipo katika baadhi hospitali kubwa za mijini nchini humo.

“Hii ni huduma ghali sana duniani lakini kwa sababu Zanzibar na China ni marafiki wa karibu sana, tumeleta huduma hii ili watu wa Zanzibar nao wafaidike,” alisema.

Aidha alisema operesheni za macho kwa watoto wadogo, ambazo kabla zilikuwa zikifanyika katika hospitali ya CBRT kwa gharama za serikali ya Zanzibar sasa zinafanywa katika hospitali ya Mnazi mmoja.

Dkt. Jiangdong alisema asilimia 6.7 ya watu weusi wako kwenye hatari ya kuugua presha ya macho ikilinganishwa na watu weupe ambao ni asilimia 1-2.

Alisema mara nyingi huwapata watu walio na umri wa miaka 30-40 na 35-50.

Mapema Daktari dhamana wa kitengo cha macho katika hospitali hiyo, Dkt. Slim Mohammed, alisema gharama za matibabu kama hayo ambazo katika hospitali za Tanzania Bara zinafanywa kwa zaidi ya shilingi 400,000, kwa Zanzibar mgonjwa hutakiwa kuchangia shilingi 15,000 tu.

Aidha alisema kile kilio cha wananchi kudai kuwa viongozi wamekuwa wakifuata matibabu nje ya nchi sasa kimekwisha kwa kuwa viongozi wa juu wamekuwa wakipatiwa matibabu katika kliniki hiyo.

“Hakuna sababu kwa viongozi kufuata huduma ya macho nje ya nchi kwa sababu kile wanachokifata sasa kinapatikana Zanzibar,” alisema.

Gazeti hili lilimshuhudia Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Mawasiliano na Uchukuzi, Machano Othman Said akipatiwa huduma ya macho katika kliniki hiyo.

Akizungumzia suala la wataalamu wazalendo watakaotoa huduma hiyo baada ya jopo la madaktari wa China kuondoka, Dkt. Mohammed alisema serikali tayari inasomesha wataalamu wake nchini China.

“Wataalamu wanzalendo tayari wako China na hivi karibuni tunatarajiwa watarejea kuanza kutoa huduma ya macho,” alisema.

Hata hivyo, alisema serikali ina mkataba na China kwa karibu miaka 10 wa kuwapatia madaktari bingwa wa fani tofauti.

Alisema matibabu ya presha ya macho mara nyingi hufanywa kwa kutumia dawa, upasuaji na hatua zinachukuliwa kutibu maradhi hayo kwa kutumia leser ambayo kwa sasa inatumiwa Afrika Kusini pekee.

Dkt. Mohammed alisema presha ya macho ni ugonjwa wa pili baada ya mtoto wa jicho unao
sababisha upofu Zanzibar.

Hivyo, aliwataka wananchi kuwahi hospitali haraka mara wanapoona dalili za kuumwa na kichwa au kutoona vizuri.

Tayari zaidi ya wagonjwa 600 wameshapatiwa matibabu ya macho tokea kuja kwa madaktari bingwa kutoka China, Unguja na Pemba na lengo ni kuwahudumia wagonjwa 1,400 kwa mwaka.

China ndio mfadhili mkuu wa kiliniki ya macho Zanzibar, ambapo imechangia vifaa vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya dola 800,000 pamoja na jopo la madaktari bingwa.

No comments:

Post a Comment