Wednesday, January 19, 2011

Tuungane na Maalim, Balozi Seif wauza 'unga' watafute kazi nyengine wafanye

Na Juma Khamis
NAAMINI pamoja na ugumu wa vita dhidi ya dawa za kulevya unaoelezwa, iwapo tutashikamana kwa dhati Zanzibar tutashinda na kuwaokoa vijana wetu na janga la dawa za kulevya ambalo limeanza kuleta madhara makubwa na kuonesha hatma mbaya Zanzibar.

Viongozi wa Zanzibar waliopita hasa awamu ya sita walijaribu sana kupambana na biashara pamoja na matumizi ya dawa za kulevya, lakini kutokana na vikwazo vuigumu vilivyokuwa vimejitokeza, ikiwemo kukosekana mshikamano miongoni mwa wanajamii na rushwa mafanikio yalikuwa hafifu.

Lakini kwa serikali hii ya awamu ya saba kutokana na misingi iliyojengewa ya umoja mshikamano na maelewano naweza kusema kwamba wafanyabiashara wa dawa za kulevya iwapo tutaamua kwa dhati basi wakatafute kazi nyengine za kufanya mapema, kabla ya kufichuliwa na kukashifika mbele ya jamii.

Turufu kubwa ya ushindi katika vita hivi itakuwa ni uzalendo miongoni mwa wananchi baada ya kuona viongozi wa juu ni mfano mzuri kwao katika kudumisha mshikamano ambao ulikosekana kwa kiasi kikubwa huko nyuma, na zaidi baada ya kuja kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

Hivi sasa viongozi wetu wote wajuu namaanisha Rais Dk. Shein, Makamo wa kwanza Maalim Seif na Makamo wa pili wa Rais Balozi Idd imedhihirika kwamba wanafanya kazi kwa pamoja na mashirikiano makubwa hali inayomaanisha mwanzo mwema kuelekea kwenye mafanikio.

Kama ingekuwa mpira wa miguu basi tungesema ushindi upo wazi kwasababu viungo wa timu ni wazuri na wanaona sana, na kilichobakia ni mabeki pamoja na wafungaji kuwa imara kwa vile mchezo tumeshaudhibiti pale kati kati, basi kwanini Idara zilizobakia zizembee.

Umoja kati ya viongozi hao haunashaka kutokana na kauli, lakini na matendo tunayoyaona tokea siku za mwanzo za serikali hii ya awamu ya saba, hali inayomaanisha kumbe tukiamua hakuna cha kutushinda.

Rais Dk. Shein tayari alithibitisha umoja na maelewano ya hali ya juu kati yake na wasaidizi wake hao, pale alipokuwa akihutubia kwenye kilele cha maadhimisho ya mika 47 ya Mapinduzi ya Zanzibar wiki uwanja wa Amaan mbele ya umati mkubwa wa wananchi, viongozi na wawakilishi wa mataifa ya kigeni.

Lakini pia Maalim Seif naye alithibitisha mashirikiano makubwa na ya aina yake kati yake Rais Dk. Shein na Balozi Seif Idd katika hafla nyingi ikiwemo mkutano wa kwanza wa hadhara wa CUF tangu walipojumuika katika serikali ya umoja wa kitaifa huko katika viwanja vya Kibandamaiti.

Tukumbuke kwamba viongozi hao wote watatu wanachukia sana rushwa, uzembe na tamaa mbaya ya kujilimbikizia mali, na wameweka uzalendo wao kwa Zanzibar, hivyo matumaini yetu ni vigumu kwa 'vidudu mtu' kujipenyeza katika ngome hiyo.

Nimewataja Maalim Seif kwasababu afisi yake ndiyo iliyokabidhiwa rungu kupambana na dawa za kulevya, na Balozi Seif Idd ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za serikali, wakifanya kazi chini ya Dk. Shein na kwa ufupi ngoma imepata wachezaji.

Kwa vile tumeshadhibiti nafasi za viungo, tuwatake walinzi waetu wa timu hii ambao tunaweza kusema ni polisi, mahakama na taasisi nyengine za ulinzi, usalama na kusimamia haki nao wawe tayari kwa ushindi.

Katika kuktadha huu safu ya wapachika mabao itakuwa ni wanajamii wenyewe, ambao bila shaka wanaishi pamoja na kuwatumikia wauzaji hao wa dawa za kulevya. Vijana wetu wanaathirika sana na dawa hizi za kulevya na watumiaji wanasambaa kwa kasi, leo usijekushangaa ukisikia hata kule nyumbani kwetu kisiwani Tumbatu kuna 'mateja' wa dawa za kulevya..

Tukumbuke kwamba tamaa kwa baadhi ya watendaji wakiwemo baadhi ya Polisi na watendaji wa vyombo vya kutoa haki kama tulivyovitaja hapo juu ni maeneo ambayo yalilega lega sana na maadui kupenya kwa miaka mingi tangu kuja kwa biashara huria nchini kwetu.

Tukio la miaka kadhaa nyuma ambapo tulielezwa kuwa pipi zilizokuwa na dawa za kulevya baadaye ilibainika ulikuwa ni unga wa sembe ni mfano mmoja wapo wa udhaifu katika vyombo vyetu hivi vyenye umuhimu wa kipekee kutokomeza maovu haya.

Wengi tulijiuliza inaama inawezekana mtu kuweka pipi yenye unga wa sembe tumboni kutoka Pakistani hadi ije itolewe Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, basi unga wa sembe huo wa Pakistani ni mzuri sana.

Katika mkutano mmoja kati ya wazazi wa Shehia kadhaa za Mji Mkongwe na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za Baraza la Habari (MCT), wakati huo zikiwa mtaa wa Shangani mjini Zanzibar, hofu kuu ya wazazi katika kuwafichua wahusika wakuu wa dawa za kulevya ilikuwa hofu ya kupelekwa majina yao kwa maharamia hao wa mihadarati.

Hofu hii hakiuwa kwa wazazi wa vijana walioathirika na matumizi ya dawa hizo pekee, lakini baadhi ya Msheha katika mji wa Unguja katika mkutano mmoja wa kujadili tatizo la dawa za kulevya mmoja wao alisema 'leo ukimtaja muuzaji wa dawa za kulevya, basi kesho atakufuata nyumbani na kukuonya kwa vitisho vikubwa kwamba utakiona cha moto'.

Kauli za Masheha na wazazi wa Mji Mkongwe kwa kifupi zilimaanisha kwamba miongoni mwa askari Polisi walikuwepo au wapo wanaonufaika na biashara hiyo na wanatumiwa na vigogo hao wa dawa za kulevya.

Kama tulivyogusia katika safu hii wiki iliyopita rushwa, muhali uliopita kiwango na kulindana ndiyo sumu kwa ustawi wa Zanzibar, kwa vile serikali hii imeonesha nia na kwa vitendo kuondoa hali hiyo kwanini wanajamii wote wasitoe wasishirikiane kutauta matatizo yaliyopo.

Tukijipanga kama hivyo na jamii yote kuonesha kuchoshwa na janga hili linalotishia mustakabali wa Zanzibar, dawa za kulevya zitapita wapi kuwafikia vijana. Hivi sasa wenzetu Kenya katika mji wa Mombasa wamefanikiwa sana kufanya 'unga' ni bidhaa adimu katika eneo hilo na vijana wengi walioathirika kwa muda mrefu sasa wanatibiwa katika vituo na wamekuwa na matumaini mapya.

Sote tunaathiriwa na hali ya kukithiri dawa za kulevya Zanzibar, kwa njia moja ama nyengine kama si mwanao, kaka, rafiki, au jirani yako aliyejiingiza kwenye janga hilo, basi utakuwa umeibiwa nyumbani, umekwapuliwa barabarani, au kama hayo yote hayajakukuta basi utakuwa unaishi kwa hofu usijevamiwa na vijana hao iwe njiani au barabarani siku moja.

No comments:

Post a Comment