Monday, June 21, 2010

Pindi tukizishinda changamoto hizi hakuna mtu atakaebakia pembezoni

Na Juma Khamis

KILA ifikapo May 9 ya kila mwaka, Umoja wa Ulaya (EU) huadhimisha siku yake kukumbuka siku ambayo Robert Schuman aliwasilisha pendekezo la kuundwa Muungano wa Ulaya mwaka 1950.

Pendekezo hilo lililopewa jina la "Azimio la Schuman", linachukuliwa kama mzizi uliosababisha kuuundwa kwa Umoja wa Ulaya.

Siku hii huadhimishwa kwa shughuli mbali mbali pamoja na matamasha yanayowakutanisha pamoja raia kutoka Muungano huo.

Siku hiyo pia huadhimishwa katika mataifa mbali mbali duniani, ambayo EU ina ushawishi wake ikiwemo Zanzibar.

Kwa mwaka 2010 Zanzibar ilikuwa mwenyeji, ambapo shughuli mbali mbali za maendeleo ya wananchi ambazo zinaungwa mkono na EU zilipewa kipaumbe cha kwanza.

Kwa mfano Balozi wa EU nchini Tanzania Tim Clarke, alipata fursa ya kukagua miradi ya kilimo katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar, pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wakulima na wananchi kwa ujumla.

Clarke pia alipata fursa ya kusikiliza vilio kutoka kwa wananchi moja kwa moja au kupitia taasisi zinazowakilisha watu wanaoishi pembezoni, ambao idadi yao ni kubwa zaidi.

Licha ya jitihada kubwa zinazochukuliwa na EU, kuanzisha miradi mbali kwa lengo la kuwakomboa watu waliosahaulika, bado tatizo limebakia pale pale; matajiri wanaendelea kunawiri kwa utajiri na maskini wanaendelea kudidimia katika dimbwi la umaskini.

Tatizo ni kwamba miradi mingi inapoanzishwa na kuwa chini ya ufadhili, inawawia vigumu wananchi kuiendeleza baada ya mfadhili kuondoka.

Tatizo hili limejitokeza katika miradi kadhaa, ambayo sasa imekufa kabisa huku faida yake kwa wananchi ambao ndio walengwa ikiwa haionekani.

Tatizo jengine ni wananchi kutoshirikishwa kwa ukamilifu katika miradi husika huku wakipewa asilimia ndogo sana ya uendeshaji wa miradi.

Wao hawana nguvu ya kutumia fedha za miradi badala yake kutakiwa kuomba miradi kwa watu ambao walitakiwa tu kuwa wasimamizi na sio waendeshaji.

Changamoto zinazowakabili watu walioko pembezoni ni nyingi na zinaonekana katika mataifa mbali mbali duniani, lakini athari zaidi inajotokeza katika nchi maskini Zanzibar ikiwa miongoni mwao.

Makundi yaliyo pembezoni bado hayajaonekana ipasavyo na hayafikiwi na rasilimali muhimu za taifa (national cake) au zinawafikia kwa asilimia ndogo ambazo hazikidhi mahitaji yao wala hazitoshelezi kutoka na wingi wao.

Kwa mfano, vijana ambao ndio watu muhimu katika jamii bado wanakabiliwa matatizo makubwa ikiwemo upungufu wa ajira, ambapo zaidi ya asilimia 70 ya vijana hawana ajira za uhakika za kujipatia kipato.

Hali hii huwafanya wengi wao kujitumbukiza katika makundi maovu ya kutumia dawa za kulevya, wizi wa kutumia nguvu na ubakaji.

Ni kweli wizi haukubaliki katika jamii lakini kama kijana huyu angeandaliwa mazingira bora, bila shaka asingekuwa na muda wa kufanya uhalifu.

Lakini pia lazima ifike muda tukubali kuwa mfumo wetu wa elimu, haumsaidii kijana kujitegemea baada ya kumaliza shule.

Wapo wengi ambao wamemaliza elimu ya juu (shahada), lakini hawana kazi za kufanya na badala yake wanaendelea kuwa tegemezi kwa wengine.

Unyanyasaji mkubwa pia unaonekana kushamiri kwa wafanyakazi wa nyumbani, ambao daima wamekuwa wakilalamika lakini maskini sauti zao hazisikilikani na kama vile wameshindwa na mtu wa kuwatetea.

Hawa ni waathirika wa kulipwa mishahara midogo tena isiyo zingatia wakati, kiwango kidogo cha elimu, pamoja na udhalilishaji wa kimapenzi unaofanywa na waajiri.

Baba mwenye nyumba haoni tabu kumuomba penzi mfanyakazi wake wa ndani na kutishia kumfukuza pale anapokataa ‘kumuhudumia’.

Tatizo hili linaweza kuondoka tu kwa kuandaa mikataba kwa wafanyakazi wa ndani, kwa sababu kama zilivyo sekta nyegine sekta hii nayo ni muhimu.

Kundi jengine lililosahaulika ni la watu wenye ulemavu; kundi hili bado halifaidiki na mfumo wa elimu ulipo sasa, unyanyasaji unaofanywa na madereva, lakini pia mfumo wa miundombinu unaonekana haukuwazingatia watu wenye ulemavu.

Kwa mfano barabara hazijatengwa kwa watu wenye ulemavu, hali ambayo huwafanya kugongwa na madereva wazembe.

Changamoto nyengine zinazowakabili watu waliosahaulika ni kukithiri kwa matukio ya ubakaji kwa watoto wadogo, utelekezaji wa familia, upungufu wa miradi kwa wajasiriamali na ukosefu wa sheria zinazozingatia wakati na mazingira halisi yaliyopo sasa.

Kama kweli tutazimaliza changamoto hizi ni dhahiri hakuna mtu atakaebakia pambezoni.

1 comment:

  1. Citizen Titanium's Dive Watch | iTanium Arts
    The latest grade 23 titanium release of titanium camping cookware Citizen Titanium, the most advanced diving titanium frames device, designed and titanium piercings developed by independent craftsmen. Read more mens titanium watches and claim

    ReplyDelete