Sunday, July 4, 2010

Kila Mzanzibari aliyetimiza umri wa miaka kumi na nane anaweza kuandikishwa kuwa mpiga kura

Wataalamu wengi wa masuala ya siasa na sheria wanapendekeza taratibu mbali mbali za kuendesha uchaguzi wa viongozi.

Moja kati ya taratibu hizo ni kuwashirikisha wananchi wote katika kuchagua aina ya viongozi wanaowataka.

Katika kuwashirikisha huko wananchi lazima wawe huru kuchagua kiongozi wanaemtaka.

Kwa upande wa Zanzibar uchaguzi unaendeshwa kupitia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Sheria ya Uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984, Kanuni mbali mbali zilizotungwa na Tume ya Uchaguzi pamoja na maelekezo mbali mbali ambayo hutolewa na Tume.

Katiba ndiyo iliyounda Tume ya Uchaguzi ambayo imepewa mamlaka ya kuendesha na kusimamia mchakato wote wa uchaguzi huku sheria ya Uchaguzi kwa upande wake ikiweka misingi na taratibu nyengine za uchaguzi wa Zanzibar.

Kanuni nazo zimefafanua baadhi ya mambo ambayo hayakuelezwa wazi katika sheria.

Pamoja na hayo Tume kupitia sheria ya uchaguzi inao uwezo wa kutoa maelekezo na ufafanuzi wa jambo lolote ambalo linahitaji kutolewa ufafanunuzi linalohusiana na uchaguzi.

Neno uchaguzi kwa mujibu wa sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya mwaka 1984 limetafsiriwa katika hatua tatu tofauti.

Hatua ya kwanza ni uchaguzi wa Rais ambapo maana yake ni uchaguzi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Hatua ya pili ni uchaguzi wa Baraza la Wawakilishi ambapo maana yake ni uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na inajumuisha uchaguzi mdogo.

Hatua ya tatu ni uchaguzi wa serikali za Mitaa ambapo maana yake ni uchaguzi wa viongozi wa serikali za Mitaa ambao ni Madiwani na inajumuisha uchaguzi mdogo.

Tunaposema sheria ya uchaguzi inakusudiwa sheria Na. 11 ya mwaka 1984, sheria ambayo imeweka misingi na taratibu mbali mbali za uchaguzi kwa upande wa Zanzibar. Katika seria hii uchaguzi umegawika katika hatua kuu saba.

Kuandikisha wapiga kura, kufanya uteuzi wa wagombea, kufanya kampeni, kupiga kura, kuhesabu kura, kujumlisha kura na kutangaza matokeo.

Sheria hii ya uchaguzi imeweka utaratibu wa kila hatua tuliyoitaja hapo juu, hatua hizo zinawahusisha wananchi, vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi , kwa kuanzia hebu tujikumbushe hatua hizo walau kwa ufupi.

Kuandikisha wapiga kura

Katika zoezi hili, sheria imeweka wazi sifa za mtu kuweza kuandikishwa kuwa mpiga kura.

Kwa mfano kifungu cha 11 kinaeleza kuwa kila Mzanzibari aliyetimiza umri wa miaka kumi na nane (18) anaweza kuandikishwa kuwa mpiga kura kwa mujibu wa masharti ya sheria isipokuwa awe amezuiliwa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi au sheria nyengine yoyote ile.

Hivyo, chini ya masharti ya sheria ya uchaguzi, ili mtu aweze kuandikishwa kama mpiga kura ni lazima awe na sifa zifuatazo.

Awe Mzanzibari; na awe na umri wa kuanzia miaka kumi na nane; na awe hajazuiliwa kuandikishwa na sheria.

Hizi ndizo sifa mama kwa mtu kuweza kuandikishwa kuwa mpiga kura kwa uchaguzi wa viongozi chini ya sheria ya uchaguzi.

Kufanya uteuzi wa wagombea

Kama tunavyojua kuwa uchaguzi unahusisha wagombea kutoka vyama tofauti vilivyopata usajili wa kudumu Tanzania.

Hivyo kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi jukumu la kufanya uteuzi wa wagombea ili waweze kushiriki katika uchaguzi lipo mikononi mwa Tume ya Uchaguzi.

Uteuzi wa wagombea nao umegawanyika katika hatua tatu tofauti kutegemea aina ya uchaguzi.

Uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Urais; uteuzi wa wagomvea wa nafasi ya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi; na uteuzi wa wagombea wa nafasi ya udiwani.

Uteuzi wa wagombea wa urais

Kifungu cha 31 kimeweka masharti ya uteuzi kwa wagombea wa kiti cha urais; masharti hayo ni kama yafuatayo.

Mgombea lazima awe anatoka kwenye chama cha siasa kilichosajiliwa.

Mgombea lazima awe amedhaminiwa na watu wasiopungua mia mbili waliondikishwa kuwa wapiga kura, kutoka katika kila mkoa katika mikoa mitano ya Zanzibar.

Taarifa za wagombea lazima ziwasilishwe kwa Tume katika fomu maalum itakayotolewa na Tume kwa kuwasilishwa katika afisi ya Tume ndani ya kipindi kilichowekwa na Tume; na

Mgombea kulipa fedha kama dhamana kiasi kama kitakachowekwa na Tume.

Mara baada ya hatua hizo kukamilika, Tume itafanya uteuzi kwa kuangalia sifa za mgombea kama zilivyoelezwa katika fomu iliyowasilishwa na baada ya kuridhika na sifa pamoja na masharti mengine, Tume itafanya uteuzi kwa kutangaza majina ya wagombea wa nafasi ya urais.

Uteuzi wa wagombea wa uwakilishi

Kwa upande wa nafasi ya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, sheria ya uchaguzi imeeleza utaratibu wa uteuzi katika kifungu cha 46, chini ya kifungu hichi yapo masharti makuu manne nayo ni:-

Mgombea lazima awe anatoka katika chama kilichosajiliwa;

Mgombea lazima awe amedhaminiwa na wapiga kura wa chama chake wasiopungua ishirini na tano ambao wameandikishwa kuwa wapiga kura katika eneo la uchaguzi lililomo ndani ya jimbo analotaka kugombea;

Taarifa za mgombea zitolewe katika fomu maalum iliyotolewa na Tume na kuwasilishwa kwa Tume ndani ya muda uliowekwa na Tume; na

Mgombea kulipa dhamana ya kima cha fedha kama kitakachowekwa na Tume.

No comments:

Post a Comment