Wednesday, July 21, 2010

Wagombea, mawakala wanayo haki ya kuhoji na kuangalia hatua za kujumlisha kura

Kuhesabu kura ni hatua inayofuata mara baada ya zoezi la kupiga kura kumalizika. Sheria ya uchaguzi imeweka utaratibu wa kuhesabu kura katika vituo vya kupigia kura.

Kwa kifupi, wasimamizi wa vituo vya kupigia kura ndio watakaohusika na kuhesabu kura vituoni.

Wakati wa kuhesabu vituo vya kupigia kura na maofisa wa kupiga kura, vitaitwa vituo vya kuhesabu kura na maofisa nao watakuwa maofisa wa kuhesabu kura.

Watu walioruhusiwa kuwemo katika vituo vya kupigia kura ndio watakaoruhusiwa kuwemo katika vituo vya kuhesabu kura.

Kifungu cha 80 cha sheria ya uchaguzi kimeweka utaratibu mzuri wa namna ya kuhesabu kura.

Lakini kabla ya kuhesabu kura msimamizi wa wa kituo atatakiwa kutoa taarifa zifuatazo kwa watu wanaoshikiri katika zoezi hilo.
Hesabu ya kura zilizopelekwa katika kituo cha kupigia kura
Hesabu za watu waliopiga kura
Hesabu ya kura zilizobakia ambazo hazikupigwa
Hesabu ya karatasi za kura
Idadi ya wapiga kura waliopiga kura, na
Hesabu za kura zote zilizotumika.

Na baada ya hapo, atakagua kifungio na kuhakikisha kuwa hakikufunguliwa au kufanyiwa udanganyifu, kufungua kifungio na kufungua sanduku tayari kwa kauanza kuhesabu kura.

Hatua hizi ni lazima zifuatwe ili kutekeleza yale matakwa ya kanuni na kisheria inayosema kwamba ‘sio tu kwamba haki itendeke bali ionekane bayana ikitendeka’.

Sheria inaelezea uwazi zaidi wa kuhesabu kura, kwa kumtaka msimamizi wa kuhesabu kura kukunjua karatasi ya kura na kutamka kwa sauti kilichoonekana katika karatasi hiyo, na hayo lazima yashuhudiwe na watu waliopo katika kituo cha kuhesabu kura.

Hata hivyo, ili kujua ipi halali na ipi batili, jukumu hilo limewekwa kwa Tume kwa kutunga kanuni kueleza ni ipi kura halali na ipi sio halali.

Hata hivyo, utaratibu unaotumika sasa ni kukubaliana kwa waliopo katika chumba cha kuhesabu kura, ipi kura halali na ipi kura batili.

Kujumlisha kura

Hii ni hatua inayofuata baada ya kuhesabu kura kutoka vituoni.

Ni hatua ambayo matokeo yote ya vituo vya kupigia kura hujumlishwa katika jimbo la uchaguzi ili kupata matokeo ya jumla kwa jimbo zima na hatimae kumpata mshindi.

Kifungu cha 83A kimewataja watu wanaoruhusiwa kuwepo wakati wa zoezi la kujumlisha matokeo ni.

(a) Msimamizi wa uchaguzi
(b) Msaidizi Msimamizi wa uchaguzi
(c) Mjumbe wa Tume
(d) Mkurugenzi wa Uchaguzi au Afisa wa uchaguzi wa Tume
(e) Mgombea
(f) Wakala wa kuhesabu kura
(g) Polisi au mtu mwenye jukumu la kuweka usalama katika kituo cha kuhesabu kura
(h) Waangalizi walioruhusiwa na Tume.

Wakati wa zoezi la kujumlisha matokeo, wagombea au wakala wao wanayo haki ya kuhoji na kuangalia hatua zote za kujumlisha kura na iwapo watakuwa na mashaka wanaweza kuomba kwa msimamizi wa uchaguzi ili kujiridhisha na ujumlishaji huo.

Aidha kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, matokeo ya kura ya Urais yatajumlishwa na tofauti na yale ya Wawakilishi na Udiwani.

Kutangaza matokeo

Kutangaza matokeo ya uchaguzi ni hatua ya mwisho katika uchaguzi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.

Mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi kwa ngazi zote yapo kwa Tume.

Kwa mujibu wa kifungu cha 88, inaelezwa kuwa, mara baada ya zoezi la kuhesabu na kujumlisha kura kukamilika na matokeo kuthibitishwa, Msimamizi wa uchaguzi atamtangaza mgombea aliyepata wingi wa kura halali.

Taarifa za matokeo pia zitapelekwa kwa maandishi kwa mshindi na baadae kutangazwa katika Gazeti rasmi la serikali.
Aidha kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi matokeo ya uchaguzi kwa uwakilishi na udiwani yatatangazwa na Wasimamizi wa uchaguzi wa Majimbo vituoni, na kwa ngazi ya Urais yatatangazwana Tume makao makuu.

Kwa maana hiyo, matokeo halali kwa mujibu wa sheria ni yale yatakayotangazwa na Tume na sio vyenginevyo.

Hizi ndizo taratibu za uchaguzi wa viongozi wa Zanzibar chini ya Sheria ya Uchaguzi Nam 11 ya mwaka 1984.

No comments:

Post a Comment