Thursday, July 15, 2010

Kampeni ya nyumba kwa nyumba ni kosa kwa mujibu wa sheria

Uteuzi wa wagombea wa udiwani

Ama kwa upande wa wagombea wa udiwani, masharti ya uteuzi yameelezwa katika kifungu cha 59 na 60, masharti yenyewe ni kama yafuatayo:

(a) Mgombea lazima awe amedhaminiwa na chama cha siasa kilichosajiliwa.

(b) Mgombea lazima awe amedhaminiwa kwa maandishi na wapiga kura wasiopungua kumi na tano (15) walioandikishwa kuwa wapiga kura katika eneo la uchaguzi analogombea.

(c) Mgombea alipe dhamana ya kima cha fedha kama kitakachowekwa na Tume.

Kama ilivyo kwa uteuzi wa wagombea wa urais, kwa upande wa uwakilishi na udiwani, baada ya hatua za chama au mgombea kuwasilisha fomu zao za kugombea kwa Tume, Tume itafanya uhakiki wa sifa na masharti mengine kama yalivyoelezwa na Katiba na Sheria ya uchaguzi, na baadae itafanya uteuzi wa wagombea waliotimiza sifa na vigenzo vilivyowekwa na katiba pamoja na sheria.

Kufanya kampeni
Kampeni ni hatua inayofuata baada ya uteuzi wa wagombea. Kwa kawaida kampeni hufanywa na chama au mgombea wa chama.

Hivyo sheria ya uchaguzi imeweka masharti ya kufuatwa na vyama au wagombea wakati wa kufanya kampeni kwa ajili ya uchaguzi.

Kifungu cha 56 kinaelezea kuwa kila chama kitawasilisha kwa Tume ya Uchaguzi ratiba ya mikutano ya kampeni inayoonesha wakati na pahali mikutano hiyo itakapofanyika na nakala ya ratiba hiyo kupelekwa kwa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuandaa usalama wakati wa kampeni.

Tume inatakiwa kuhakikisha kuwa ratiba ya kampeni ya chama kimoja haigongani na ratiba ya chama chengine ili kuondoa hali ya kuwepo kwa kampeni mbili katika sehemu moja.

Sharti jengine lililowekwa katika kifungu hichi ni kwamba chama au mgombea kutofanya kampeni katika maeneo ya ibada au taasisi za taaluma.

Hata hivyo, maeneo ya taalamu au taasisi za ibada zimeelezwa kuwa ni maeneo yote yanayotumiwa na waumini kufanyia ibada ikiwemo misikiti, makanisa au madrasa au sehemu nyingine yoyote inayotumiwa na waumini kwa ajili ya ibada.

Aidha taasisi za taaluma ni sehemu yoyote inayotumika kwa ajili ya kutoa taaluma ikiwa ni pamoja na shule, vyuo na maeneo kwa hayo.

Pia sheria imepiga marufuku kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba.

Kampeni za nyumba kwa nyumba ni kwa chama au mgombea kupita majumbani na kutangaza au kushawishi watu wapige kura chama au mgombea fulani.

Kupiga kura

Baada ya hatua ya kampeni kumalizika, hatua inayofuata ni kupiga kura. Sheria ya uchaguzi inasema kuwa Tume itatangaza siku ya kupiga kura na namna ya kupiga kura.

Zoezi la kupiga kura litafanyika katika vituo vya kupigia kura ambapo wapiga kura watatakiwa kufuata maelekezo yatakayotolewa na Tume juu ya utaratibu na namna ya kupiga kura, ikiwemo jinsi ya kujipanga kwa utaratibu maalum kama utakavyowekwa na kutangaza na Tume.

Hata hivyo, kupiga kura itakuwa kwa wale walioandikishwa na kupewa shahada za kupigia kura.

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi kila mtu atatakiwa apiga kura katika sehemu aliyoandilishwa kama mpiga kura katika eneo hilo, kinyume na hivyo mtu hatokuwa na haki ya kupiga kura.

Kuwepo utaratibu wa kuwawezesha wapiga kura wapige kura zao kwa njia ya siri na kwa upande wa wale watu wasioona, walemavu wa viungo au kushindwa kusoma, Tume ya uchaguzi inatakiwa kuanda utaratibu wa kuwawezesha watu wote hao wapige kura kwa namna iliyo huru, ikiwemo kuwaruhusu watu wao karibu kuweza kuwasaidia kupiga kura zao.

Vile vile sheria inaelekeza kuwa katika vituo vya kupigia kura, kutaruhusiwa watu maalum kuingia au kuwepo katika vituo hivyo. Watu watakaoruhusiwa kuwemo katika kituo cha kupigia kura ni:

(i) Mkuu wa kituo cha kupigia kura;
(ii) Msaidizi wa kituo cha kupigia kura
(iii) Wakala wa upigaji kura
(iv) Mpiga kura
(v) Mtu anayemsaidia mpiga kura mwenyewe ulemavu
(vi) Mwangalizi wa uchaguzi aliyepewa utambulisho na Tume
(vii) Mgombea
(viii) Mjumbe wa Tume
(ix) Mkurugenzi wa uchaguzi
(x) Afisa wa uchaguzi
(xi) Afisa wa polisi au mtu mwengine mwenye dhamana ya usalama katika kituo cha kupigia kura; na
(xii) Msimamizi wa uchaguzi na Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi.

Hivyo kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi hawa ndio watu wanaoruhusiwa kuingia katika kituo cha kupigia kura.

Aidha mara baada ya zoezi la kupiga kura kumalizika, sheria inaelekeza utaratibu wa kuhidafhi masanduku ya kura baada ya kukubaliana na wahusika wote na kuyafunga namna ambavyo hayataweza kufunguliwa na hakuna chochote kinachoweza kuingizwa katika masanduku hayo.

Kuhesabu kura

Kuhesabu kura ni hatua inayofuata mara baada ya zoezi la kupiga kura kumalizika. Sheria ya uchaguzi imeweka utaratibu wa kuhesabu kura katika vituo vya kupigia kura.

Kwa kifupi, wasimamizi wa vituo vya kupigia kura ndio watakaohusika na kuhesabu kura vituoni.

Wakati wa kuhesabu vituo vya kupigia kura na maofisa wa kupiga kura, vitaitwa vituo vya kuhesabu kura na maofisa nao watakuwa maofisa wa kuhesabu kura.

No comments:

Post a Comment