Sunday, July 4, 2010

Dk. Shein: Msiwachague viongozi wachoyo, wabinafsi, wasiopenda umoja

WATANZANIA wametakiwa kuwa macho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu na kuacha kuwachagua viongozi, wabinafsi, wachoyo na wanaopinga umoja nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ali Mohammed Shein, alipozindua mbio za mwenge wa Uhuru mwaka huu kitaifa, uwanja wa Kwaraa, Mjini Babati Mkoani Manyara.

“ Msiwachague viongozi wachoyo, wenye ubinafsi kwa kuweka maslahi yao mbele, na hasa wale wenye kuwagawa wananchi na kudhoofisha umoja wa Taifa”Alisema Dk. Shein.

Aidha ametoa wito kwa vyama vya siasa na taasisi za kiraia, kushajiisha wananchi kujitokeza katika kupiga kura kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini kote Oktoba mwaka huu.

“Uchaguzi huu utatoa fursa kwa wananchi kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuleta maendeleo nchini na kudumisha umoja, amani na utulivu bila kuzingatia ukabila, rangi, dini, mitazamo yao kisiasa au jinsia zao” alifafanua Makamu wa Rais.

Akizungumzia rushwa katika uchaguzi mkuu, Dk. Shein alieleza kuwa lengo la kupambana na vitendo hivyo la Serikali ya awamu ya nne, linaendelea, ambapo amezitaka taasisi zote zinazohusika kwa njia moja au nyengine kwenye uchaguzi huo kuwajibika ipasavyo.

Pia Dk. Shein aliwasisitiza wananchi kuongeza nguvu ya kupambana na maradhi ya malaria, Ukimwi na dawa za kulevya, pamoja na kuacha na kulaani mauaji ya albino na kuwataja wahusika wa vitendo hivyo.

Aidha Dk. Shein, alieleza mkakati wa Serikali kuwapa kipaumbele watu walio katika makundi maalum, wakiwemo wenye ulemavu, wanawake, vijana na watoto kwa kuwawezesha, ili waweze kukabiliana na matatizo yanayowakabili.

Kwa mujibu wa waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, Prof. Juma Kapuya, mwenge wa uhuru mwaka huu utamaliza mbio zake Oktoba 14, Mkoani Kigoma.

Ujumbe wa Uhuru mwaka huu ni mapambano dhidi ya malaria, dawa za kulevya, Ukimwi na uchaguzi mkuu wa amani 2010.

Hata hivyo alisema pia mwenge huo mwaka huu utaendelea kukumbusha vita dhidi ya mauaji ya albino, rushwa na mambo yenye kuhusiana na haki za wanawake.

Sherehe hizo na uzinduzi pia zimehudhuriwa na Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto Zanzibar, Asha Abdalla Juma, Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, Mkurugenzi wa ILO, wabunge na viongozi wengine wa vyama vya siasa na Serikali.
Mwenge huo mwaka huu utakimbizwa na vijana sita, wawili kutoka Zanzibar na wanne Tanzania Bara, ambapo kiongozi wao ni Nassor Ali Matuzya kutoka Mkoa wa Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment