Wednesday, July 28, 2010

Mgombea anaweza kutumia gharama zake mwenyewe wakati wa kampeni

Na Juma Khamis

KWA muda mrefu, Tanzania haikuwa na mfumo maalum wa kusimamia na kuratibu gharama za uchaguzi kwa gombea wa vyama vya siasa.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010, kumekuwepo na mawazo na pia kujengeka utamaduni kwamba uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha.

Tofauti za uwezo wa wagombea zimekuwa kubwa kiasi ambacho wananchi hawapati fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka badala yake wale wenye fedha tu ndio wanachaguliwa kwa sababu ya fedha zao.

Baada ya kuona hali hiyo, serikali ya Tanzania iliona iko haja ya kuimarisha demokrasia ya uchaguzi kwa kuhakikisha kwamba kunakuwepo mazingira yaliyo salama na sawa kwa wagombea wakati wa uchaguzi ili kuweza kupata viongozi wenye uwezo wa kuongoza na kuwatumikia wananchi kwa ushawishi wa sera ya vyama vyao na sio fedha.

Katika kutimiza dhamira hiyo, serikali iliamua kutunga sheria ya gharama za uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010 iliyopitishwa na Bunge Februari 11, 2010.

Hata hivyo, kwa kuwa sheria hii bado haijarasimishwa na Baraza la Wawakilishi kutumika katika mamlaka ya Zanzibar, haitakuwa na meno ya kuuma (haitafanya kazi) kwa nafasi za Urais wa Zanzibar, Uwakilishi na Udiwani, badala yake itatumika kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge (ingawa sheria ya uchaguzi kwa Wabunge wa Zanzibar inasimamiwa na sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar nambari 11 ya mwaka 1984).

Lengo la sheria hii ni kuutambua kisheria mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya vyama vya siasa kuanzia ngazi ya kura za maoni na kusimamisha wagombea.

Kuweka utaratibu wa kisheria utakaosimamia na kuratibu mapato na kudhibiti matumizi pamoja na gharama za uchaguzi kwa vyama vya siasa na wagombea.

Kuweka viwango kwa matumizi na gharama za uchaguzi; kuweka utaratibu utakaosimamia mapato na matumizi ya vyama vya siasa ikiwa ni pamoja na zawadi, misaada na michango itakayotolewa na wagombea au wahisani wakati wa kampeni za uchaguzi.

Kudhibiti michango na zawadi kutoka nje, kuweka utaraibu na mfumo wa uwajibikaji wa mapato na matumizi ya fedha za uchaguzi kwa upande wa vyama vya siasa na wagombea na kuainisha adhabu kwa watakaokiuka masharti yaliyowekwa na sheria yenyewe.


Nini gharama za uchaguzi?

Gharama za uchaguzi maana yake ni fedha zote ambazo zimetumika au gharama zote zilizotumika kwa ajili ya kuendesha au kusimamia kura za maoni, kampeni za uchaguzi na uchaguzi kwa chama cha siasa, mgombea na serikali. Hii imeelezwa kwa kina katika kifungu cha 7(1) cha sheria ya gharama za uchaguzi.

Kwa hivyo, gharama ni matumizi yote yatakayohusika wakati wa kura za maoni ambayo yatakuwa yamegharamiwa na chama cha siasa, matumizi au gharama zozote zitakazo husika na chama ili kuwezesha uteuzi wa mgombea wake, gharama zozote au matumizi yoyote yatakayohusika na chama cha siasa au mgombea wakati wa kampeni ikiwa ni pamoja na gharama zote zitakazotumika kwa ajili ya vikundi vya uhamasishaji kwa ajili ya kumnadi mgombea.

Pia gharama za chakula, vinywaji, malazi au usafiri ambazo mgombea amegharamia wakati wa kampeni na gharama zozote au matumizi yoyote yatakayohusika na serikali, chama cha siasa au mgombea wakati wa uchaguzi yatajumuisha gharama za uchaguzi.

Sheria imeweka bayana kwamba kila chama cha siasa kitagharamia kampeni za uchaguzi kwa kutumia gharama za uchaguzi zinazotokana na vyanzo vyake, kwa mujibu wa kifungu cha 8(1) cha sheria hii.

Hata hivyo, kifungu cha 8(2) kimezingatia kuwa mgombea anaweza kutumia gharama zake mwenyewe wakati wa kampeni pale inapobidi kulingana na mahitaji ya kampeni zake.

Uwazi wa mapato na matumizi

Sheria hii inaweka sharti la uwazi katika mapato na matumizi ya vyama na wagombea kwa ajili ya uchaguzi kabla, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Sheria hii pia inaelekeza utaratibu wa kufuatwa na vyama vya siasa na wagombea kutoa taarifa zao za mapato na matumizi ya uchaguzi, kama ilivyobainishwa katika kifungu cha 9(1) ambacho kinasema
“Mgombea atatakiwa kutoa taarifa ya fedha alizonazo na anazotarajia kupata na anakusudia kuzitumia kama gharama za uchaguzi ndani ya siku saba (7) baada ya siku ya uteuzi.”

Taarifa hizo zitawasiliskwa kwa Katibu Mkuu wa chama kwa mgombea wa nafasi ya Urais na kwa mgombea wa nafasi ya Ubunge taarifa zake ataziwasilisha kwa Katibu wa Chama wilaya.

Kila chama cha siasa kinachoshiriki katika uchaguzi ni lazima ndani ya siku thelathini (30) baada ya siku ya uteuzi wa wagombea kufanywa na Tume ya Uchaguzi kitoe taarifa kwa Msajili juu ya fedha zote ambazo kinakusudia kutumia kama gharama za uchaguzi; na kutumia kwa kuwadhamini wagombea wa chama hicho zikiwa ni kama gharama za uchaguzi.

No comments:

Post a Comment