Wednesday, July 28, 2010

Kanali Farrah atumia 99m/- kuimarisha chama, maendeleo ya jimbo Rahaleo

UPIGAJI kura ya maoni kwa wagombea Ubunge na Uwakilishi kwa tiketi ya CCM, itafanyika Agosti 1, siku moja tu baada ya Wazanzibari kupiga kura ya maoni kuhusu mfumo mpya wa serikali.

Kura hiyo inafanyika huku majimbo yakiwa yamefurika wagombea, hali ambayo haijawahi kutokea katika historia ya chama hicho.

Wagombea wa zamani wamekuwa wakijaribu bahati zao kwa mara nyengine tena huku wapya nao wakitaka kuingia kwa mara ya kwanza.

Miongoni mwao yumo Kanali mstaafu wa Jeshi, Saleh Ali Farrah, anaegombea tena nafasi ya Ubunge katika jimbo la Rahaleo.

Kanali Farrah anawania nafasi hiyo akiwa na matarajio makubwa ya kushinda, hasa kutoka na juhudi zake kubwa alizochukua katika kulijenga kimaendeleo jimbo la Rahaleo pamoja na chama cha Mapindunzi kwa ujumla.

Farah anasema, amefanya mengi ya kujivunia na ya kupigiwa mfano kwa wananchi wa Rahaleo, akisema maendeleo yaliyofikiwa hayajawahi kuonekana katika miaka kadhaa iliyopita.

Kanali Farrah anasema katika kipindi chake cha miaka mitano cha kuwatumikia wananchi wa Rahaleo, ametumia jumla ya shilingi milioni 99 kwa ajili ya kuleta maendeleo ya jamii, elimu, afya, michezo na kuimarisha shughuli za chama.

Farrah katika kipindi chake kilichomalizika pamoja na mambo mengine, ameweza kulipa posho kwa watendaji wa chama kila mwezi kati ya shilingi 10,000 na 30,000 kwa ngazi ya matawi, wadi na jimbo.

Malipo hayo ameyafanya katika kipindi cha miezi 56, ambayo yamemugharimu shilingi milioni 13,440,000.

Katika michango ya kuimarisha chama, Farrah kila mwezi amekuwa akitoa mchango wa shilingi 70,000 makao makuu ya CCM Kisiwandui, ambapo kwa Mkoa wa Mjini Magharibi amekuwa akichangia shilingi 40,000 wakati kwa wilaya ya mjini amekuwa akichangia shilingi 20,000 na kufanya jumla ya pesa alizochangia katika kipindi cha miezi 56 kufikia milioni 7,280,000.

Hakuishia hapo, kwa upande wa matembezi ya mshikamano, Kanali Farrah amechangia kila mwaka shilingi 200,000 na kufanya idadi ya fedha alizochangia katika matembezi hayo kufikia shilingi 1,000,000.

Katika uimarishaji wa maskani kaka ya Kisonge, Kanali Farrah amechangia shilingi 1,000,000 kwa maskani hiyo na kiasi kama hicho kwa maskani ya Kachorora ambazo ni maskani zenye nguvu kwa Zanzibar.

Akizungumzia uimarishaji wa wadi na jimbo, Farrah alisema amechangia mashine ya fotokopi kwa kila wadi ya jimbo hilo, huku Wadi ya Rahaleo ambao ina matawi matatu ikipatiwa shilingi 2,000,000 wakati Wadi ya Mlandege ambayo ina matawi manne akichangia shilingi 4,000,000.

Kanali Farrah, amekwenda mbali zaidi hata nje ya jimbo lake, anasema katika kufanikisha uchanguzi mdogo wa Magogoni, alichangia shilingi 1,000,000 wakati katika mfuko wa Mkoa wa kufanikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 tayari ameshachangia shilingi 5,000,000 huku mfuko wa wilaya akichangia shilingi 1,500,000.

Katika matengenezo ya matawil ya Mwembeshauri, Rahaleo na tawi la Makadara, Kanali Farrah amechangia shilingi 9,750,000 huku katika daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza, mwanajeshi huyo wa zamani alichangia shilingi 1,500,000 na awamu ya pili kiasi kama hicho cha fedha na kufanya idadi ya pesa alizochangia kufikia shilingi 3,000,000.

Ili jamii iweze kupata elimu bora, Kanali Farrah pia hakuwa nyuma akiamini kama kiongozi wa jimbo la Rahaleo huo ni wajibu wake.

Katika suala hilo, amechangia jumla ya shilingi 10,120,000 ikiwa ni pamoja mchango kwa wanafunzi wa michepuo wa skuli zilizomo ndani ya jimbo lake, tunzo kwa walimu, uchimbaji wa kisima kwa ajili ya wanafunzi na kumalizia ujenzi wa skuli ya msingi ya makadara.

Kwa kuwa Farrah pia ni mwanamichezo, muda wake mwingi amekuwa akiitumia kwa hali na mali kusaidia wanamichezo.

Tayari ametoa jezi seti moja yenye thamani ya shilingi 450,000 kwa klabu ya Mwembeshauri na klabu ya Rangers ya Makadara ambayo ilikabidhiwa seti ya jezi yenye thamani ya shilingi 250,000.

Aidha ametoa seti tatu za jezi kwa timu ya Jimbo na huduma nyengine kwa timu hiyo zenye thamani ya shilingi 4,500,000.

Mbali ya juhudi hizo alizochukua, pia amekuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama.

Katika nyanja hiyo, amechipa visima viwili katika Wadi ya Rahaleo kilichogharimu shilingi 3,000,000 na chengine Mwembeshauri ambacho kimegharimu shilingi 3,000,000.

Visima hivyo vyote vinatoa huduma kwa wananchi wa maeneo hayo kwa wakati wote.

Farrah pia amekiwa akiumwa na tatizo kwa watu wenye ulemavu; tayari amenunua viti vya walemavu kwa gharama ya shilingi 17,500,000 kuwasaidia wananchi ndani ya jimbo lake.

Katika kuvisaidia vikundi vilivyoanzishwa katika jimbo lake, Mbunge huyo anaemaliza muda wake ametumia wastani wa shilingi 1,500,000 kwa vikundi 15 kufungua vitabu vya benki ili kuweza kuendeleza shughuli zake.

Kwa watu wenye matatizo binafisi, Farrah ametumia shilingi 17,340,000 na anaamini bila ya msaada wao kumchagua katika uchaguzi wa mwaka 2005 asingeweza kutekeleza hayo.

Kanali Farrah anasema anarejea tena kuomba ridhaa ya wananchi jimboni akiwa msafi na akiamini kwamba amekamilisha yale ambayo wananchi walitaka ayatekeleze.

Farrah amewahakikishia wananchi wa Rahaleo kwamba, endapo watamchagulia tena watarajie maendeleo mapya ambayo yatakidhi mfumo wa sasa wa ilimwengu.

Farrah alizaliwa Juni 5, 1949 na kuanza elimu ya msingi katika skuli ya St Joseph Convent mwaka 1958 na kuhitimu mwaka 1965.

Baadae alijiunga na skuli ya Lumumba kuanzia mwaka 1966 hadi mwaka 1969 kabla ya kujiunga na chuo cha kijeshi mwaka 1980 hadi mwaka 1981.

Katika utumishi Farrah amelitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika ngazi mbali mbali kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1990 alipoteuliwa kuwa mlinzi wa Rais wa Zanzibar hadi mwaka 1999.

Katika kukitumikia chama alijiunga na ASP mwaka 1972, mbapo mwaka 1975 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa tawi la ASP hadi mwaka 1976.

Mwaka 1977 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM hadi mwaka 1989.

No comments:

Post a Comment