Sunday, July 4, 2010

Balozi Karume asema hana tatizo na serikali ya Umoja wa Kitaifa

Na Juma Khamis

BALOZI wa Tanzania nchini Italia, Ali Abeid Karume (60), amesema kura yake ya NDIO au HAPANA katika kura ya maoni kuamua mfumo wa uendeshaji serikali, itategemea nani atapitishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) Julai 9 kuwa mgombea Urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao.

Kura ya maoni kuhusu mfumo wa serikali itafanyika Julai 31, takribani siku 20 baada ya CCM kuchagua mgombea wake wa Urais.

Balozi Karume aliyasema hayo hoteli ya Serena alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa kutoka chama chake kuteuliwa kuwa mgombea Urais wa Zanzibar.

“Tufikirie kwa makini kabisa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa na mimi hili naliunga mkono lakini kura yangu ya NDIO au HAPANA itategemea mgombea wa Urais wa CCM atatoka upande upi,” alisema Karume.

Hata hivyo, alisema ni matarajio yake kwamba CC itawatendea haki wagombea wote na kuchagua mwanachama ‘asilia’ wa Zanzibar kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar.

“Tutashinda tukichagua kiongozi bora na si bora kiongozi,” alisema Balozi Karume huku akisisitiza kuwa kama atapitishwa na kushinda basi wala rushwa wataendelea tu kubakia na utaifa wa Zanzibar lakini wajiandae kutafuta nchi yao ya kuishi, akimaanisha kwamba atakabiliana kwa nguvu zake zote na mafisadi.

Akizungumzia nia yake ya kugombea kuteuliwa katika nafasi ya Urais, Balozi Karume ambae ni mdogo wa Rais wa sasa wa Zanzibar Amani Abeid Karume alisema: “Nimechangia vya kutosha Tanzania na sasa muda umefika kuchangia nchini kwangu. Nia ninayo, sababu ninayo na uwezo ninao, nakiomba chama kinipitishe.”

Balozi Karume ambae ana kadi ya CCM No. AA 270259 aliyoipata Februari 5, 1977 msukumo mkubwa anaojivunia ni kuungwa mkono na vijana hasa wanawake.

“Kabla ya kuchukua fomu nimeshauriana na wengi wakiwemo Marais wastaafu lakini msukumo nilioupata zaidi ni kutoka kwa vijana na hasa wanawake,” alisema Karume ambae ni mtoto wa pili wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Balozi Karume ambae ana Shahada ya Uzamili (Master Degree) kutoka Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani, aliwahi kusoma pamoja chuoni hapo na Rais wa sasa wa Marekani, Barack Obama wakati huo akichukua shahada ya kwanza aliyopita baada ya kutunukiwa Schorlaship na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1978, ingawa Obama alikuwa nyuma yake kwa mwaka mmoja.

Amesema akipata ridhaa ya wananchi ataongeza kasi kuimarisha uchumi na pato la mwananchi wa kawaida hasa kwa vijana.

No comments:

Post a Comment