Monday, April 18, 2011

Kuondolewa muswada wa katiba ni ushindi wa kwanza kwa Watanzania

WIKI iliyopita serikali ya Tanzania ilikubali kuuondoa muswada wa katiba baada ya Kamati ya Sheria na Katiba ya Bunge kuomba marekebisho kadhaa ikiwemo kuletwa kwa lugha ya Kiswahili, na kutangazwa kwenye magazeti ili uwafikie Watanzania wengi popote walipo.
Kuondolewa kwa muswada huu, ni ushindi mkubwa wa kwanza kwa wananchi, ambao tayari walishaanza kampeni mbali mbali za kuupinga kiasi cha kufikia hatua ya kuchanwa na kuchomwa moto.
Ni dhahiri kwamba muswada huu ulikuwa ukijadiliwa na Wabunge bila ya wananchi kushirikishwa, kwani ni kundi dogo sana la wananchi ndio lililopata fursa ya kuuona au kuusoma.
Kwa mara ya kwanza, tuliushuhudia wakati Kamati ya Sheria na Katiba ya Bunge, ilipofanya mikutano yake miwili hapa Zanzibar tena kwa muda mfupi sana, lakini kundi kubwa lililo nyuma yetu, lilikuwa likisikia tu.
Hatua ya Kamati ya Sheria na Katiba, kuomba muda zaidi ni ishara kwamba imekisikia kilio cha wananchi walio wengi, kwamba muswada haujawafikia na hivyo Bunge lisingepaswa kuujadili.
Kwa mfano katika maeneo mengi ya Tanzania, hasa Unguja na Pemba wananchi wengi walikuwa hawafahamu kinachoendelea; ndio walikuwa wakifuatilia vyombo vya habari lakini maudhui ya muswada huu walikuwa hawayaelewi kutokana na kikwazo cha lugha.
Lugha iliyotumika kwenye muswada huo ni Kingereza, wakati wananchi waliopelekewa wengi wao hawafahamu kabisa lugha ya kingereza, hivyo wasingeweza kujadili kitu wasiochokifahamu.
Kuvishirikisha vyombo vya habari kutangaza muswada huu ndio hatua pekee ya kutafuta mawazo ya wananchi ambao ndio wanaoguswa na mabadiliko ya katiba.
Ingekuwa dhambi kubwa kwa Wabunge ambao wamechanguliwa na wananchi kujadili muswada ambao hauna baraka zao na kitendo hichi kingekuwa cha usaliti mkubwa kwa wananchi.
Mbali na marekebisho hayo, Tume ya Katiba na Sheria, pia inapaswa kuyazingatia yote yale iliyokusanya katika kipindi kifupi kutoka kwa wananchi, hasa yake kutoka upande wa Zanzibar.
Tunataka kuitanabahisha Tume kuwa hakuna cha kubeza katika michango ile, vyenginevyo yanaweza kutia doa kubwa yatakapopuuzwa kiasi cha kuwepo kampeni ya ‘Yes’ na ‘No’, kama ilivyotokea Kenya.
Aidha, mtakapopeleka muswada huu kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya kuchapwa msiwasahau watu wenye ulemavu, hasa watu wasioona kwa sababu na wao kama raia wa Tanzania wana haki ya kutoa mchango kama yalivyo makubndi mengine.

No comments:

Post a Comment