Monday, April 18, 2011

Tupambane na wanaowapa ujauzito watu wenye ulemavu kisha wakawatelekeza

MATUKIO ya wanawake walemavu kupewa ujauzito na kisha kutelekezwa yanaongezeka kila uchao katika jamii yetu.
Tumeyasikia mara kadhaa na mengine yamekuwa yakiwakumba ndugu zetu wa karibu katika nyumba tunazoishi.
Watu wenye ulemavu wamekuwa wakirubuniwa na wanaume wenye tamaa ya ngono na baada ya kupata wanachohitaji wanawakimbia na kuwaacha katika mateso makubwa ya kulea ujauzito.
Ndio ni haki na ni wajibu kwa mlemavu kuwa na familia yake, lakini siyo kwa kwa kupewa ujauzito vichochoroni na kisha kutelekezwa na kuachwa katika mazingira magumu ya maisha.
Walemavu wengi hawana elimu, hawana ajira na mazingira yao ya kujipatia kipato ni magumu mno kiasi cha kuwafanya wakati mwengine kuishi ama kwa msaada wa ndugu zao au kujitahidi kufanya kazi hata zile ngumu huku wengine wakigeuka kuwa omba omba.
Bila shaka hakuna atakaebisha kuwa watu wenye ulemavu ni miongoni mwa omba omba katika mitaa yetu mengi, hii yote ni kwa sababu tumewasahau.
Wanapoongezewa tatizo jingine zito kama la ujauzito na kisha kutelekezwa ni kuwazidishia machungu kiuchumi na kisaikolojia wao pamoja na familia zao.
Ni ukatili na ukosefu wa imani kwa binadamu kuwa na tamaa kiasi cha kumbebesha ujauzito mwanamke mwenye ulemavu na kisha kumtoroka au kuukana ujauzito.
Tabia hii sio tu inapigiwa kelele kwa watu wenye uleamvu, lakini pia haipendezi kufanyiwa watu wengine wasiokuwa na ulemavu, lakini linapotokea kwa watu wenye ulemavu huwa ni machungu zaidi kutokana na maumbile yao.
Kitendo cha kufanya mapenzi kinapaswa kuwa shirikishi kwa maana ya kuwahusu moja kwa moja wazazi na hivyo ridhaa ya kufanya tendo hilo lazima ipatikane kwa wote na pale inapotokea mama akapata ujauzito ni wajibu wa baba nae kuwajibika hadi ujauzito huo utakapozaliwa.
Hivyo inapotokea mmoja kuachiwa jukumu hilo pekee linakuwa ni tatizo si kwake tu, hata kwa kiumbe atakayezaliwa kwani atakuwa amekosa matunzo ya baba.
Sasa jukumu hilo linapoachwa kwa mwanamke mwenye ulemavu hali inakuwa ni ya mashaka sana kwa sababu uwezo wake wa kumlea mtoto huyu ni mdogo na hasa pale atakapokosa msaada wa baba na mama kama wataamua kumtenga.
Huu ni ukatili mkubwa kwa kuwa kitendo hicho kina matokeo mabaya kwao kwa sababu hawana uwezo wa kujitetea wasifanyiwe hivyo, hawana uwezo wa kiuchumi wa kumudu ulezi wa mimba wala mtoto atakayezaliwa na isitoshe hawana uhakika wa mlo wao wa siku na ndio maana nikasema wanapoachiwa jukumu hilo maisha yao yanakuwa ya mashaka makubwa.
Ni wanaume wachache ambao huwa na mapenzi ya dhati kiasi cha kuoa au kulea mimba wanazowapa wanawake wenye ulemavu, lakini wanahesabika kwa sababu wengi wanaamini kufunga ndoa na mlemavu ni mzigo.
Asilimia kubwa huwarubuni na kuwapa mimba na kisha kutokomea; tumeshawahi kusikia taarifa za hata wagonjwa wa akili kupewa ujauzito na kisha kutelekezwa.
Nilishawahi kuzungumzia adha nyingine wanazokumbana nazo wenzetu walio na ulemavu, kwa kiwango kikubwa wamekosa mazingira rafiki ya miundombinu kama majengo, usafiri na elimu.
Tunapozungumzia kutelekezwa kwa walemavu, waathirika wakubwa ni wanawake kwa sababu ndio walioko katika tabaka la kunyanyaswa na kukosa haki zao za msingi.
Kukataliwa, kupewa ujauzito, kubakwa, kutelekezwa ,kukoseshwa elimu na ajira ni madhila machache kati ya mengi yayowakumba watu wenye ulemavu.
Hizi ni changamoto kubwa ambazo kama hatutakubali kuzifanyika kazi, azma yetu ya kupambana na umaskini na unyanyasaji wa kijinsia haitafanikiwa.
Kwa upande wetu watu wenye ulemavu, wawe tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola, kuwafichua wale wenye tabia ya kuwapa ujauzito walemavu, badala ya kuendelea na tabia ya kuwastiri kwani kuwaficha wahalifu ni sawa na kuchangia kufanya uhalifu.
Aidha Jumuiya za watu wenye ulemavu kama UWZ, zinapaswa kuandaa mikakati endelevu ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wanachama wenu kuweza kujiamini na kuhakikisha hawarubuniwi na wapenda ngono kiasi cha kubebeshwa ujauzito na baadae kutelekezwa.

1 comment:

  1. Wanaume wanaokamata wake zao ugoni wanawaka asila mbaya na kuamua kutoa maamuzi mabaya kwa walalamikiwa mfano makosa ya jinai,kwani wanaona wamepunguziwa hadhi na utu wao wamezalaulika,wamenyanyasika na kujiona si kitu tena Hivyo kuwepo na adhabu kali ili kuondoa matendo hayo ya ugoni na kulinda ndoa za watu.pia watoto wanaozaliwa ndani ya ndoa ndoa ikivunjika upoteza mwelekeo wa maisha kwani malezi na makuziya watoto ni ya wazazi wote kwa pamoja.Naomba azabu kwa wasababishi iwe kali sana.

    ReplyDelete